NA RHOBI CHACHA, DAR ES SALAAM
BEI ya vyakula katika soko la Mabibo haijapanda, tofauti na ilivyo kwenye masoko mingine katika kipindi hiki cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Kwa kawaida, wakati wa Mwezi wa Ramadhani vyakula huwa vinapanda bei, hali inayoongeza ugumu wa maisha kwa Waislamu wanaofunga na wengineo.
Akizungumza na MTANZANIA, Katibu wa Soko la ndizi Mabibo, Juma Chombo, alisema soko lao huwa hawaangalii Mwezi Mtukufu ndiyo wapandishe bidhaa, isipokuwa inategemea uingiaji wa bidhaa zenyewe.
Aidha alisema mwezi huu bidhaa nyingi katika soko lao ni za chini, isipokuwa magimbi na ndizi mzuzu ndizo zilizopanda.
“Unajua sisi tunajali sana wateja wetu, hivyo hatuwezi kupandisha bidhaa kwa sababu ya mwezi mtukufu, tunapandisha bidhaa kutokana na uigiaji wa bidhaa, kama bidhaa zikiingia nyingi hatupandishi na kama zikiingia chache ndio tunapandisha
“Ndiyo maana kwa upande wa bidhaa za ndizi mzuzu na magimbi tumepandisha kutokana na uingiaji wa bidhaa hizo, kwa sasa ndizi mzuzu mkungu ni Sh 30,000, wakati zamani ilikuwa Sh 25,000 hadi 20,000 na magimbi kiroba kidogo Sh 70,000 wakati zamani ilikuwa sh 50,000,” alisema Juma Chombo.
Alisema kuwa magimbi hayo kiroba kikubwa ni Sh 120,000, wakati zamani ilikuwa Sh 100,000.
Hivi karibuni Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mbeya, Juma Killa, amewaasa wafanyabiashara kutotumia mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kujinufaisha binafsi kwa kupandisha bei za vyakula sokoni.