Na Malima Lubasha, Musoma
KAMPUNI Binafsi ya Utalii ya Awesome Expedition yenye makao makuu yake mkoani Arusha imeandaa programu ya kuhamasisha utalii ijulikanayo kama Awoke International Sports Tourism Conference and Expo iliyofanyika mjini Musoma mkoani Mara.
Mratibu wa mpango huo uliofanyika jana mjini musoma ukiwashirikisha Wakurugenzi Watendaji, Maafisa Utamaduni, Mabaraza ya Wazee, Maafisa Habari Wilaya, Wasanii, Wadau wa Utalii, Waandishi wa Habari wa Mara na Nje, Madiwani,Wenyeviti wa Halmashauri na Wadau wa Maendeleo, Buchebuche Enosy amesema unalenga kuhamasisha utalii na ni wa kwanza kuanzishwa Afrika Mashariki na utaanzia mkoani Mara.
Mapema akiwasilisha mada ya programu hiyo amesema itafanyika Septemba, mwaka huu kwa ajili ya kuhamasisha utalii katika Mkoa wa Mara ambapo wajasiriamali na wafanyabiashara mbalimbali watapata fursa ya kuonyesha na kuuza bidhaa zao.
Enosy amesema utalii wa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti utafanyika kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Mara nchini Tanzania kwa kushirikiana na waandishi wa habari kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Congo, Malawi, Zambia, Ghana, Uturuki, Marekani, Canada, India na Israel.
Amesema kupitia vyombo vya habari wataripoti habari za kuhamasisha utalii yakiwemo maonyesho ya bidhaa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambapo wanahabari wataripoti na kuandaa vipindi na makala na kuvirusha katika vyombo vyao vya habari katika nchi zao kwa lengo la kutangaza vivutio vya Mkoa wa Mara ili kuw vutia watu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania kufanya utalii mkoani humo sambamba na kutembelea hifadhi ya Serengeti.
Amesema hii ni kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya utalii na kuhamasisha utalii wa ndani na kimataifa kupitia Filamu ya Royal Tour.
‘’Kwanza kabisa ningependa kuifahamisha jamii yetu ya Tanzania na ya kimataifa kuwa Awesome Expedi tion ni kampuni binafsi ya kitalii yenye makao yake makuu mkoani Arusha nchini Tanzania na imeandaa kongamano hili la kuhamasisha utalii la Awoke International Sports Tourism Conference and Expo litakalofanyika mjini Musoma mkoani Mara,’’ amesema Enosy.
Amefafanua kuwa pia kutakuwa na mkutano wa kimataifa (International Conference) utakaofanyika mjini Musoma ukumbi wa Mukendo Plaza kwa siku tatu ambapo zaidiya wageni 350 watahudhuria.
‘’Mada sita zitajadiliwa ambazo zitahusu Safari, Michezo na Burudani, Utalii, Mitumbwi ya makasia, kutembea kwa miguu, Matamasha ya asili na mchezo wa kuvua samaki,”amesema.
Awali, akifungua kongamano hilo Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Msalika Makungu alisema mratibu wa mpango huu Buchebuche Enosy ameonyesha njia kuhamasisha utalii kuinua uchumi wa taifa kupitia sekta na ipohaja ya kuungwa mkono.
Amesema wazo hili ni kuongeza na kuimarisha mahusiano nchi za Afrika ya Mashariki kukuza utalii kupitia majukwaa mbalimbali waweze kutembelea vivutio vya Mkoa wa Mara, Hifadhi za Taifa na vya nchi hizo ambapo mpango huu kuanzishwaa mkoani mara ni kuchochea ushirikiano katika utalii wa nchi za Afrika Mashariki na kuagiza viongozi wa Serikali na Halmahauri za wilaya kuanisha vivutio katika maeneo yao kutangaza wazo hili na kuhimiza kuboresha miundo mbinu ya barabara kwa ajili ya watalii wa ndani na nje.
“Wazo hili halina mmiliki kwa waliolileta bali linatakiwa kufikishwa kwa jamii likifanikwa watakaonufaika ni wengi wakiwama kimataifa na watanzani wenyewe wazo hili pia lifikishwe mikoa mingine kuonyesha vivutio vyake,” amesema Makungu.
Makungu alishauri Halmashauri za wilaya zijengwe uwezo ili kuimarisha na kutanga vivutio vya utalii ha pa nchini katika kukusanya mapato kuinua uchumi wa taifa.