24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 28, 2023

Contact us: [email protected]

Wabunge katika mtihani kupitisha muswada wa Jinsia

JE, wabunge Kenya leo watapitisha Muswada wa Jinsia utakaoshuhudia ongezeko la idadi ya wabunge wanawake, au tusubiri kushuhudia sarakasi bungeni?

Hii itakuwa mara ya tatu muswada huo unaletwa bungeni baada ya kukumbana na vikwazo. Ni miaka minane sasa tangu Katiba Mpya kupitishwa na Muswada wa Jinsia bado haujatekelezeka. Kwa mara ya kwanza muswada huo uliwasilishwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Samuel Chepkonga lakini waliokuwa wanaupinga walidai hakukuwa na muda maalumu kuanza kutekelezwa hivyo ilihitaji kwanza ushauri wa Mahakama ya Juu.

Kwa mara ya pili tena, Kiongozi wa Walio wengi bungeni, Aden Duale (Mbunge wa Garissa Township) aliwasilisha muswada huo lakini ikishindikana baada ya wabunge 178 kati ya 199 kuunga mkono. Wabunge wengine 13 waliupinga na watano hawakupiga kura kabisa.

Seneta wa zamani, Judy Sijeny, naye alijaribu kushinikiza muswada huo kupitia Bunge la Seneti mwaka jana lakini hali ikawa hivyo hivyo. Alishindwa kupata idadi inayohitajika ili muswada huo uende hatua inayofuata baada ya wabunge 23 tu kati ya 67 ndiyo waliokwemo wakati wa kupiga kura ilhali ilihitajika angalau maseneta 45.

Mshikemshike unasubiriwa bungeni leo huku baadhi ya Wakenya wakihoji muswada huo ni kwa faida ya nani? Kuna wale wanaodai tayari gharama ya maisha ipo juu na kwamba kuongeza idadi ya wabunge ni kumuumiza Mkenya wa kawaida.

Aliyekuwa mgombea urais ambaye pia ni kiongozi wa Chama cha Thirdway Alliance, Ekuru Aukot ni miongoni mwa wanasiasa wanaoupinga muswada huo akisisitiza hauendani na malengo ya Rais Uhuru Kenyatta anayeonesha kujali kuhusu gharama kubwa inayohitajika kutekeleza Katiba Mpya.

“Tunawaomba wabunge wetu waache kujifanya kutokana na kile kinachoendelea kwenye Bunge kuhusu kubadili Katiba ili kuleta usawa kati ya wanaume na wanawake kupitia Muswada wa Duale (Mbunge wa Garissa Township aliyewasilisha muswada huo),” alisema.

Japo Aukot anakubali ipo haja ya uwepo wa asilimia 50 ya wanawake bungeni na kwamba pia wanastahili heshima na usawa lakini sio kupitia muswada huo ambao anasema una malengo tofauti.

Wachambuzi wengine wa siasa nao wanadai licha ya idadi ya wabunge wanawake ambao kwa sasa wapo bungeni, bado wameshindwa kutekeleza mahitaji hususani ya wanawake wenzao na kuongeza haitasaidia idadi ya wanawake bungeni kuwa sawa na wanaume.

Kwa mtazamo wao wangeridhika laiti muswada huo ungeangazia zaidi kuongeza idadi ya wabunge watakaowakilisha watu ambao sauti zao hazisikiki kama vile walemavu na jamii zenye watu wachache Kenya.

Licha ya wabunge kuchangia hoja ya muswada huo na kuonesha kuunga mkono, kuna dalili akidi ikashindwa kutimia kama ilivyokuwa muswada wa kubadilisha tarehe ya kupiga kura ambayo ingewaongezea wabunge muda wa kushikilia nyadhifa zao. Inahitajika wabunge 233 wa Bunge la Taifa na 45 wa Bunge la Seneti kupitisha muswada huo.

Lakini pia tunaweza tukashuhudia kama yale yaliyotokea wakati wa upitishaji wa Muswada wa Fedha 2018 ambapo wabunge wengi waliupinga lakini Spika akatangaza wabunge waliupitisha. Haya yote yalitendeka bungeni licha ya Rais Uhuru na kinara wa upinzani Raila Odinga kuwasihi wabunge wao kuupitisha Muswada wa Fedha 2018.

Tayari Rais Uhuru, Naibu Rais William Ruto, Kiongozi wa ODM Raila na mwenzaka wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka wamewasisitizia wabunge kuupitisha Muswada wa Jinsia kama inavyotakiwa kikatiba.

Jana Rais Uhuru alitarajiwa kukutana na wabunge wa Chama cha Jubilee kuwashawishi waupitishe muswada huo huku Raila naye akikutana na wabunge wa ODM kwa jambo hilo hilo. Ni muswada ambao ukipitishwa utashuhudia Bunge likiwa na thuluthi mbili ya wanawake.

Kuna watu wanahoji kwanini Rais Uhuru anashinikiza muswada huo upitishwe wakati baraza lake la mawaziri nalo halijakidhi thuluthi mbili ya mawaziri wanawake? Hata hivyo kwa mujibu wa Katiba iliyopitishwa miaka minane iliyopita, kinachohitajika zaidi ni usawa uwepo bungeni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,222FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles