26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge Chadema wajiweka Karantini siku 14

 RAMADHANI HASSAN -DODOMA 

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema wabunge wote wa chama hicho kwa wiki mbili hawatahudhuria vikao vya Bunge, ikiwa ni sehemu ya kujipima kama wameathirika na corona na kama wameathirika basi wasiisambaze watu wengine. 

Uamuzi huo wa Chadema, umeungwa mkono na baadhi ya wanaharakati pamoja na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, aliyetaka vyama vingine kufuata njia ya Chadema katika kudhibiti ugonjwa huo. 

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Zitto aliandika “natoa pongezi za dhati kwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni ndg. HYPERLINK “https:// twitter.com/freemanmbowetz” @ freemanmbowetz kwa uamuzi huu wa kiuongozi. Hii ni hatua muhimu sana na itachangia kwa kiasi chake kuokoa maisha ya watu. Nawashauri viongozi wengine wa vyama vyenye wabunge kuelekeza wabunge wao kujitenga (isolation).” 

Chadema jana walitoa tangazo lao muda mfupi baada ya kutangazwa kifo cha Balozi Augustine Mahiga, ambaye anakuwa mbunge wa tatu kufariki dunia ndani ya siku 11. 

Waliomtangulia ni Mbunge wa Viti Malimu (CCM), Mchungaji Getrude Rwakatare aliyefariki dunia Aprili 20 na Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndasa aliyefariki dunia Aprili 29. 

Licha ya kwamba mamlaka husika hazijatangaza kama wabunge hao walifariki kwa corona, jana Mbowe alitoa taarifa kwa umma akisema chama hicho kimeendelea kupokea kwa masikitiko taarifa za misiba ya wabunge na Watanzania wengine inayosababishwa na kusambaa kwa COVD-19. 

“Kama ambavyo tumeshauri mara kadhaa, ni dhahiri hatua za ziada za dharura zinapaswa kuchukuliwa kupunguza kasi ya maambukizi na hivyo kuokoa kadri iwezekanavyo maisha ya Watanzania. 

“Wakati tukisubiri wenye mamlaka kuchukua hatua hizo na maadam Chadema tulishasisitiza kila mmoja wetu kuwa mstari wa kwanza wa kujikinga na kukinga wenzake, chama kinatoa maelekezo yafuatayo kwa wabunge wake wote. 

“Wabunge wote wa Chadema waache mara moja kuhudhuria vikao vya Bunge au Kamati za Bunge, wabunge wote wa Chadema kutofika kabisa katika eneo lote la Bunge Dodoma na Dar es Salaam, wabunge 

 wote wa Chadema kujiweka karantini kwa muda usiopungua wiki mbili. 

“Tunasisitiza wabunge wetu walioko Dodoma wasiende majimboni, mikoani bali wabaki Dodoma kwenye karantini hadi itakapothibitika wao ni salama au kupata maelekezo mengine yoyote yaliyo rasmi,”ilieleza taarifa hiyo. 

Pia Chadema inawasihi wabunge wa vyama vingine kutafakari kama ni salama kuendelea na vikao vya Bunge katika mazingira yaliyopo. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Chadema walitaka Bunge kusitisha shughuli zake kwa siku 21 ili wabunge na watumishi wa Bunge wakae karantini. 

Pia ilitaka wabunge, watumishi wa Bunge na familia zao wapimwe ili kubaini ni wangapi wana virusi hivyo ili hatua sitahiki za kitabibu zichukuliwe.

Chadema pia walitaka kamati mahususi za Bunge hususan Kamati ya Huduma za Bunge na Kamati ya Uongozi zifanye vikao vyake kwa njia ya mtandao ili maamuzi muhimu kuhusu utawala na mwenendo wa Bunge yaweze kufanyika. 

“Chadema inaendelea kusisitiza kwa watanzania wote kuwa mstari wa kwanza wa kinga.Tunasisitiza ni uzembe kasubiri kufanyiwa kinga na mwenzio.Anza wewe,”ilieleza taarifa hiyo. 

Mahiga ambaye hadi umauti unamfika alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria, anakuwa ni waziri wa kwanza kufariki dunia tangu Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakeni Oktoba 2015 na anakuwa mbunge wa tisa kufariki tangu kuanza kwa Bunge la 11. 

 Mbali na Balozi Mahiga ambaye ni mbunge wa kuteuliwa na Rais, wengine waliofariki mbali na Lwakatare na Ndasa ni aliyekuwa Mbunge wa Newala Vijijini (CCM), Rashid Akbar, Stephen Ngonyani (Maji marefu) aliyekuwa Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Dk. Elly Macha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Hafidh Ally Tahir aliyekuwa Mbunge wa Dimani (CCM), Leonidas Gama aliyekuwa Mbunge wa Songea Mjini (CCM) na Kasuku Bilago aliyekuwa Mbunge wa Buyungu, (Chadema). 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles