27.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Waandishi wa habari watakiwa kutokuwa waoga

JANETH MUSHI -ARUSHA

Waandishi wa habari wameaswa kutokuwa waoga na kuripoti habari mbalimbali zinazolenga kusaidia na kuleta matokeo chanya kwa jamii, bila kukiuka kanuni na sheria zilizowekwa, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na wakili kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), William Mtwazi, wakati wa mafunzo yaliyokuwa na lengo la kukutanisha waandishi wa habari na kujadili kuhusu uhuru wa kujieleza na kukusanyika.

Akizungumzia uhuru, hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linaelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, Mtwazi alisema sasa wanahabari wamekuwa waoga kuripoti baadhi ya masuala yanayojitokeza katika jamii.

Alitaja baadhi ya sababu zinazochangia waandishi wengi nchini kuogopa kuripoti masuala mbalimbali yanayojitokeza katika jamii, ni pamoja na kauli za baadhi ya viongozi ambazo zinakuwa hazizingatii weledi.

Mtwazi alisema baadhi ya matamko yamekuwa kikwazo kikubwa kwa wanahabari na kuongeza kuwa taaluma yao ni daraja kati ya Serikali na wananchi na wadau wengine ili waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo, ikiwamo kuibua masuala mbalimbali yanayojitokeza katika jamii, hivyo lazima wawe huru.

“Matamko endelevu ya baadhi ya viongozi yasiyofuata misingi ya maadili au yasiyolingana na sheria za nchi tumekuwa tukishuhudia na nyie ni mashahidi, kuna baadhi ya viongozi wanatoa matamko yasiyozingatia viwango na weledi katika ufanisi wa kazi zao, yanachangia kuleta hofu.

“Tumeshuhudia namna gani waandishi wa habari wanavyokamatwa na kupelekwa vituo vya polisi na kukaa zaidi ya saa 48 wakinyimwa nafasi ya kusikilizwa au kuwa na wanasheria,” alisema Mtwazi.

Alisema kituo hicho kinafanya kazi kwa ukaribu na waandishi wa habari na wamekuwa wakitoa msaada wa kisheria pindi wanapokumbwa na kadhia mbalimbali wakati wakitekeleza majukumu yao.

Naye mwanasheria Fortunata Ntwale aliwataka waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo kwa kuandika habari zenye kuleta matokeo chanya kwa jamii na kutokuwa sehemu ya uvunjifu wa kanuni na sheria za nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,903FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles