23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge CCM: Uchumi wa nchi unayumba

bunge1*Wairarua Serikali, mawaziri wa JK wahoji ahadi za JPM
Na Bakari Kimwanga -DODOMA

WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamesema uchumi wa nchi unayumba, huku mawaziri walioteuliwa na Rais Dk. John Magufuli wanaogopa kumweleza ukweli kiongozi huyo kuhusu hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi.

Kutokana na hali hiyo, wamesema ipo haja kwa Serikali kujitafakari na mipango yake mingi ambayo imekuwa na ugumu katika utekelezaji wake.

Akichangia hotuba ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa ya 2017/18 na Mwongozo wa Kuandaa Bajeti, iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango bungeni jana, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alisema hotuba ya waziri huyo haina jipya ila imerudia mambo yaliyopita ya mwaka 2015/16, huku akihisi nchi hii ni ya watu wa hali ya juu pekee.

Alisema kuwa Waziri Mpango alitakiwa kuichambua ripoti iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB) Oktoba 20, mwaka huu ambayo inaonyesha uchumi wa nchi umezidi kuporomoka hadi kushika namba 139 duniani.
Bashe alisema kilichowasilishwa na Waziri Mpango ni tofauti na hali halisi ya maisha ya kawaida ya wananchi waliopo mitaani.

“Waziri wa Fedha usirudie uliyoyafanya 2016/17, nalisema kwa sababu angalia vitabu vyake hapo, nchi hii si ya Executive Only (si ya watu wakubwa pekee). Unakuja na kitu kilekile, eti eneo la kimkakati Kurasini, huku unataka kuua Kariakoo ili Wachina watumie ile nafasi.
“Jamani hatuwezi kwenda hivyo, boresheni Kariakoo ili mruhusu hawa waswahili walipe kodi, tuacheni kabisa dhana mbaya.

“…Sijui kwa kuwa wewe hukuomba kura na hujui hali ngumu iliyopo mitaani, vijijini fedha hakuna halafu unakuja hapa kusema tunatekeleza. Waziri wa Fedha asipochukua tunayomshauri, tuna jukumu la kuungana bila kujali itikadi zetu humu ndani bungeni,” alisema Bashe.

Alisema ni lazima waziri aangalie sheria za nchi kama zinavutia wawekezaji wote na si wa nje peke yao.
“Ninashangaa sana katika taarifa ya waziri, anasema mazingira na hali ya hewa itakuwa nzuri huku taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), zinasema kuna ukame. Leo hali ya hewa kwa nchi jirani unasema ni nzuri si kweli, kwa 2017/18 nchi zinazotuzunguka zina hali mbaya ya chakula na hata taarifa ya TMA inasema hivyo,” alisema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Solwa, Ahmed Salum (CCM), alisema hivi sasa kuna tatizo la mzunguko wa fedha katika jamii, huku akishangazwa na kauli ya Waziri Mpango ya uchumi kuimarika.
Alisema anashangazwa na taarifa ya kuimarika uchumi, japo bado kuna matatizo ya uchumi, ikiwamo upande wa wawekezaji wanaokuja nchini.
Mbunge huyo alisema hakuna kituo kimoja kwa ajili ya kuhakikisha wawekezaji hawasumbuliwi, lakini bado kuna tatizo Kituo cha Uwekezaji (TIC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao hukaa na nyaraka muda mrefu bila kufanya uamuzi.

“Mambo yamekuwa yakichelewa, kila mtu ana uamuzi, tatizo hili ni kubwa. Tukitaka tushinde kwenye viwanda, sheria lazima ibadilishwe. Baada ya kufanya utafiti wa kina nimebaini kuna tatizo kubwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC). Si kwamba wao ni tatizo, ila sheria tumechukua za nje na ‘kuzi-copy na ku-paste’ kwetu.

“Hali hii imekuwa ni tofauti kabisa, na hili tunashindwa kwenda, tofauti na wawekezaji, na wawekezaji watakaoweza ni wale wa nje wanaokuwa na Dola milioni 50 hadi 200, hawa ndiyo wanakuja kuwekeza.
“Lakini kama ukitaka Watanzania waweze kuinuka kwa sheria tulizokuwa nazo kwa watendaji waonaofanya kazi kwa mazoea bila kuwa na mfumo mzuri, hatuwezi kufika,” alisema.

Alisema hivi sasa kodi ya nchi hata akiambiwa Waziri wa Fedha awasilishe taarifa ukiacha na madeni (areas), kuna watu waliouza magari kati ya manane hadi 10 ndio wamekuwa wakibanwa kulipia kodi.

Salum alisema ikiwa watu hao watalipa na itafika mahali itakwisha, areas zitakuwa zimekwisha na kubaki na makusanyo ya siku hiyo (cash revenue), hapo ndipo itaonekana kutoka Sh trilioni 1.5 na hata kushuka hadi Sh bilioni 800 iliyoachwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

“Rais Kikwete ameacha makusanyo ya Sh bilioni 850, nchi ilikuwa inakwenda na hali ya maisha ilikuwa nzuri na mambo yanakwenda raha kwa kwenda mbele. Sasa Mheshimiwa Magufuli ana ‘vision’ kubwa kwa nchi hii kwa kutamani tutoke kama Thailand ilivyotoka.

“Kukimbiwa na wafanyabiashara wa Zaire (DRC), Waziri wa Miundombinu anajibu kama kwamba yeye ni waziri wa Zaire, anasema wameweka pale ili wakusanye ushuru, inatuhusu nini mambo ya Zaire humu?

“Ile kuwawekea ofisi Wazaire walipe ushuru ndiyo iliyowakimbiza. Kama Rais Joseph Kabila amekuwa hapa kwa Magufuli, alikuwa anataka walipe ushuru hapa angeshindwa? Ndiye aliwaambia waende Beira na Mombasa.
“Toeni Single Custome Territory pamoja na VAT katika mizigo ya wafanyabiashara wa nchi ya Kenya, Msumbiji wamesoma sheria zetu wakaona hawa Watanzania hawaelewi wakatoa hadi check poit kutoka sita hadi mbili.

“Bandari kama ingefanyiwa kazi vizuri ina uwezo wa kuingiza trilioni tano kwa mwaka, leo tunapokea kontena 500,000. Tuifanye kama ‘private’ sekta kwa ajili ya kuleta mapato kwa Serikali yetu. Leo waziri unawabana hadi wenye bodaboda unaacha bandari?” alisema na kuhoji.

Kwa upande wake Mbunge wa Maswa Mashariki, Stanlaus Nyongo (CCM), alisema suala la uwapo wa kodi zaidi ya 41 ni kero kwa nchi kwa sababu zinawaumiza wafanyabiashara wa ndani.

Mawaziri wa JK wahoji ahadi za JPM

Katika hatua nyingine, wabunge wa chama hicho tawala, wamehoji utekelezaji wa ahadi zilizonadiwa na Rais Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana.
Wabunge hao ambao walipata kuwa manaibu mawaziri katika Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, walitaka kujua ni lini ahadi ya kugawa Sh milioni 50 kwa kila kijiji, itaanza kutekelezwa.

Akiuliza swali bungeni jana, Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele, aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, alitaka kujua Serikali itaanza lini kutekeleza ahadi ya milioni 50 kwa kila kijiji na mitaa, ili kutatua tatizo la ajira na mitaji kwa vijana na akina mama.

Kwa upande wake Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia, aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, akiuliza swali la nyongeza alihoji utayari wa Serikali kuwatangazia wananchi kusubiri fedha hizo, hadi Baraza la Mawaziri litakapokaa na kutoa mwongozo wa kuzitumia.
“Hatua hii itatusaidia wabunge tusipate wakati mgumu majimboni kuulizwa kuhusu milioni 50 za kila kijiji,” alisema Nkamia.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana), Anthony Mavunde, alisema Serikali katika mwaka wa fedha 2016/17 imetenga Sh bilioni 59.5 kwa ajili ya kutekeleza ahadi hiyo.
Mavunde alisema tayari waraka utakaoongoza utoaji wa fedha hizo umeshaandaliwa na kujadiliwa katika kamati ya makatibu wakuu na sasa unasubiri kujadiliwa na Baraza la Mawaziri, ili kuweka mfumo utakaoratibu utoaji wa fedha hizo.

Akitoa majibu ya ziada Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, alisema Serikali imeshatenga bajeti na kuona umuhimu wa kuanza haraka utekelezaji wa jambo hilo.
Alisema hatua hiyo itawezesha fedha hizo kuwafikia wanyonge kwa kuwa imeanza kuweka mfumo mzuri wa kuratibu zoezi hilo.
Waziri huyo alisema mara mfumo huo utakapokamilika, Serikali itawaambia wananchi ni mfumo gani utakaotumika.

Mbowe
Awali akiuliza swali la nyongeza bungeni jana, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani ambaye pia ni Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), alisema hakuna muujiza utakaofanyika kwa sasa ili kutoa fedha hizo, kwani Serikali imefilisika.

Alisema ikiwa Serikali imeshindwa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, huku wizara zikiendelea kusotea fedha za miradi ya maendeleo, itatoa wapi fedha hizo?
Mbowe alisema imekuwa ni tabia kwa Serikali ya CCM kutoa ahadi tamu kwa wananchi wakati wa uchaguzi.
“Katika Serikali ya awamu ya nne ulianzishwa mpango wa mabilioni ya JK ambao ulikufa bila Bunge wala Watanzania kuelezwa sababu.

“Sasa mwaka umepita tangu kumaliza Uchaguzi Mkuu na Baraza la Mawaziri linajua hadi robo ya mwaka wa fedha 2016/17 inakwisha kuna wizara kadhaa hazijapata fedha za maendeleo.

“Ni miujiza gani itakayotumika na Serikali ya CCM ambayo imefilisika na leo (jana) imeshindwa kutoa mikopo kwawanafunzi wa chuo kikuu na ni miujiza gani itatumika kupatikana kwa fedha hizo bilioni 960 badala ya kuwadanganya wananchi?” alihoji Mbowe.

Akijibu swali hilo, Mhagama alisema Serikali haifanyi kazi kwa miujiza bali inafanya kazi kwa mpangilio wa bajeti iliyojiwekea.
“Uthibitisho wa jambo hili kuwa linatekelezeka kama tulivyoweza kuwashangaza Watanzania kwa kutoa elimu bure iliyogharimu mabilioni ya fedha, pia kuwashangaza Watanzania kwa kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ununuaji wa ndege,” alisema.

Waziri Mhagama alisema fedha hizo zitatolewa na Watanzania watazipata, kwani Serikali haitafanya kazi kwa miujiza bali itafanya kwa mpango wa utekelezaji wa bajeti ya wananchi. “Fedha hizo zitafika hata kwenye majimbo ya wabunge wa upinzani,” alisema.

Dk. Mpango
Wakati huo huo, Serikali imesema inategemea kukopa Dola za Marekani milioni 900 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh trilioni 2. kutoka vyanzo vya nje vyenye masharti ya kibiashara ili kuweza kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alipokuwa akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2017/18 na Mwongozo wa Kuandaa Bajeti.
Licha ya hali hiyo, alisema Serikali pia itakopa Sh trilioni 4.434 ambazo ni mikopo ya ndani kwa ajili ya kulipia hati fungani na dhamana za Serikali zinazoiva.

Dk. Mpango alisema Sh trilioni 1.859 ambazo ni sawa na asilimia 1.5 ya Pato la Taifa ni mikopo mipya ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh trilioni 3.700.

Kuhamia Dodoma
Akizungumzia mikakati ya kuhamia kwa Serikali Dodoma, Dk. Mpango alisema maofisa masuuli wanatakiwa kuhamisha shughuli zao mkoani humo kwa kujumuisha mahitaji ya mpango wa bajeti kama ratiba iliyotolewa na Serikali inavyoelekeza.

“Mipango ya ujenzi wa majengo na miundombinu ya Serikali iliyopangwa kujengwa Dar es Salaam ihamishiwe Dodoma. Ujenzi wa majengo na miundombinu yoyote inayotegemewa kujengwa Dodoma ni lazima ipate kibali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu,” alisema.

Mdee amvaa JPM
Kwa upande wake, Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Fedha na Mipango, Halima Mdee, alisema uongozi mbovu unachangia kuyumba kwa uchumi wa nchi.
Alisema licha ya mbwembwe nyingi za Serikali ya awamu ya tano, mengi yameshuhudiwa ikiwamo suala la ‘Serikali iliyotengeneza watumishi hewa’ ikisitisha ajira kwa kigezo kuwa inafanya uhakiki wa watumishi wake.
Alisema kusimamishwa kwa ajira mpya kumefanya nguvu kazi iliyokuwa na uwezo wa kuzalisha kuishi kama ombaomba .
Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chadema), alisema Serikali imekuwa ikiwaumiza wafanyabiashara wakubwa na wa kati kwa kukamata mali zao kama Rais alivyofanya kwa kukamata mali za mfanyabiashara Said Salim Bakhresa.

“Sukari yake ilishikiliwa na serikali bila kutoa sababu zozote zile na Rais aliamua kuachia sukari hiyo bila kutoa sababu zozote za maana kwa umma.

“Hali iko hivyo kwa wafanyabiashara wengi ambao akaunti zao Benki zimeshikiliwa na Serikali bila kuelezwa sababu, jambo linalopelekea kuporomoka kwa uchumi kwa kasi katika taifa letu.
“Kambi rasmi inaunga mkono hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wale wote waliokuwa wanahusika kwa namna moja au nyingine kuhujumu uchumi.

“Lakini tunapinga kwa nguvu zote kwa dola kutumia mamlaka yake kuonea au kunyanyasa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao kwa kufuata sheria na taratibu za nchi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles