26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wabunge CCM wapinga mikakati ya Ukawa

bungeniNa Kulwa Mzee, Dodoma

BAADHI ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamesema maazimio ya wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuwasusia hata katika salamu ni utoto na hiyo si siasa ni uadui.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jana katika viwanja vya Bunge, walieleza kusikitishwa na kuhuzunishwa na hatua iliyofikiwa na wabunge hao.

Mbunge wa Korogwe Vijijini, Hilary Ngonyani maarufu ‘Profesa Maji Marefu’ (CCM), alisema kwa kuwa wameshaamua kususa hata kusalimiana kuna haja ya kujipanga upya.

“Hayo wanayofanya yalikuwa ndani ya Bunge, siasa zilitakiwa kuishia ndani ya Bunge, sasa wanayatoa nje sijui itamsaidia nani, hii siyo siasa ni uadui.

“Mambo yanayofanyika Zanzibar wanatuletea bungeni, wamejitoa katika magrupu hata ya WhatsApp ambayo mara zote tumekuwa tukifahamishana nini kinaendelea na kujadili vitu kwa pamoja.

“Nilimshuhudia Mbunge wa Viti Maalum, Anna Lupembe (CCM),  akimsalimia Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), hakuitika salamu wala hakumpa mkono,”alisema Maji Marefu.

Alisema wanakoelekea lazima wakae meza moja kutafuta suluhu kwa sababu  hali hiyo ina athari kubwa katika masuala ya maendeleo.

Mbunge wa Mafinga, Cosato Chumi (CCM) alisema wabunge wanategemewa kwa kiasi kikubwa kutokana na uwakilishi wao katika majimbo.

“Kwa kweli wanachofanya wenzetu ni utoto, sina lugha nyingine ya kusemea hili, haya yanayofanywa yanashuka chini kwa wananchi.

“Tukifanya mema yanashuka kwa wananchi pia, haya ya kubaguana sisi Watanzania hatuna, sina neno jingine, huu ni utoto wa kupindukia,” alisema.

Alisema kama wameshafikia hatua hiyo wajitafakari upya kwa kuangalia waliokuwa nyuma yao watafanya nini.

“Uamuzi waliofikia una athari kubwa, ni jambo la kuhuzunisha na kusononesha hivyo wanatakiwa kuangalia je, lina tija kwa jamii ama laa?” alisema Chumi.

Alisema wabunge wanatakiwa kuangalia mustakali wa taifa na katika mwezi huu wa toba kama mtu alikwazwa asamehe ili wasonge mbele kwa sababu  zama za jino kwa jino siyo hizi.

Akizungumzia hatua yao, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CCM), alisema waliamua kufanya hayo kwa sababu wakiwasilisha masuala ya msingi yanachukuliwa  kwa mzahamzaha.

“Tumeamua kujitenga nao, hatuoni haja ya kushirikiana nao kwa sababu katika vitu vya msingi wao wanaleta utani,” alisema Msigwa.

Juzi, wabunge wa Ukawa waliazimia kwa pamoja kutoshirikiana na wenzao wa CCM kwa madai kwamba hawatendewi haki na  Naibu Spika, Tulia Ackson.

Kwa kuonyesha hisia zao bungeni, juzi waliingia bungeni saa tatu asubuhi lakini walitoka huku wakiwa wamebandika plasta kwenye midomo yao baada ya Dk. Tulia kuingia.

“Sisi tuliingia tukiwa hatujajifunga plasta, plasta tuliingia nazo, baada ya dua ya kuliombea Bunge tukazifunga na kutoka nje,” alisema Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea(Chadema).

Wabunge hao walisusa futari iliyoandaliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hivi karibuni, na kuamua kuandaa futari yao katika Hoteli ya African Dream huku wakigoma kuwaalika wabunge wenzao wa CCM.

“Hayo ni makubaliano ya wiki mbili, baada ya wiki mbili tutajua tumefikia uamuzi gani katika hatua za kutafuta kupata haki yetu,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa ambaye ni Mbunge wa Vunjo, James Mbatia( NCCR-Mageuzi), alisema Naibu Spika, Dk. Tulia Ackon,  amekuwa akishiriki katika vitendo vya uchochezi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles