Hadija Omary, Ruangwa
Wanachama wa Vyama vya Ushirika nchini wametakiwa kuacha kuchanganya mambo ya siasa na ushirika ili kuondoa migogoro na migongano inayotokea mara kwa mara katika vyama vyao.
Kaimu Mrajisi ushirika huo nchini, Tito Haule ametoa rai hiyo leo wakati akizungumza na wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika (RUNALI) kinachokutanisha wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale mkoani Lindi.
Haule amesema kuna tabia ya baadhi ya wanachama wa vyama vya ushirika kuchanganya mambo ya kisiasa na ushirika jambo lilonasababisha migogoro ndani ya vyama vyao na kubadilisha dhana na malengo ya ushirika ya kuwaunganisha wakulima pamoja.
“Lengo la kuanzisha ushirika ni kuwaunganisha wakulima kuwa na sauti moja ili kuweza kupanga bei ya mazao na kuzuia mianya ya walanguzi, shida kubwa wana ushirika hasa kusini ni kuchanaganya masuala ya uchumi na maslahi kisha wanachagua viongozi kwa ushabiki,” amesema Haule.
Kwa upande wake Salima Chilima kutoka Chama cha Msingi cha Muungano (AMCOS), alisema suala hilo la kuchanganya siasa na shughuli za ushirika linawafanya wanaushirika kugwanyika kutokana na itikadi za vyama vyao.