26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge CCM wamkingia kifua Naibu Spika  

tuliaAZIZA MASOUD NA KHAMIS MKOTYA, DODOMA

WABUNGE watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamepinga kusudio la wabunge wa Kambi ya Upinzani la kumwondoa katika madaraka yake Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.

Wakizungumza na waandishi wa habari bungeni Dodoma jana, wabunge hao, Profesa Anna Tibaijuka wa Muleba Kusini, Joseph Kakunda wa Sikonge na Mbunge wa kuteuliwa, Dk. Abdallah Possi ambaye pia ni Naibu wa Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, walisema uamuzi wao wa kuibuka hadharani kupinga kusudio la hoja ya kumwondoa Dk. Tulia kwenye wadhfa wake hauna shinikizo wala msukomo wowote bali utashi wao binafsi.

Akizungumza kwanza, Dk. Possi, alisema yeye binafsi haoni kama kuna mgogoro baina ya Dk. Tulia na wabunge wa kambi ya upinzani.

Dk. Possi alisema hoja ya kutaka kumwondoa Dk. Tulia ni dhaifu kwa sababu kiti cha spika kinaendeshwa kwa mujibu wa kanuni.

“Hii si mara ya kwanza kwa Bunge hili kwa mtu kutolewa nje wala si mara ya kwanza kwa wabunge kuadhibiwa kwa wabunge kutolewa nje au kufukuzwa.

“Alichokifanya Naibu Spika siku ile ni kwa mujibu wa kanuni. Kama watu hawakuridhika na uamuzi ule kanuni zinaruhusu kuyakatia rufaa. “Hakuna uhalisia wowote kati ya kilichotokea bungeni na kinachoendelea, mimi naamini kinachoendelea ni harakati za kisiasa na uwepo wa kikundi cha watu wanaoamini katika migogoro binafsi,” alisema Dk. Possi.

Alisema kiti cha spika kina uwezo wa kukatiwa rufaa kuhusu uamuzi kinaotoa kwa mujibu wa kanuni ya 5 (4) na lakini si kukigomewa.

Dk. Possi alisema wabunge wa upinzani waliopeleka hoja hiyo wamehamaki bila sababu za msingi na inawezekana wanatafuta njia ya kuonekana.

“Hii ni sawa na mtu unaingia na motion (dhamira) fulani unataka kutoka unashindwa kwa sababu mbalimbali,” alisema Dk Possi.

Kwa upande wake, Kakunda, aliwashangaa wabunge wa upinzani wanaolia sasa badala ya wenzao waliofukuzwa bungeni.

“Unajua popote pale hata ukienda mahakamani kwenye mpira kuna sheria zake na kanuni zake na hata Bunge ni hivyo hivyo. Kama ilivyo kwenye mpira wa miguu mtu akikosea anapewa kadi ya njano na Bunge nalo ni hivyo hivyo, bungeni mtu akikosea anapewa kadi ya njano kwa namna yake.

“Mtu akikosa kosa kubwa anapewa adhabu kubwa. Hivyo wabunge nao wanapaswa kukubali adhabu bila kuchapwa viboko. Hapa ninachokiona watu wanatafuta umaarufu nje ya Bunge ambao hauna msingi ili lawama zote ziende CCM,” alisema Kakunda.

Naye Profesa Tibaijuka alisema kusudio hilo la wabunge wa upinzani ameliangalia kwa mtizamo wa kijinsia na kubaini kwamba ni vita dhidi ya mwanamke.

“Naibu Spika ni msomi na anaweza, sisi wanawake tunaweza na ndiyo maana nasema kwa namna yoyote ile Dk. Tulia ni msomi na anaweza huwezi kubisha mumpende msimpende, lakini huo ndiyo ukweli. Nionavyo mimi kinachoendelea ni ishara ya kumdharau mwanamke na siku zote wanawake wanajadiliwa vibaya.

“Bunge liliongozwa na Samuel Sitta linasifiwa, kwani katika Bunge hilo wabunge hawakuwahi kutolewa nje? Hawakuwahi kusimamishwa? Hawakuwahi kukatwa posho? Nendeni kwenye Hansard (kumbu kumbu rasmi za Bunge),” alisema Profesa Tibaijuka.

 Juzi, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa msimamo wa wabunge wa upinzani kususia vikao vinavyoongozwa na Dk. Tulia hauwezi kuathiri shughuli za Bunge.

“Sisi hatuoni tatizo la Naibu Spika, labda tatizo lake ni kusimamia vizuri kanuni,  kama wana tatizo naye jingine waseme lakini kama ni kuliongoza Bunge hatuoni tatizo,” alisema Dk. Kashilillah.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles