PATRICIA KIMELEMETA, ESTHER MNYIKA NA PAULINA KEBAKI (TUDARCO), DAR ES SALAAM
SIKU moja baada ya kumalizika kwa kikao cha viongozi wa dini, Serikali na vyama vyenye uwakilishi bungeni, maazimio ya kikao hicho yanatarajiwa kuwasilishwa kwa Rais Dk. John Magufuli.
Maazimio hayo yanatakiwa kumfikia rais kabla ya kufanyika kwa kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa kilichoitishwa na Msajili wa vyama hivyo, Jaji Fransis Mutungi.
Kikao hicho kilichofanyika Dar es Salaam juzi, kilikuwa na ajenda kuu mbili ambazo ni wabunge wa upinzani kususia vikao vya Bunge katika Bunge la bajeti pamoja na hali ya siasa iliyopo nchini kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Katika makubaliano ya pamoja, viongozi hao waliafikiana kuwa maazimio yote yaliyofikiwa katika hoja zilizowasilishwa na kukubaliwa, yapelekwe kwa Rais Magufuli kwa ajili ya utekelezaji kabla ya kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa kinachotarajiwa kufanyika Jumanne na Jumatano ijayo.
Akitoa maazimio ya kikao hicho kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, mmoja wa wajumbe walioshiriki, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema kwa kuwa viongozi wa dini ndio waliokiitisha, wanaamini hoja hizo zitafanyiwa kazi na kuleta mrejesho chanya kwa masilahi ya taifa.
Hata hivyo katika mkutano huo wa jana na waandishi, viongozi wa dini hawakuwapo. Walikuwa na kikao cha siri katika Hoteli ya Southern Sun kwa ajili ya kupitia maazimio hayo na kujiandaa kuonana na rais.
Mbatia alisema pamoja na mambo mengine, viongozi hao wa dini walitaka kujua sababu za kuanzishwa kwa Operesheni Ukuta na kirefu chake.
Alisema waliwaeleza kuwa Ukuta imeanzishwa baada ya Rais Magufuli kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa kinyume na ibara ya 20 (1) ya katiba pamoja na sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 kifungu cha 11.
Aidha aliongeza kuwa viongozi wa dini walitaka kujua tatizo lililowafanya wabunge wa upinzani kususia vikao vya Bunge la bajeti, ambavyo vilikuwa vinajadili masilahi ya taifa na wananchi kwa ujumla.
Awali katika mkutano na waandishi wa habari, Mbatia alisema wapinzani walieleza namna Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, anavyotumia vibaya kiti chake kwa ajili ya kutetea masilahi ya Serikali bila ya kuangalia masilahi ya wananchi.
Alisema kitendo hicho kilileta migongano ndani ya Bunge, jambo ambalo lilisababisha uhasama kwa wabunge wa CCM na wale wa upinzani.
“Pia tulijadili kuhusu kuzuiwa kuonyesha matangazo ya Bunge ya moja kwa moja ni kinyume na ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatoa uhuru wa maoni na uhuru wa kupata habari kwa kila mwananchi.
Alisema baada ya kushauriwa juu ya suala la kususia vikao vya Bunge, vyama hivyo vimekubaliana kwa pamoja kurudi kwenye vikao hivyo na kuendelea kujadili ajenda zitakazowakilishwa ili kulinda masilahi ya wananchi.
Katika kikao cha juzi, viongozi wa dini waliwakilishwa na maaskofu kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu TarcisiusNgalalekumtwa wa Iringa, Paul Ruzoka wa Tabora na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT), Fredrick Shoo pamoja na Nabii na Mtume Josephat Mwingira wa Kanisa la Efatha.
Upande wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) uliwakilishwa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum na baadhi ya masheikh kutoka Ofisi ya Mufti.
Kwa upande wa Zanzibar, waliwakilishwa na Askofu Augustino Shao wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC-Zanzibar), Naibu Mufti wa Zanzibar, Mahmoud Mussa Wadi na baadhi ya masheikh kutoka visiwani humo.
Serikali iliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiwakilishwa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana na msemaji wa chama hicho, Christopher ole Sendeka.
Vyama vyenye uwakilishi bungeni vikiongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), viliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Said Issa Mohamed na Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyeki wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira na Riziki Mngwai na Mbalala Maharagande wa Chama Cha Wananchi (CUF).
WASOMI WATOFAUTIANA
Katika hatua nyingine, wasomi waliohojiwa na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jana, wametofautiana kuhusu uamuzi wa Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya ndani ya kisiasa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, alisema katazo hilo litachochea moto wa hali ya kisiasa nchini.
“Kuna ‘political tension’ ambayo inasababishwa na mazuio ya polisi yanayoambatana na mazoezi yao yanayoendelea nchi nzima.
“Polisi wanategemea kutumia mabavu zaidi kuliko busara kupambana na watu ambao kimsingi wanadai haki yao ya msingi,” alisema.
Alilishutumu jeshi hilo kwa kufanya kazi kwa upendeleo, kwamba limekuwa likiruhusu chama kimoja kufanya mikutano na vingine vinakatazwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitila Mkumbo, alisema kinachofanyika ni kuendelea kuminya demokrasia licha ya suala hilo kupigiwa kelele muda mrefu.
“Tumeshaongea sana kuhusu suala hili. Bado ni ile dhana ya kubinya demokrasia,” alisema Prof. Mkumbo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema anaunga mkono zuio la polisi kwani anaamini wana mamlaka hayo kwa mujibu wa sheria.
“Naamini polisi kwa mujibu wa sheria ndiyo taasisi yenye mamlaka ya kutathmini na kuelewa matukio yanayoweza kuhatarisha usalama wa raia na mali zao,” alisema.
Naye mtaalamu wa masuala ya siasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ali, alisema kuna mkwamo mkubwa ambao hauna budi kutatuliwa na taasisi husika zilizopo kwenye mfumo wa demokrasia ya ubwanyenye.
Alisema endapo vyombo husika vikishindwa kutatua tatizo lililopo, basi itakuwa nchi imeshindwa mfumo wa demokrasia.
LHRC
Kwa upande wake, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimelishauri Jeshi la Polisi kuacha kuzuia mikutano ya ndani na nje ya vyama vya siasa pamoja na kuwazuia wanasiasa kwenda watakapo kwani ni kuingilia uhuru walionao kikatiba na kisheria.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, DK. Helen Kijo Bisimba, alisema haki za kiraia na kisiasa nchini kwa sasa zipo kwenye ya hali ya sintofahamu.
Alisema siku za hivi karibuni wameshuhudia Jeshi la Polisi likifanya mazoezi katika mitaa na maeneo mbalimbali nchini na kuzua hofu kwa wananchi.
“Jeshi la Polisi jukumu lake kikatiba na kisheria ni kulinda raia na mali zao, lakini limejipambanua kama jeshi la kupambana na wananchi na kufanya mazoezi na majaribio ya vifaa vya jeshi, huku wakilipua milipuko bila sababu za msingi,” alisema Dk. Bisimba.