29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

VURUGU NDANI YA CUF ZITAKWISHA LINI?

UAMUZI uliofanywa na Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahimu Lipumba wa kubadilisha gia angani na kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu, ndiyo ambao unaendelea kuleta migogoro isiyokwisha ndani ya Chama cha Wananchi (CUF).

Profesa Lipumba, msomi aliyebobea kwenye fani ya uchumi alitangaza kujiuzulu na kisha kuamua kutengua uamuzi wake huo baada ya uchaguzi mkuu katika hali iliyowashangaza wengi.

Kurudi katika siasa kwa msomi huyu na hususani Chama cha CUF, kunatafsiriwa kwa namna tofauti na wachambuzi wa masuala ya kisiasa.

Itakumbukwa kuwa Profesa Lipumba aliamua kujiuzulu kwa ridhaa yake mwenyewe nafasi yake ya uenyekiti wa chama baada ya kutoridhishwa na hatua ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa), kumteua Edward Lowassa kuwa mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya umoja huo kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka 2015.

Mwanzoni mwa mchakato wa kumpata mgombea kupitia Ukawa, Lipumba alikuwa akiunga mkono uteuzi wa Lowassa. Hata hivyo, haikuchukua kipindi kirefu kabla msomi huyo kugeuka na kuanza kupinga uteuzi na mwisho alijiuzulu.

Hatua ya kujiuzulu Lipumba ilielezewa na baadhi ya wachambuzi wa mambo ya siasa kama mkakati ulioratibiwa na mahasimu wa Ukawa, Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya Lowassa kuhamia Ukawa kipindi ambacho joto la siasa lilipanda sana na kuwatia hofu vigogo ndani ya CCM.

Mengi yalizungumzwa ikiwa ni pamoja na tuhuma kuwa msomi huyo alishawishiwa na vigogo wa CCM kujiuzulu na kuzungumza mabaya juu ya Ukawa kwa ahadi ambazo zilikuwa ni siri kati yake yeye na vigogo hao.

Kweli Profesa Lipumba alikaa nje ya siasa kwa kipindi chote cha uchaguzi na baada ya uchaguzi, alitangaza kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu jambo ambalo lililowashangaza wengi.

Japokuwa alirudi kwenye siasa kwa staili ya aina yake, Lipumba alionyesha kuwa alitoka kwa mpango maalumu na anarudi kwa mpango maalumu na kilichofuatia ni Msajili wa Vyama vya Siasa kutangaza kuwa alikuwa akimtambua msomi huyo kama mwenyekiti halali wa CUF, jambo ambalo lilimpa nguvu.

Profesa huyo wa uchumi alirudi ofisini chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi ambao walimlinda ili mtu asimbughudhi akiwa ofisini. Hata hivyo, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa chama hasa wa upinzani kupewa ulinzi binafsi wa umma wakati akifanya shughuli za kisiasa ofisini kwake.

Lipumba aliendelea kunufaika na misaada isiyo ya kawaida kutoka katika ofisi za umma. Baada ya kutangaza kuwa anamtambua kama mwenyekiti halali, Msajili alimpatia barua Profesa Lipumba, ambayo inadaiwa ililenga kumsaidia kufungua akaunti ya benki ili kufanikisha zoezi la kupata ruzuku ambayo kimsingi hastahili kuipata kwa kuwa wakati wenzake wakikipigania chama kwenye uchaguzi mkuu, yeye alikuwa akifanya shughuli zake binafsi.

Zoezi la kufungua akaunti ya benki lilipokuwa gumu Msajili aliamua kuweka fedha kwenye akaunti ya chama ngazi ya wilaya. Wakati wa mgogoro huu, Jaji Mutungi alinukuliwa akisema: Ofisi yake haitatoa fedha za ruzuku za CUF mpaka watakapomaliza mgogoro wao wa ndani.

Cha kushangaza ni kuwa Msajili alikiuka alichokisema mwanzoni kuwa hatalipa fedha za ruzuku kwa Chama cha CUF mpaka pande zisizoelewana kuweza kumaliza tofauti zao.

Msajili amekuwa akitumia nguvu kubwa sana kusema anamtambua Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF jambo ambalo linawafanya watu kumtilia mashaka.

Watu wanajiuliza kwanini asitumie nguvu kama hiyo kuwashauri wapatane? Kwani anavyosema anamtambua Lipumba kama mwenyekiti wakati anafahamu mgogoro uliopo maana yake ni kuwa amefunga milango ya majadiliano.

Mwishoni mwa wiki iliyopita lilitokea tukio la kuvamiwa viongozi wa CUF pamoja na waandishi wa habari wakati wakiwa kwenye mkutano katika hoteli moja jijini Dar es Salaam. Waandishi pamoja na viongozi walipigwa na watu ambao wanaaminika walitumwa na Profesa Lipumba kuvuruga mkutano huo.

Mmoja wa watu hao waliovamia na ambaye alikamatwa, alikiri wazi kuwa walikuwa wametumwa na Lipumba kuvuruga mkutano huo.

Kama ni kweli Lipumba atakuwa ndiye aliyewatuma, atakuwa ni kiongozi wa ajabu kabisa na pengine ni muda mwafaka wa yeye kufanya shughuli nyingine kwa kuwa kiatu cha siasa kinaonekana kumpwaya.

Hata kwa upande mwingine, si jambo la kushangaza kwa kuwa pamoja na usomi wake, Lipumba ameonyesha ukomavu mdogo sana wa kisiasa tangu atangaze kujiuzulu na kurudi. Kinachomvutia kwa sasa ni ruzuku ya chama na si kingine.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles