26.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 19, 2022

VYOMBO VYA ULINZI VITAFUTE KIINI MAUAJI YA POLISI MKURANGA, KIBITI

KWA mara nyingine tena Taifa limeshuhudia mauaji ya kutisha ya askari polisi saba yaliyotokea katika Wilaya ya Kibiti.

Tukio hili linashtua na kuibua maswali mengi hasa kutokana na kile kinachoonekana kuwa ni mwendelezo wa matukio ya aina hiyo katika Mkoa wa Pwani.

Askari hao saba ambao walishambuliwa kwa risasi wakati wakitoka doria yametokea katika kipindi kisichozidi miezi miwili tangu Februari mwaka huu watu watatu akiwemo Ofisa Upelelezi wa Wilaya (OC CID) wa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, Mrakibu wa Polisi, Peter Kubezya, wakiuawa kwa risasi.

Wengine waliouawa ni Ofisa wa Misitu ambaye alikuwa Mkaguzi wa Kituo cha Ukusanyaji mapato ya ushuru katika Kijiji cha Jaribu, Peter Kitundu na Rashid Mgamba ambaye ni mlinzi/mgambo ambao walipigwa risasi kichwani na begani na walikufa papo hapo eneo la tukio.

Kumekuwapo na mlolongo wa matukio ya mauaji katika Wilaya ya Kibiti na Mkuranga na kinachozua maswali ni kitendo cha wauaji kutochukua mali yoyote.

Mei, 2016 Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Said Mbwana, aliuawa kwa risasi.

Oktoba, 2016, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho hicho, Aly Milandu, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wanne.

Novemba, 2016 wenyeviti wawili wa vitongoji wa kijiji hicho, waliuawa kwa kupigwa risasi.

Januari, 2017 watu ambao Jeshi la Polisi hadi sasa halijawafahamu waliomuua mfanyabiashara, Oswald Mrope kwa kumpiga risasi mbele ya familia yake.

Februari 3, 2017 watu wasiojulikana walivamia nyumba ya mwenyekiti wa Kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga na kuichoma moto huku yeye mwenyewe akifanikiwa kuwatoroka.

Tukio la sasa la kuuawa kwa askari saba limetokea ikiwa ni siku chache baada ya askari wa Jeshi la Polisi kuwaua kwa risasi wanaume watatu waliokuwa wamevalia buibui za kike.

Wanaume hao ambao walikuwa na pikipiki mbili, walikuwa wakijaribu kukwepa vihunzi vya polisi vilivyokuwa vimewekwa katika daraja la Mkapa.

Sisi MTANZANIA Jumamosi tunadhani sasa ni wakati mwafaka kwa Jeshi la Polisi pamoja na mamlaka nyingine kulitazama jambo hili kwa kina ili kupata kiini cha kuwapo kwa matukio hayo.

Tunasema hivyo kwa sababu ni jambo linalozua maswali na kuacha hisia nyingi  hasa ikizangatiwa matukio hayo yanatokea katika maeneo yale yale, kuna nini nyuma ya pazia?

Hiki ni kitendawili ambacho hakipaswi kuachiwa Jeshi la Polisi tu bali vyombo vyetu vyote vya ulinzi na usalama.

Tunaamini vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vina mkono mrefu zaidi, visiishie kukamata tu viende mbali na ili kubaini kiini cha tatizo.

Hatutarajii tena kuona tukio la sasa likipoa na kuvisahaulisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.

Mwisho tunatoa pole kwa Jeshi la Polisi na Taifa kwa ujumla kwa kupoteza askari ambao walikuwa na mchango mkubwa katika kutekeleza wajibu wao wa kulinda raia na mali zao.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
175,234FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles