Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Kampuni ya Vodacom Tanzania, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) pamoja na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (Costech) wametangaza ushirikiano wa pamoja wa kuandaa Wiki ya Ubunifu Tanzania 2025 (IWTz2025).
Tukio hili litakalojumuisha Mkutano wa Future Ready wa Vodacom litafanyika kuanzia Mei 12 hadi 16,2025 jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia leo Februari 5,2025 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Phillip Besiimire, amesema ushirikiano huo utaleta mabadiliko katika sekta ya ubunifu nchini kwa kuunganisha wabunifu na wajasiriamali wa kimataifa kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Amesema mkutano wa Vodacom wa Future Ready Summit (FRS2025) ni tukio linaloweka msingi wa maadhimisho hayo.
Mkutano huo uliobeba kaulimbiu ya ‘Kubadilisha hatma ya miji: Usasa, Uendelevu na Jumuishi’, inasisitiza umuhimu wa kubadili miji ya Tanzania kwa ajili ya kutatua changamoto zinazotokana na ukuaji wa kasi, mabadiliko ya tabia nchi na mabadiliko ya teknolojia.

Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara, amesisitiza dhamira ya kujenga mfumo wa ubunifu ulio jumuishi na wenye ustahimilivu.
“Tunatambua kuwa ubunifu ni nyenzo muhimu katika kushughulikia changamoto za maendeleo endelevu na kuunda fursa shirikishi hivyo kupitia ushirikiano huu tunalenga kuwainua Watanzania hasa vijana na wanawake, kuwa chachu ya mabadiliko chanya,” amesema Komatsubara.
Amesema wiki ya Ubunifu Tanzania 2025 (IWTz2025) itaonyesha ari ya ubunifu Tanzania kwenye jukwaa la kimataifa, kuvutia uhamasishaji na ushirikiano kupitia na mifumo iliyofanikiwa duniani.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Mkurugenzi wa Kituo cha Maendeleo na Uhamisho wa Teknolojia kutoka Costech, Dk. Athumani Ngumia amesema mchango muhimu wa ushirikiano huo ni kukuza ubunifu.
“Costech imejidhatiti kuwaunganisha wadau kwa lengo la kuchochea utafiti, teknolojia na ubunifu ambao unaendana na vipaumbele vya nchi katika maendeleo na maono ya mwaka 2050,” amesema Dk. Ngumia.
Mada Kuu mada ya mwaka huu ni ‘Ubunifu kwa Maendeleo Jumuishi na Yenye Ustahimilivu’ ikilenga kuonyesha dhamira ya pamoja ya kujenga jamii endelevu, jumuishi na ya kisasa katika kutatua changamoto ya ajira kwa vijana kwenye zama hizi za kidijitali na kuchochea ukuaji wa kibiashara kupitia tafiti na ubunifu.
Wiki ya ubunifu 2025 (IWTZ2025) na mkutano wa Future Ready Summit (FRS2025) inatarajia kuwaleta pamoja washiriki, wazungumzaji na wabunifu kutoka Tanzania, Afrika na sehemu mbalimbali duniani na kubadilishana maarifa, kuendeleza ushirikiano wenye tija na kuhamasisha mawazo yenye kuleta mabadiliko.