25.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 28, 2022

Contact us: [email protected]

Vyama vya siasa vyatakiwa kufuata maadili

Na MWANDISHI WETU-SIMIYU

VYAMA vya siasa wilayani Busega mkoani Simiyu, vimetakiwa kufuata sheria, maadili, taratibu na kanuni za Uchaguzi Mkuu wa kuchagua rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 28. 

Hayo yamesemwa jana na Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Anderson Kabuko wakati wa kikao kati yake na vyama vya siasa, ikiwa ni maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Alivitaka vyama vya siasa vilivyopo wilayani Busega kuwa na utulivu na kufuata sheria na kanuni za uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu na kuwaasa kuteua wagombea watakaokuwa na mawazo chanya, hivyo kukubalika na wananchi.

“Utakapofika muda sahihi wa kufanya kampeni, tufanye vizuri kampeni kwa kuzuia taharuki, kuzuia mihemko na uchochezi ili kupita salama katika jambo hilo, na naomba Mwenyezi Mungu atusimamie tuweze kusimamia salama mpaka mwisho wa zoezi hili,” alisema Kabuko.

Alivitaka vyama vya siasa na wagombea wao kujikita kueleza sera zao na si vinginevyo kwani hatua hiyo itasaidia kuepuka uchochezi kwa jamii jambo ambalo linaweza kuzua taharuki kwa wapigakura.

Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Busega, Rutagumirwa Rutalemwa alivisisitiza vyama vya siasa na wagombea watakaopata nafasi ya kugombea kuzingatia maagizo ya maadili yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili nchi iweze kupita salama kwenye Uchaguzi Mkuu.

“Vyombo vya ulinzi na usalama wilayani Busega vitafanya kazi kwa muda wote ili kuhakikisha amani inatawala kwa kipindi chote cha uchaguzi. Tutumie lugha za ustarabu na staha ili kuepuka lugha za matusi na tuheshimu utu wa mtu,” alisema Rutalemwa.

Naye Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Busega, Hamad Mabula aliwaomba wawakilishi wa vyama vya siasa kutambua kwamba taasisi hiyo itakuwa macho katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi.

“Takukuru itakuwa macho muda wote na haitasita kuchukua hatua kwa mtu yeyote kutoka chama chochote atakayefanya vitendo vitakavyoashiria rushwa.  Tutamkamata, kumuhoji na kumfikisha mahakamani mtu yeyote wakati na baada ya uchaguzi kama tutakuwa na shaka ya vitendo vyovyote vya kuashiria rushwa,” alisema Mabula.

Vyama vilivyoshiriki mkutano huo ni CCM, Chadema, CUF, ACT Wazalendo na UDP.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,444FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles