30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Waandishi wa habari watahadharishwa

Pg 2 kibandaNA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM

JUKWAA la Wahariri (TEF), limewataka waandishi wa habari kuchukua tahadhari, hasa wakati huu wa uchaguzi kwa kufanya kazi zao kwa weledi na kuzingatia maadili ya taaluma yao.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru, Christopher Lissa, kudaiwa kupigwa wakati akipiga picha za watu wanaodaiwa kujifanya ni wanachama wa Chadema walioandamana kwenda makao makuu ya chama hicho kuunga mkono hotuba ya aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TEF, Absalom Kibanda, alilaani tukio hilo na kusema ni mwendelezo wa vitendo vyenye mwelekeo wa kuzuia waandishi wa habari kutekeleza wajibu wao wa msingi wa kukusanya taarifa na kuuhabarisha umma.

“Kama waandishi wa habari wanafanya makosa wanapaswa kufikishwa katika vyombo vya dola kwa mujibu wa sheria za nchi na si raia au mtu yeyote kuwashambulia.

“Vyama vya siasa kama taasisi na wanachama wake, viache mara moja vitendo vya kuwashambulia waandishi wa habari, vikiendelea tutachukua hatua stahiki, ikibidi kususia matukio na mikutano ya vyama hivyo,” alisema Kibanda.

Alisema matukio hayo si tu yanahatarisha usalama wa wanahabari, bali pia yanaingilia uhuru wao wa kufanya kazi.

“Ukimpiga mwandishi wa habari mmoja hata kama unakubaliana naye au hukubaliani naye, utakuwa umepiga tasnia nzima ya habari,” alisema.

Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, alisema hakuna habari ambayo ina thamani kuliko maisha ya mwandishi, hivyo jukumu la kujilinda ni la mwandishi husika.

“Wanasiasa, wachumi na watu wengine ni marafiki zetu wa kikazi, msingi muhimu ni kutambua dhima na wajibu wetu kama wanahabari…hii si tasnia dhahifu au dhalili, hivyo anapopigwa mwandishi mmoja ni sawa na kupiga waandishi wote jambo ambalo hatutalikubali,” alisema.

Katika hatua nyingine, TEF imevitaka vyama vya siasa na watu binafsi wanaoandaa mikutano ya waandishi wa habari kutowaalika makada wa vyama vyao ambao si wanataaluma.

Kibanda, alisema utamaduni wa kuchanganya makada wa vyama na wanataaluma, unawanyima fursa waandishi wa habari kutekeleza wajibu wao kwa uhuru na unaweza kuhatarisha maisha yao.

“Mikutano ya Gwajima (Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima) na Dk. Slaa (Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema), ilikuwa ni ya waandishi, lakini ilijumuisha makundi ya watu ambao si wanahabari, ambao walisikika wakipiga makofi, kushabikia na hata kuuliza maswali,” alisema.

Pia TEF imevitaka vyombo vya ulinzi na usalama na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kujenga mazingira rafiki ya kikazi kwa waandishi wa habari kwani wana wajibu mkubwa katika mchakato mzima wa uchaguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles