27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Vyama 10 vyahoji mambo 5 Muswada Vyama vya Siasa


Na ANDREW MSECHU

VIONGOZI wa vyama 10 vya upinzani wametangaza kuupinga hadharani Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa wakisema unatengeneza kaburi la vyama vya siasa na demokrasia nchini.

Wakizungumza kwa pamoja katika mkutano wao uliofanyika Dar es Salaam jana, viongozi hao walisema wanaupinga muswada huo kwa kuwa hauna manufaa wala maslahi kwa umma wa Watanzania, kwani unakwenda kuondoa uhuru wa kufanya siasa.

Akisoma tamko la vyama hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chaumma), Hashim Rungwe, alitaja sababu tano zilizowasukuma kutumia Siku ya kumbukumbu ya Uhuru wa Taifa kuupinga muswada huo aliodai unaonekana kuwa na nia ya kurudisha nyuma demokrasia.

“Kwa hiyo tumeamua kutumia siku hii ya kumbukumbu ya kupata Uhuru kudai ‘uhuru wa kufanya siasa’ katika Taifa letu kwa sababu sheria inayopendekezwa na Serikali inakwenda kuondoa kabisa. Tumeanza rasmi safari ya kuudai uhuru wetu kama vyama vya siasa na kamwe hatutakubali upokwe,” alisema.

Alisema sababu ya kwanza, unakiuka Katiba ya nchi inayotoa uhuru wa watu kujumuika na kuunda vyama vya siasa, hivyo ni vyema sheria iliyopo kwa sasa iendelee kutumika kwa kuwa inaonekana ina afadhali kuliko sheria hiyo mpya inayopendekezwa.

Alisema sababu ya pili ni kutoshirikishwa vyema kwa wahusika wakuu katika mchakato wa kuandaliwa kwa muswada huo na hata pale walipotoa maoni yao bado Serikali iliyatupilia mbali na hayajawekwa popote katika muswada huo.

Alisema sababu ya tatu, muswada huo ukipitishwa kuwa sheria kamili unakwenda kufanya shughuli za siasa nchini kuwa kosa la jinai na wapinzani hawatapa nafasi ya kufanya kazi zao.

Alisema sababu ya nne ni pale Msajili wa Vyama vya Siasa anapopewa mamlaka makubwa kwa kiwango cha hata kuwa na uwezo wa kuingilia uamuzi wa ndani ya vyama vya siasa wakati anapaswa kuwa mlezi wa vyama.

Alisema sababu nyingine, hata kabla ya sheria hiyo kutungwa na Bunge tayari Msajili wa Vyama vya Siasa ameshatunga kanuni na kuziwasilisha kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi ya Baraza la Vyama vya Siasa.

“Kamwe hatuwezi kuwa sehemu ya kulidharau Bunge letu. Tunatoa wito kwa Bunge bila kugawanywa na tofauti zao za kiitikadi na vyama lifanye kazi yake vyema lilinde kwa wivu mkubwa mamlaka yake,” alisema.  

Maeneo wanayopinga

Rungwe, alisema maeneo wanayoyapinga katika muswada huo ni kuua sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 iliyoweka utaratibu wa kuwapo  mfumo wa vyama vingi kwa lengo la kujenga demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.

Alisema muswada huo, unampa mamlaka makubwa Msajili ambaye atakwenda kuwa si msajili tena bali mdhibiti wa vyama vya siasa ambapo kifungu namba 4 kinafanyiwa marekebisho kumpa nguvu hiyo.

“Pia muswada huo umejaa adhabu za jinai na kufanya shughuli za vyama vya siasa kuwa jinai wakati ni haki ya kikatiba. Vifungu vipya vyote vimeweka adhabu ya faini au kifungo au vyote hata kwa mambo madogo kama vile kukosea taarifa au msajili akitaka kujua taarifa za vikao vya chama,” alisema.

Rungwe alisema kifungu cha 3 ambacho kinafanyia marekebisho kifungu cha 4 kinatoa mamlaka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia mfumo wa uchaguzi wa ndani wa chama na kuamua nani awe kiongozi wa chama wakati yeye si mwanachama wa chama husika.

Alisema eneo jingine, ni kifungu cha tano ambacho kinatunga kifungu cha 5A kinachotoa sharti kuhusu elimu ya uraia/mafunzo ya kujenga uwezo yanayotolewa na taasisi au mtu aliyesajiliwa nchini au nje ya nchi kuomba kibali kwa Msajili kabla ya kufanya hivyo, lengo likiwa kuvidhibiti vyama vya siasa kuwa na mahusiano na taasisi au mashirika ya kimataifa.

Alieleza kuwa muswada huo pia unampa mamlaka makubwa Msajili wa Vyama vya Siasa kutaka taarifa yoyote kutoka kwenye chama au kiongozi wa chama kupitia mamlaka jumuishi na kupitia kifungu cha 5B, asipopewa hata kama ni taarifa za siri wanachama na viongozi wanakabiliwa na adhabu ya faini au kifungo.

Alisema katika kifungu kipya cha 6A(3) kinaingilia utaratibu wa katiba za vyama kwa kutoa sharti kuwa Mkutano Mkuu au Kamati Kuu havitakiwi kukasimu mamlaka yake kwa vyombo vingine ndani ya chama, suala ambalo halikubakili kwani  hata Bunge hukasimu mamlaka yake kwa kamati zake na kuziruhusu kutoa uamuzi kwa niaba ya Bunge zima.

Rungwe aliainisha kuwa kifungu kipya cha 8D(2) kinampa msajili mamlaka ya kuamuru chama kufuta au kurekebisha kifungu chochote cha katiba yake.

Alieleza pia kifungu cha 8E kinazuia vyama kuwa na kikundi cha ulinzi suala ambalo si zuri kwa kuwa kwa mujibu wa katiba, ulinzi ni jukumu la kila mtu.

“Lakini pia kuna kifungu cha 21E kinachompa msajili mamlaka ya kumsimamisha au kumfukuza uanachama mwanachama wa chama cha siasa. Lengo hapa ni kuwaondoa viongozi wa vyama wanaoikosoa Serikali kwa kuwa akimsimamisha uanachama na uongozi wake unakoma.

“Pia kuna uwezekano msajili akatumia kifungu hiki nyakati za chaguzi kama za urais, ubunge na udiwani kuwafukuza wagombea ambao wanaonekana kukubalika na hivyo kuwafanya wagombea wa CCM kupita bila kupingwa,” alisema.

Alisema kifungu cha 6A(6) kinazuia vyama vya siasa kufanya shughuli za harakati au kuweka shinikizo kwa umma kuhusu masuala yanayowahusu watu hivyo kinafuta dhima ya chama cha siasa kama chombo cha kupinga ukandamizwaji na kutetea haki.

“Kwa hiyo kupitia kifungu hiki, sasa vyama vya siasa havitatakiwa kuwatetea wafanyakazi, wakulima, wavuvi na makundi ya kijamii kwa kuwa kwa kufanya hivyo itakuwa ni kufanya harakati,” alisema.

Kauli za viongozi

Akizungumzia mchakato wa upitishwaji wa muswada huo, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema waliotunga muswada huo tayari wameshatunga na kanuni hatua inayonyesha dharau kwa Bunge.

“Kwa kawaida muswada wowote unapoandaliwa lazima upelekwe bungeni, ujadiliwe ndipo upitishwe. “Ukishapitishwa ndipo unapotungiwa kanuni na waziri husika, lakini huu kabla hata haujafikishwa bungeni wala kujadiliwa na kamati husika tayari umeshatungiwa kanuni. “Kwa hali ilivyo muswada huu ni mbovu na hautakiwi hata kufika kwenye korido ya ofisi za Bunge,” alisema.

Kwa upande wake mwakilishi wa CUF, Joram Bashange alisema muswada huo, una mazingira  magumu.

Viongozi waliotia saini tamko hilo na majina yao kwenye mabano ni Katibu Mkuu Chadema, Vicent Mashinji, ACT-Wazalendo (Yeremia Maganja) na Chaumma (Hashim Rungwe).

Wengine ni ADC (Doyo Hassan), CCK (David Mwaijojele), CUF (Joram Bashange), DP (Georgia Mtikila), NCCR-Mageuzi (Martin Mung’ong’o), NLD (Tozi Matwanga) na UPDP (Fahmi Dovutwa).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles