26.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, January 18, 2022

WAANDISHI WA MTANZANIA WACHOMOZA TUZO ZA EJAT

Na LEONARD MANG’OHA

-DAR ES SALAAM

WAANDISHI wanne wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited wamepitishwa kuwania tuzo za umahiri katika uandishi wa habari (EJAT), imefahamika.

Tuzo hizo, ambazo huhusisha waandishi wa habari wa magazeti, redio, luninga, wapiga picha na wachora vibonzo, litafanyika Aprili 29, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Waandishi waliopitishwa kupitia kazi mbalimbali zilizochapishwa katika gazeti la MTANZANIA ni pamoja na Mhariri wa habari wa gazeti hilo, Bakari Kimwanga, waandishi Veronica Romwald, Rodrick Ngowi na Nora Damian, ambaye pia ni mshindi wa tuzo hizo katika kipengele cha mwandishi bora wa habari za sayansi na teknolojia.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tuzo hizo, Kajubi Mukajanga, alisema waandishi hao wanaungana na wengine 62 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini walioteuliwa baada ya mchujo wa awali uliofanyika kati ya Aprili 6 na 13, mwaka huu Bagamoyo, mkoani Pwani.

Wateule hao watachuana kuwania tuzo hizo katika vipengele 19, ikiwa ni pamoja na tuzo ya uandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha, michezo na burudani, afya, kilimo na biashara na biashara ya kilimo, elimu, uandishi wa habari na uchambuzi wa matukio.

Nyingine ni habari za utalii na uhifadhi, afya ya uzazi kwa vijana, manunuzi ya umma, kodi na ukusanyaji mapato, habari za uchunguzi, data na haki za binadamu na utawala bora, VVU na Ukimwi, jinsia, wazee na watoto na kundi la wazi, mpiga picha bora za runinga, magazeti na mchora katuni bora.

Alisema kuwa, mwaka huu mwitikio ulikuwa mkubwa ikilinganishwa na mwaka uliopita, ambapo jumla ya waandishi 810 waliwasilisha kazi zao kutoka 568.

Alisema idadi hiyo ni dalili njema na inaonesha jinsi gani waandishi wanalipa uzito mkubwa shindano hilo.

Pamoja na kujitokeza kwa idadi kubwa ya kazi zilizowasilishwa, idadi ya kazi zilizopitishwa imeshuka kutoka 84 mwaka jana hadi 66 mwaka huu.

“Pamoja na kuwa kulikuwa na kazi nyingi zilizowasilishwa na wanahabari wa vyombo vya kielektroniki, ubora wao haukuwa mzuri. Majaji walisema kazi kutoka kwenye magazeti zilikuwa na ubora zaidi,” alisema Mukajanga.

Mukajanga alisema kuwa, shindano hilo ni mwelekeo mzuri kwa wanahabari kutambua na kutathmini tuzo hizo kama kipimo cha umahiri wa uandishi wa habari.

Aliongeza jopo la majaji waliofanya mchujo huo liliongozwa na Valerie Msoka, Katibu alikuwa Dk. Joyce Bazira, wengine waliokuwapo ni Dk. Mzuri Issa, Hasan Mhelela, Pili Mtambalike, Mwanzo Millinga na Nathan Mpangala.

Mgeni rasmi katika shindano hilo litakalofanyika katika Hoteli ya Blue Pearl iliyopo Ubungo, Dar es Salaam, anatarajiwa kuwa mshindi wa tuzo ya mafanikio ya maisha ya uandishi wa habari mwaka 2014, Jenerali Ulimwengu.

“Tumekuwa tukialika wageni mbalimbali wa kisiasa kama vile Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, wakati huu tumeamua kumwalika mwenzetu kwa kutambua mchango wake mkubwa katika tasnia hii,” alisema Mukajanga.

Tuzo za EJAT huandaliwa kila mwaka kwa ushirikiano baina ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Tasisi ya Vyombo vya Habari ya Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA-Tan), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa).

Wengine ni Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), HakiElimu, AMREF, ANSAF, Best-Dialogue na SIKIKA.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
174,926FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles