23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 22, 2023

Contact us: [email protected]

Vyama vyasisitiza umakini kamati wataalam katiba mpya

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Vyama vya Siasa vimeshauri kuwepo kwa umakini mkubwa wakati wa kuchagua wajumbe wa Kamati ya Wataalam wa Katiba Mpya.

Vyama hivyo Mei 26, 2023 vimekutana katika kikao maalumu kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan mwanzoni mwa mwezi huu ambaye alimuagiza Msajili kuhitisha kikao hicho.

Rais Samia aliagiza kihitishwe kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi kilichokuwa kikiratibu maoni ya wadau kuhusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.

Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Chama cha United Democtaric (UDP), John Cheyo, ameshauri baraza lihusishwe katika kuchagua wajumbe wa kamati ya wataalam wa katiba.

“Katiba inatengenezwa na wataalam…watatoka wapi, nani atawachagua? Kwa sababu naona kuna ugomvi kati ya wanasiasa na wataalam, bila kuwahusisha wanasiasa hatuwezi kumaliza tatizo la katiba,” amesema Cheyo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima (AFP), Said Sudi, ameshauri wachaguliwe wajumbe watakaofikisha mahala pazuri mchakato huo.

“Kamshauri Rais asije akatuletea wataalam watakaotuchafua, tunataka wataalam watakaotufikisha mahala pazuri,” amesema Sudi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ameshauri kutumiwa vizuri muda uliobaki ili kuhakikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025 unafanyika vizuri.

“Lazima twende na wakati, kuna mambo ya kuyatazama na kuyapa kipaumbele ili kuhakikisha chaguzi zinakwenda vizuri,” amesema Profesa Lipumba.

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema watahakikisha mchakato wa kupata katiba mpya unakuwa shirikishi na kwamba majina ya wajumbe wa kamati ya wataalam wa katiba yatatokana na mapendekezo kutoka sehemu mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa.

“Mama (Rais Samia) alivyotuita ilikuwa kama ametufungulia njia, tujadiliane namna gani tutakavyoenenda ili tuepukane na kukwama kama mchakato wa kwanza ulivyokwama.

“Kamati ya wataalam majina yatatokana na mapendekezo ambayo yatatoka sehemu mbalimbali ‘plus’ vyama vya siasa,” amesema Jaji Mutungi.

Mwenyekiti wa Baraza hilo, Juma Khatibu, amesema wanatarajia kukutana mwezi ujao kupitia ripoti ya Kikosi Kazi na baada ya kikao hicho utafuatia mkutano mkubwa wa wadau utakaofanyika Agosti mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles