24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Vodacom yajipanga kutafuta bosi mwingine

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM                     |                   


KAMPUNI ya simu ya Vodacom Tanzania, imesema iko katika mchakato wa kutafuta Mkurugenzi Mtendaji mpya baada ya yule wa awali, raia wa Kenya, Sylivia Mulinge, kunyimwa kibali na Serikali   kufanya kazi  nchini.

Akizungumza Dar es Salaam jana  baada ya mkutano mkuu wa pili wa mwaka wa wanahisa, Mwenyekiti wa Bodi ya Vodacom Tanzania, Ali Mufuruki alisema kikao hicho kiliazimia kumtafuta mkurugenzi mpya ingawa itachukua muda mrefu kumpata mwingine.

“Tutachukua muda sasa kumtafuta CEO mwingine… hatutafanya kazi hii kwa haraka sana na hatutafanya kazi kwa haraka hadi kuonyesha soko kuwa bila kuwa na mkurugenzi  hakuna wasiwasi kwa sababu  viongozi waliopo kwenye kila idara wanafanya kazi zao vizuri.

“Siwezi kupanga tarehe ya kupata mkurugenzi mpya   kwa sababu  hata viongozi waliopo nao wanafanya kazi zao vizuri.

“Lakini pia tunatafuta viongozi ambao watakuwa na uwezo wa kufanya kazi na siyo CEO pekee, tutafanya hivyo katika ngazi zote za uongozi,’’alisema Mufuruki.

Alisema biashara ya simu  inabadilika kulingana na hali ya soko na kila idara ni muhimu.

Mufuruki alisema kwa sababu hiyo ni muhimu kupata viongozi wenye uwezo, kuanzia huduma za  fedha – Mpesa,  maana ni sawa na benki.

“Hii ni biashara kubwa tofauti na simu lazima kuwa na kiongozi mzuri,  lazima pia katika idara ya matangazo kuwa na kiongozi mzuri anayeweza kuwa amekamiliki katika eneo hilo pia, hivyo ni lazima kupata kiongozi mzuri kila mahali,’’ alisema.

Mufuruki alisema katika suala la  Mtendaji Mkuu kampuni haitaki  kuingia katika mgogoro na serikali ikizingatiwa  ni mara   ya kwanza kunyimwa kibali kwa mfanyakazi kutoka nje ya nchi.

Alisema   si kampuni hiyo  pekee  inayoajiri Ofisa Mtendaji Mkuu kutoka nje ila hata kampuni nyingine za simu kama Halotel, Airtel  nazo si mara  ya kwanza kufanya hivyo.

“Niseme tu hatutaki kuingia ugomvi na serikali yetu kama  walivyoamua wao ingawa ndiyo ndiyo mara ya kwanza kutokea kitu kama hiki.

“Lakini pia kuna kampuni nyingine kama vile Halotel, Airtel wameajiri kutoka nje hivyo si ajabu pia,’’ alisema Mufuruki.

Ofisa Mtendaji Mkuu  wa Vodacoma Tanzania raia Kenya aliyezuiwa kwa sasa ni mkurugenzi wa miradi wa Safaricom na alikuwa akisubiri kibali cha kufanya kazi Tanzania kwa takriban miezi minne tangu ateuliwe.

Kwa sasa nafasi hiyo ya Ofisa Mtendaji Mkuu  inakaimiwa na  Hisham Hendi hadi atakapopatikana wa kuziba nafasi hiyo.

Mufuruki  alisema pia kuwa  licha ya kuwa na changamoto nyingi katika biashara, kampuni imeweza  kuongeza idadi ya wateja ambako  mwaka jana    milioni 12.9 na   mwaka huu wamefikia  wateja milioni 13.2.

Alisema  kampuni ina  wanahisa zaidi ya 40,000 na katika kila hisa moja litatolewa gawio la Sh 17.33 wakati wowote kuanzia sasa hadi Novemba 30, mwaka huu

Baadhi ya wanahisa walilalamikia kuahidiwa kupewa mara mbili ya gawio la sasa lakini Mufuruki alitoa ufafanuzi kuwa gawio la hisa litatolewa moja kutokana na changamoto za biashara zinazokwenda na sheria mbalimbali zilizowekwa ingawa kampuni imejipanga vema.

“Pamoja na ushindani mkubwa wa biashara,  tumewaeleza wanahisa kuwa tumejipanga vema, soko bado tunalo na tunafanya vizuri.

“Tutahakikisha tunaendelea kufanya vizuri zaidi katika soko na mfano mzuri ni katika ongezeko la wateja wetu,’’ alisema Mufuruki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles