Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Wabunge mbalimbali wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Bara na Zanzibar wameendelea kuchangia bajeti ya Wizara ya Nishati iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma Mei 31, mwaka huu na Waziri wa Nishati, January Makamba.
Miongoni mwa wabunge hao waliopata nafasi ya kuchangia bajeti hiyo mapema leo Juni 1, ni Bunge wa Viti Maalum, Ester Bulaya ambaye amesema kuwa Watanzania wanaona fahari kuhusu mwenendo wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere mradi ambao umefikia hatua nzuri.
“Watanzania wote tunaona fahari ya bwawa la mwalimu Nyerere, hilo tunakubaliana kabisa. Lakini, tunatamani uendeshaji wake, ukamilishaji wake pia uendane na thamani ya pesa iliyowekezwa pale ambayo ni kodi ya Watanzania na ni fahari ya nchi yetu,” amesema Bulaya.
Mbali na Bulaya mwingine aliyechangia bajeti hiyo nimbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay ambaye amemsihi Waziri Makamba kupeleka umeme katika maeneo ambayo wanaishi Wahadzabe nakwamba jambo hilo litaweka historia.
“Mheshimiwa Waziriwa Nishati, January Makamba hebu weka historia, wewe uwe waziri wa kwanza kuwapelekea Wahadzabe umeme,” amesema Massay.
Itakumbukwa mapema jana Waziri Makamba alisema kuwa katika mwaka wa fedha ujao kila kijiji nchini kitafikiwa na umeme na hivyo kuweka historia.
Upande wake Mbunge wa Msalala, Iddi Kassim, mbali na kuipongeza bajeti hiyo ya waziri Makamba pia ameshauri wizara hiyo kutupia jicho katika eneo la vilainishi.
“Kama Wizara hamtaweka jicho katika kuhakikisha kwamba mnadhibiti uingizwaji wa vilainishi feki kwenye nchi hii, tutaendelea kutia hasara kubwa sana wananchi katika maeneo haya,” amesema Kassim.
Mwingine aliyepata fursa ya kuchangia katika bajeti hiyo ni mbunge wa Mpanda Mjini mkoani Katavi, Sebastian Kapufi ambaye amesema kuwa umeme wa gridi ya taifa utachochea kuzimua uchumi wa Katavi.
“Sisi wananchi wa Mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma tunaishukuru Serikali kwa jitihada mahususi za kutuletea umeme kupitia gridi ya taifa. Shughuli za kiuchumi zilikuwa zimeanza kuamka lakini baada ya umeme huu mlioleta, mambo yatakuwa mazuri zaidi,” amesema Kapufi.
Zanzibar nao wafunguka
Wabunge kutoka Zanzibar nao hawakuwa nyuma kwani kwa umoja wao wamempongeza Waziri Makamba kuhusu bajeti hiyo iliyowasilishwa bungeni hapo jana.
“Mheshimiwa Waziri, tumepanga kwa makusudi Wabunge wa Zanzibar kila atakayesimama tukupongeze, kwa punguzo lililoenda kushusha umeme wa Zanzibar. Mwaka jana kila Mbunge wa Zanzibar aliyesimama, alikuwa analalamikia bei ya umeme inayokwenda Zanzibar,“ amesema Tauhida Cassian Gallos ambaye ni mbunge wa Viti Maalum kutoka Zanzibar na kusisitiza kuwa licha ya Wizara ya Nishati siyo Wizara ya Muungano, lakini Waziri January Makamba amekuwa msikivu kwa Wabunge wa Zanzibar na kufanikisha kupungua kwa bei ya umeme visiwani humo.