33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Vyuo vyachangamkia kupanga nyumba za NSSF

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limesaini makubaliano ya awali na vyuo vya elimu ya juu vilivyopo Dar es Salaam, kwa ajili ya kuwapangisha wanafunzi nyumba zilizopo Mtoni Kijiji.

Akizungumza mara baada ya kuweka saini makubaliano hayo, jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio, alisema zaidi ya wanafunzi 17,820, watanufaika na nyumba hizo katika awamu ya kwanza.

Erio alisema kusaini makubaliano hayo ni hatua muhimu ya kukamilisha ujenzi wa majengo ili sasa yanaweze kutumika na kukaliwa na wananchi.

Alifafanua kuwa kati ya makundi wanaokusudia kutumia majengo hayo ni wanafunzi wa vyuo mbalimbali. 

Erio alisema wamesaini makubaliano rasmi na uongozi wa Chuo Kikuu cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE), ambacho kinahitaji nafasi kwa ajili ya wanafunzi 3,000.

Alisema Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kinahitaji nafasi kwa ajili ya wanafunzi 3,500, Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT), kinahitaji nafasi kwa wanafunzi 320, Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kinahitaji nafasi kwa wanafunzi 5,000 na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kinahitaji nafasi za wanafunzi takribani 6000.

“Kwa hiyo tumesaini makubaliano ya awali ambayo ni muhimu kwa pande zote mbili, kwetu sisi wakati tunakamilisha taratibu za kuwapangisha tunajua soko likoje na wao wanakuwa na uhakika kwamba wanaenda kuzungumza na wanafunzi kuwaeleza kuhusu makazi haya,”alisema.

Alisema eneo la Mtoni Kijiji kuna nyumba ambazo zipo tayari kwa ajili ya kutumika, ambazo zinaweza kuchukua wanafunzi 4,000.

Erio alisema nyumba ambazo hazijakamilishwa kujengwa ujenzi wake utakamilishwa.

Aliendelea kusema nyumba zilizopo zikiwemo za Toangoma na Dungu, zinafaa kwa makazi au kupangishwa ama kwa kuuza.

Aliwataka Watanzania kuchangamkia fursa ya kukopa ili kuzinunua au kupanga katika nyumba hizo 

Pia, alisema uwepo wa nyumba hizo ni fursa kwa taasisi za fedha kwa kuanza utaratibu kwa wanaotaka kupanga au kununua nyumba hizo waanze utaratibu wa kuwakopesha na ikiwezekana kwa riba maalumu ambayo itakuwa nafuu.

Kwa upande wake Kaimu Ras wa Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), ,Profesa Stephen Maluka aliipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa kuvifikiria vyuo kupata nafasi za makazi, kwamba chuo hicho kina wanafunzi 6,000, lakini uwezo wa chuo ni kuwapa malazi wanafunzi 420.

“Utaona zaidi ya wanafunzi 5,000 wanahangaika hawana sehemu ya kukaa, kwa hatua hii ya Serikali ya kutufikiria sehemu ya malazi tunaipongeza sana,” alisema.

Naibu Mkuu wa Chuo (Taaluma, Utafiti na Ushauri), kutoka Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dkt. Imanueli Mnzava, alisema wanalishukuru Shirika Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kuwapatia fursa ya kukaa wanafunzi wao katika nyumba hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles