29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

Waajiri wahimizwa kuhamasisha wafanyakazi kujiunga na CHF

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Waajiri nchini wameaswa kuwahamasisha wafanyakazi wao kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ulioboreshwa (CHF) ili kuwa na uhakika wa matibabu pindi wanapougua ili kutoa urahisi wa upatikanaji wa huduma bora za Afya na kwa gharama nafuu.

Wito huo umetolewa leo Juni 2, jijini Dar es Salaam na Mratibu wa CHF Mkoa wa Dar es Salaam, Yassin Kisawike katika mkutano uliowakutanisha Maafisa rasilimali wa kampuni mbalimbali nchini ambapo amesema huduma ya mfuko huo inapatikana kila Halmashauri ya Mkoa wa Dar es Salaam na wanalenga kupanua wigo zaidi wa utoaji huduma hiyo.

“Kwa Dar es Salaam bado kuna watu wanaofanya kazi katika viwanda na bado hawana bima hii ambayo kwa mtu mmoja ni Sh 40,000, familia Sh 150,000 hivyo ni wakati sasa waajiri kuhakikisha wanawahamasisha wafanyakazi wao kujiunga katika mfuko huu ili waweze kuwa na uhakika wa kupata huduma pindi wanapougua,” amesema Kisawike.

Amesema kuwa bima ya Afya ya Jamii inatoa fao la matibabu kwa wanachama, na mwanachama wa bima ya CHF anaweza kuwa mtu binafsi au familia ya watu wasiozidi 6 kwa maana ya mkuu wa kaya na wategemezi wake.

Ameongeza kuwa mkoa wa Dar es Salaam hadi sasa waliojiunga na mfuko huo ni asilimia 11 tu ya watu zaidi ya milioni tano, hivyo idadi bado ni ndogo na wanaendelea kufanya uhamasishaji ili waongeze wanufaika na wanachama wa mfuko huo na idadi itakapo kuwa kubwa na huduma itakuwa bora zaidi.

Aidha, amesema changamoto inayosababisha idadi ndogo ya wanachama ni uelewa mdogo kwa jamii kuhusu bima na pia ni hiyari hivyo hawaoni sababu ya kujiunga na bima.

“Jamii bado ina maswali mengi inajiuliza kwa nini wajiunge na bima wakati hawaumwi mara kwa mara, ila niishauri jamii kuwa bima inapunguza gharama za matibabu hususan pale ugonjwa au ajali inapotokea ghafla,” amesema.

Naye, Meneja Rasilimali watu kutoka Kampuni ya TLA Printing and Package, Joseph Mabanga amesema uwepo wa bima ya afya inawafanya wafanyekazi kujiamini na pia wanakuwa na uhakika wa matibabu yao na familia zao.

“Uhakika wa matibabu kupitia bima ya afya ya CHF iliyoboreshwa inafaida kwa mtu moja, familia na taifa kwa ujumla hivyo watanzania wajiunge na bima hiyo,” amesema Mabanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles