Na Beatrice Kaiza, Mtanzania Digital
VYUO vikuu nchini vimeshauriwa kuwekeza zaidi kwenye mafunzo ya vitendo ili viweze kuwaandaa wahitimu na ushindani wa soko la ajira.
Ushauri huo umetolewa Julai 7, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Banda lao katika maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara maarufu sabasaba yanayoendelea.
“Mimi naona vyuo vyetu ni wakati kutilia mkazo kwenye mafunzo ya vitendo leo unampika miaka miwili ule mwaka wa mwisho unampeleka kwenye mafunzo ya vitendo kwa mwaka mzima iwe kwenye kiwanda au taasisi. Hii itasaidia kumtengeneza muhitimu kuwa na ushindani hata kwa vyuo vikuu vya nje.
“Natoa wito kwa wanafunzi wote wanaotaka kwenda kusoma nje ya nchi waje kwetu tutawashauri na tutawaunganisha na chuo husika,” amesema Mollel.
Hata hivyo, Mollel amesema Global Education link itaendelea kushiriki kwenye maonesho mbalimbali kwa lengo la kuwafikia Watanzania wengi wanaotaka kwenda kusoma nje ya nchi.