21.9 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

Vyakula vya asili vinavyopotezwa na vya kisasa

ugali

NA JANETH MUSHI,

TANZANIA ina makabila yapatayo 120, kati ya makabila hayo yapo yanayoamini kuwa aina fulani ya chakula ni cha asili na utamaduni wao.

Kwa mfano, kabila la wapare wanapenda makande, wachaga wanapenda machalari na wahaya hupenda ndizi (matoke) kama chakula chao cha asili ambavyo hupikwa kwa namna inavyovifanya kuwa vya kipekee.

Kutokana na mabadiliko yanayotokana au yaliyosababishwa na utandawazi, vyakula vya asili viko hatarini kutoweka iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Hivi sasa watu wengi hukimbilia vyakula vya kisasa ambavyo baadhi vina athari kiafya, huku ukweli ukibaki kuwa vyakula vya asili vina virutubisho vya madini kwa wingi.

Ni ukweli usiopingika kuwa leo ukipita katika hoteli na migahawa mingi, huwezi kupata vyakula vingi vya asili badala yake vyakula vya kisasa vyenye viungo vya viwandani ndiyo vimejaa.

Ripoti mbalimbali za kitabibu zimebainisha kuwa kutokana na matumizi makubwa ya vyakula hivyo, watumiaji wengi wako katika hatari ya kukumbwa na magonjwa yatokanayo na unene wa kupindukia.

Umefika wakati kwa Watanzania kubadilika na kurejea asili yetu kwa kutumia vyakula vyetu vya asili vinavyotukinga na magonjwa mbalimbali ikiwamo saratani.

Watanzania hatuna budi kubadilika, tumenyang’anywa baadhi ya tamaduni zetu, ikiwa ni pamoja na mila na desturi ila nadhani hatupaswi kuangalia vyakula vya asili vikipotea.

Kila kabila hapa nchini lina vyakula vyao vya asili ambavyo wamekuwa wakivitumia miaka yote, lakini hivi sasa vyakula vya asili vinavyotumika vimebaki vichache.

Katika hali ya utandawazi ya sasa, msukumo zaidi unahitajika kutoka kwa Serikali katika kusimamia sera zinazolenga kuongeza thamani ya vyakula vyetu vya asili.

Kila mara Serikali na wadau wengine wa maendeleo wamekuwa wakihimiza juu ya matumizi ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini, jambo ambalo kwa kiasi fulani limekuwa likizingatiwa.

Cha kushangaza watu wengi ni kwamba wamesahau ulaji wa vyakula vya asili, ambapo hivi sasa vyakula vingi vinavyotumika ni vile vya kisasa, huku matumizi ya vyakula vya asili yakipungua kwa kiasi kikubwa.

Watu wengi hususani vijana hawatumii vyakula vya asili, vyakula vingi vinavyotoka nje ya nchi vina madhara kiafya na  uandaaji wake kuanzia shambani, vinakuzwa kwa namna ambayo haijali afya ya mlaji.

Vyakula hivyo vimekuwa vikiandaliwa shambani kwa matumizi makubwa ya dawa zenye kemikali nyingi ili kupambana na wadudu, jambo ambalo husababisha  magonjwa mbalimbali  ambayo wazee wa zamani hawakuwa wakiyapata.

Huko tuendako watoto wetu hawatajua vyakula vya asili kutokana na sehemu kubwa ya utamaduni wetu kuondoka.

Watanzania tunapaswa kukumbuka kuwa miongoni mwa vitu vinavyotambulisha utamaduni wetu ni pamoja na vyakula vya asili, hivyo tujitahidi kulinda utamaduni wetu kwa kula vyakula vya asili.

Tusisahau kuwa kilimo ni moja ya fursa kubwa za maendeleo ya taifa lolote, hivyo vijana wakishiriki na kuitumia fursa hiyo itasaidia kulima kilimo kinachojali mazingira na afya ya mlaji na kulinda tamaduni zetu za asili.

Vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa lolote, hivyo katika hili vijana tunaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa kulima na kufanya biashara ya chakula, ikiwezekana kwa kushirikiana na wadau wengine kuunganisha hoteli na  wakulima, kwa lengo la kuweza kutangaza vyakula vyetu vya asili.

Ili tusipoteze uhalisia na utamaduni wa vyakula vyetu vya asili, kungekuwa na utaratibu kama ambavyo imewahi kufanywa na baadhi ya makabila kama wachaga na wahaya.

Kuwe na maonyesho ya utamaduni wa makabila ambayo yatahusisha vyakula vinavyotumiwa na makabila hayo walau mara moja kwa mwaka ili kutoa nafasi kwa makabila mengine kufanya hivyo.

Hili linawezekana ni kujipanga tu, Kijiji cha Makumbusho kilikuwa na utaratibu huu ambao kimsingi ni mzuri lakini sijui iliingiwa na jinamizi gani na utaratibu huu umekufa.

Si vyakula pekee, utaratibu huu utawezesha watu kufahamu mila na desturi za kabila husika ikiwamo ngoma, jinsi ya kuposa, jinsi ya kupika vyakula hivyo na mambo mengine kama hayo.

Utandawazi umesababisha haya yote kupungua kama si kuisha kabisa kutokana na watu kuiga na kula vya kizungu ambavyo vingi vimekuwa si halisi kutokana na kuzidiwa na kemikali za viwandani.

Suala hili halihitaji serikali ni kujipanga tu wenyewe katika kudumisha mila zetu.

Tukitia nia tukafanikiwa katika hili tutawafanya hao tunaowaiga nao kutuiga sisi kwa mfano mmiliki wa mtandao maarufu wa kijamii wa Facebook, Mark Zuckerberg hivi karibuni akiwa nchini Kenya alikula ugali na samaki chakula kilichopikwa kiasili.

Angeweza kula vyakula alivyozoea lakini hakufanya hivyo kwa sababu amekuwa akila vyakula vya kizungu muda mrefu.

Kama kusingekuwa na chakula hicho ambacho hoteli nyingi hazipiki, Zuckerberg angekula nini Kenya?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,719FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles