30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho vya taifa vyafunika Sabasaba

CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM

WAKATI jana ikiwa kilele cha Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, maarufu Sabasaba, maelfu ya wananchi waliojitokeza walionekana kuwa zaidi na kiu ya kupata vitambulisho vya taifa na vyeti vya kuzaliwa.

Hayo yalijidhirisha kutokana na kuwapo mamia ya watu kwenye misururu banda la Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).

Uhitaji wa nyaraka hizo muhimu, ulifanya pia banda la Mahakama na lile la Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kuwa na watu wengi waliokuwa wakifika ili wapate mihuri ama viapo vitakavyowawezesha kupata vitambulisho vya taifa na vyeti vya kuzaliwa.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Nida, Thomas Nyakabengwe, aliiambia MTANZANIA kuwa mwamko kwa mwaka huu ni mkubwa, kwamba wamekuwa wakipokea wananchi zaidi ya 9,000 kwa siku.

“Wengi wanaofika hapa kuchukua vitambulisho hawana taarifa sahihi, hata taarifa za wazazi wao,” alisema Nyakabengwe.

Alisema wanaofika katika banda lao, wanaenda kuulizia taarifa za vitambulisho vyao, kutafuta vipya na baadhi yao wanahitaji elimu ya matumizi ya vitambulisho hivyo.

“Wanaofika kupiga picha na alama za vidole ni watu 200 kwa siku,” alisema Nyakabengwe.

Alisema kwa siku wamejipanga kuhudumia watu 200, hivyo wanalazimisha kufungua banda saa mbili asubuhi badala ya saa nne ili waweze kuhudumia kwa wakati.

Ofisa Masoko wa Rita, Edwin Mbekenga, alisema kwa mwaka huu wananchi wamejitokeza kwa wingi zaidi tofauti na miaka ya nyuma.

Alisema wengine wanashindwa kuhudumiwa kwa kukosa baadhi ya vielelezo.

“Wengi wanaofika hapa hawana vitambulisho wala vielelezo, tunajitahidi kuwapa elimu na kuwahudumia waliokamilisha taratibu,” alisema Mbekenga.

Ofisa masoko mwine wa Rita, Josephat Kimaro, alisema kwa siku wanahudumia zaidi ya watu 1,000 lakini wanaofanikiwa kukamilisha usajili ni kati ya 700.

Alisema tayari wameanza kugawa vyeti kwa waliokamilisha taratibu.

“Takwimu kamili tutazitoa baadaye na waliokamilisha vigezo na fomu zimekamilika watapata vyeti vyao,” alisema Kimaro.

Alisema changamoto iliyopo wananchi wengi wanahitaji hadi panapotokea mahitaji ndio wanatafuta vyeti.

Kimaro alisema hivi karibuni Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imefungua dirisha dogo la usajili ambapo masharti ni pamoja na waombaji kuwa na vyeti vya kuzaliwa hatua iliyofanya wengi wafike kuvitafuta.

Aliwashauri Watanzania wajenge mazoea ya kutafuta vitambulisho muhimu kwao wasisubiri hadi kuwapo changamoto.

Ofisa wa TLS, Salma Mpeta, alisema wamekuwa wakipokea zaidi ya watu 300 kwa siku ambao wengi wamekuwa wakifika kupata viapo.

Alisema TLS lengo lake kuu ni kutoa msaada wa kisheria, lakini katika maonesho wamekuwa wakipokea idadi kubwa ya wanaotaka viapo badala ya msaada wa kisheria.

“Tunaomba wananchi waje wapatiwe msaada wa kisheria, tunahitaji kuwasaidia kwa sababu wengi wanashindwa huko mitaani kwa sababu ya gharama,” alisema Salma.

Watoaji huduma Nida, Rita, TLS, Uhamiaji wamelalamikia ukosefu wa vielelezo kwa wananchi wanaofika kutaka Vitambulisho.

Alisema wengi wao hawana taarifa zao sahihi na hawafahamu umri wa wazazi wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles