26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Waangola wanavyoutazama vibaya uwekezaji wa China

JOSEPH HIZA

HAKUNA ubishi duniani, China imezidi kuimarisha uhusiano wake wa kiuchumi na Afrika kiasi cha kuangaliwa vibaya na mataifa ya magharibi.

Yote hayo ni katika kutafuta namna ya kuitii kiu yake kubwa inayozidi kuongezeka ya mahitaji ya nishati na rasilimali nyinginezo.

Kwa sababu hiyo kufikia mwaka 2008, China ilikuwa mshirika namba mbili wa kibiashara wa Afrika na ilitabiriwa itazipiku Marekani, Ufaransa na Uingereza kuwa mshirika namba moja wa Afrika kufikia 2010.

Miongoni mwa mataifa ya Afrika yanayoongoza kwa ushirika wa kibiashara na China ni Angola, ambao unaanzia kabla ya uhuru wa taifa hilo lililokuwa likitawaliwa na Wareno.

Mataifa hayo ni kama chanda na pete licha ya kwamba China ina uhusiano na mataifa mengi ya Afrika, lakini Angola ukiwa miongoni mwa uliovuka mipaka.

Hata hivyo, kutokana na kuwapo kelele, kasoro na madudu linapokuja suala la Angola kunufaika na uhusiano huo utawala wa Rais wa sasa João Lourenço ulioingia madarakani mwaka juzi umeamua kubadili mwelekeo.

Kwa mujibu wa waziri wake wa nishati, Joao Baptista Borges, Angola imepanga kupokea mikopo kutoka mataifa mengine ili kupunguza utegemezi kwa China, ambayo kwa sasa inashikilia karibu asilimia 70 ya deni la nje la taifa hilo.

Taifa hilo la kusini magharibi mwa Afrika linataka kuvutia uwekezaji zaidi pamoja na kupata mikopo kutoka mataifa kam Japan, Ulaya na Marekani.

Ili kuonesha kwamba iko makini imeanzisha sheria mpya ya uwekezaji ili kuwa kivutio kwa mataifa hayo mengine.

Mwaka juzi kabla ya ujio wa utawala mpya, deni la nje lilikuwa tayari lisimama dola bilioni 37.2, likiwa karibu sawa na asilimia 30 ya pato la taifa, kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia.

Uhusiano maalumu wa mataifa hayo unaanzia mbali sana kabla ya uhuru wa taifa hili tajiri kwa rasilimali.

Ilikuwa mwaka 1963 wakati wa sherehe za uhuru wa Kenya mwaka 1963, Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Chen Yi alikutana na aliyekuwa mbabe wa vita wa Angola, marehemu Jonas Savimbi.

Chen alimwambia Savimbi, ambaye wakati huo alikuwa katibu mkuu wa Chama cha Muungano wa Watu wa Kaskazini mwa Angola (UPNA) kwamba nchi yake itakipatia chama hicho msaada mkubwa wa kijeshi.

Miaka mitatu baadaye waasi wa UNITA waliotaka kujitenga wakiongozwa na Savimbi waliwashambulia wafanyakazi wa Ureno huko Cassamba.

Wakiwa na bunduki 10 tu aina ya NATO 7.62 zilizonunuliwa kwa msaada wa China, shambulizi hilo lilishindwa kuzuia biashara ya magogo na utawala wa kikoloni wa Ureno ukaua wapiganaji kadhaa wa UNITA.

Lengo la China lilikuwa kunufaika na biashara hilo kutokana na utajiri mwingine wa rasilimali uliopo eneo hilo na hivyo mkazo ulikuwa kujitenga.

Hali hiyo iliishtua Marekani ambayo nayo ilikuwa ikinyonya utajiri eneo hilo kwa mgongo wa makaburu wa Afrika Kusini na hivyo kuingilia kati kukutana na China.

Hata hivyo, China iliendelea na azma yake ikiisaidia watakao kujitenga UNITA iliyokuwa ikipambana pia na chama cha MPLA kilicholenga uhuru wa taifa zima.

Kwa sababu hiyo, baada ya uhuru wa Angola mwaka 1975 ulioletwa na MPLA, haikushangaza wakati Rais Agostinho Neto alipoilaani vikali China kwa uvamizi wake Vietnam Februari 1979.

Hata hivyo, mataifa haya yakaamua kuachana na uhasama na kuanzisha uhusiano mwaka 1983, ambapoAngola ikiwa chini ya Rais wa sasa Jose Eduardo dos Santos.

Neto alifariki dunia Septemba 1979 wakati akifanyiwa upasuaji kutokana na maradhi ya saratani nchini Urusi.

Uhusiano baina ya mataifa hayo ukaendelea na kushuhudia biashara baina yao ukiwa nathamani ya dola bilioni 24.8 mwaka 2010.

Na mwaka 2011 na katika miezi minane ya kwanza ya 2012, Angola ikawa mshirika namba mbili wa China barani Afrika baada ya Afrika Kusini.

Hata hivyo, namna China inavyofanya biashara na Afrika imekuwa ikilalamikiwa mno na wananchi hali ambayo ipo pia Angola.

Tangu kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, kumesababisha pengo katika akiba ya fedha ya Angola.

Pengo limetokea licha ya kwamba nchi hii inashika nafasi ya tatu kwa uchumi mkubwa katika nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.

Pengo hilo lilimaanisha kuwa taifa hilo la kusini magharibi mwa Afrika linahitaji msaada wa haraka.

Kwa sababu hiyo, Rais Jose Eduardo dos Santos kabla hajangatuka mwaka juzi, akitajwa kuwa kiongozi tajiri barani Afrika huku binti yake Isabel akitajwa kama mwanamke tajiri kuliko wote barani humu na mwenye nguvu kuliko wote nchini Angola, ilibidi atafute njia ya haraka ya kuliziba

Kiongozi huyo aliyekuwa  madarakani kwa miaka 35, na ambaye hakuwa mtu wa hadhara au kuzungumza na vyombo vya habari alielekea nchini China kusaka msaada.

Lakini mikopo ya mabilioni ya dola iliyosaniwa na baina ya taifa hilo na China mwezi uliopita imewakasirisha mno raia wa Angola.

Raia hao wa Angola wanasema wametelekezwa wakati wanasiasa wao na China wakigawana faida.

Mbali ya hilo wanalalamika na kusema ni aibu kwa taifa lao la pili kwa uzalishaji wa mafuta barani Afrika kuendelea kuitegemea zaidi China.

Katika ziara hiyo ya kwenda kutembeza bakuri, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, China iliipatia Angola dola zipatazo bilioni 20.

Malipo hayo mara nyingi hulipwa kwa mafuta au fedha kwenda moja kwa moja kwenye kampuni za ujenzi za China ambazo zimetapakaa katika nchi zote za kusini mwa Afrika zikijenga barabara, hospitali, nyumba na reli.

Hiyo ina maana kuwa hata hivyo, mkopo huo hauendi moja kwa moja kwenye uchumi wa taifa hilo ambalo lilitokea katika vita ndefu ya miaka 27 ya wenyewe kwa wenyewe iliyomalizika mwaka 2002.

Kwa kutoenda moja kwa moja katika uchumi kunamaanisha uongezeko la gharama za matumizi kwa wananchi wa kawaida wa Angola.

Ongezeko hilo linakuja ilihali tayari  mji wake mkuu wa Luanda umekuwa ukitajwa kwa karibu miongo miwili sasa kuongoza duniani kwa ukubwa wa gharama za kuishi.

Hasira na wananchi na upinzani juu ya Wachina na serikali imewafanya polisi kuimarisha usalama katika barabara za Luanda hasa maslahi ya China.

Watu kadhaa walikamatwa Juni 20 2015 kwa madai ya kupanga maandamano ya kutishia ‘amani na usalama wa umma’ kufuatia ziara ya Rais dos Santos nchini China.

Kundi la wapiganaji la FLEC ambalo linataka uhuru wa jimbo la kaskazini mwa nchi la Cabinda, lenye utajiri mkubwa wa mafuta, lilitaka China iwaondoe raia wake wote kutoka eno hilo katika kipindi cha miezi miwili la sivyo ‘wataadhibiwa vikali’.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema Angola ina jeshi imara katika eneo la kusini mwa jangwa la sahara na hivyo upinzani wa aina yoyote huweza kunyamazishwa haraka na kwa njia ya kikatili.

Kwa sababu hiyo kuna ugumu wa kuonyesha upinzani wa aina yeyote dhidi ya serikali.

Ukiachana na siasa hizo za taifa hilo zinazohesabiwa kuwa miongoni mwa zile kandamizi barani Afrika, ushawishi wa China barani Afrika kila mara umekuwa ukikosolewa.

Serikali za magharibi na baadhi ya viongozi wa Afrika wamekuwa wakiita ushawishi wake huo barani humu kuwa ukoloni mambo leo.

Wanakosoa kitendo cha taifa hilo lenye uchumi mkubwa duniani kuchukua raslimali ili kujenga miundo mbinu ambayo inachangia katika kuvifaidisha viwanda vya ujenzi vya China na kudidimiza vya nyumbani:

Kuna karibu kampuni 50 za Serikali ya China na 400 binafsi kutoka nchini humo yanayofanya kazi nchini Angola.

Kampuni hizo hutakiwa kutumia asilimia 30 ya ajira za Angola, kitu ambacho lakini kinaelezwa kuwa hakizingatiwi kwa vile ni mara chache raia wa Angola wamekuwa wakipata kazi, mbaya zaidi katika zile nafasi za chini.

“Daima Wachina wanakuwa waongozaji na Waangola wanawakuwa wasaidizi katika kile eneo, Hii ni nchi yetu.Tunapaswa kuwa waongozaji, si wao kutuongoza”alisema Paulo Nascimento, mwenye umri wa miaka 29 ambaye ni dereva teksi.

Kampuni za China zimekuwa zikikana kwa nguvu shutuma za unyonyaji, zikisema kuwa zimeijenga zaidi Angola tangu vita vimalizike miaka 13 iliyopita, kuliko wakosoaji wa Magharibi ambao wamekaa kando.

Meneja masoko wa kampuni ya simu ya China- ZTE, Pascal Wang mwenye umri wa miaka 36 alikuwa na haya ya kusema kuhusu shutuma zinazowaelekea.

Aliliambia Shirika la Habari la Reuters, ” hatuji hapa kufanya biashara tu, bali tunataka kuisaidia Angola. Kile tunachofanya na manufaa tuliyoleta kamwe huwezi kukifananisha na walicholeta mataifa ya magharibi,” alisema.

Ukiondoa uwekezaji kutoka koloni lake la zamani la Ureno na uchimbaji mafuta katika maeneo ya mwambao wa Angola hufanywa na Marekani na mataifa makubwa ya Ulaya.

Hata hivyo, kwa sasa Serikali za Magharibi, wahisani na wawekezaji wameelekeza zaidi juhudi zao kwengineko barani Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,663FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles