Na Mwandishi Wetu
-DAR ES SALAAM
KAMPUNI ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, imeshinda tuzo ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, juzi, jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Uhusiano wa Uwekezaji na Miradi Maalumu wa Vodacom Plc, Robin Kimambo, alisema tuzo hiyo ni heshima kubwa kwa kampuni ambayo sasa inaongoza kwa uvumbuzi kwenye teknolojia ya mawasiliano nchini.
“Jambo la msingi ni kuwaahidi Watanzania kuwa tutaendelea kuwa wabunifu na wavumbuzi ili kuendelea kutoa huduma ambapo kwa sasa tuna takriban wateja zaidi ya milioni 14 nchi nzima,” alisema.
Tuzo hizo ziliongozwa na kauli mbiu ya ‘Mazingira, Jamii na Utawala Endelevu’, ambapo miongoni mwa wadau walishiriki ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, kampuni zilizoorodheshwa DSE pamoja na madalali au wafanyabiashara, washauri waliopendekezwa pamoja na vyombo vya habari vya kidigitali na magazeti.
Kampuni ya Vodacom Tanzania Plc iliorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam Agosti 15, 2017.
Mwisho