25.9 C
Dar es Salaam
Friday, May 27, 2022

Viwanja vinavyozitesa Simba, Yanga

simba-yangaNa ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM

KIMFAACHO mtu chake, kwa hakika Simba na Yanga wanapaswa kufahamu hili ili liwafae na kuwa somo kwao.

Sasa hivi ni wazi kuwa klabu za Simba na Yanga zinatapatapa kuhusiana na uwanja kutokana na Serikali hivi karibuni kupitia kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kuzuia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutumiwa na klabu hizo kwa muda usiojulikana kutokana na uharibifu wa mali uliofanywa na mashabiki wao.

Uwanja wa Taifa ndio mkubwa kuliko viwanja vyote nchini unaochukua watazamaji 60,000 na ndio bora barani Afrika.

Uwanja wa Taifa ulijengwa mwaka 2007 ukiwa sawa na ule wa Kasarani wa Mathare nchini Kenya ambao unachukua watazamaji sawa.

Mashabiki wa Simba  na Yanga walifanya uharibifu wa viti na mageti ya uwanja huo, katika mechi yao iliyochezwa Oktoba mosi  mwaka huu na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Kutokana na zuio hilo, klabu hizo kongwe zipo kwenye wakati mgumu  wa kuchagua ni viwanja gani watavitumia kucheza mechi zao za Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa wenyeji.

Yanga wao walitoa taarifa ya kuomba kuutumia Uwanja wa Amaan, Zanzibar lakini ikashindikana kutokana na sheria na kanuni za soka kutoruhusu timu yoyote inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa na uwanja nje ya sehemu husika ligi inapochezwa.

Kwa upande wa Simba wao wameiomba radhi Serikali kwa jambo lililofanywa na mashabiki wake, huku wakiiomba iwaruhusu kuutumia uwanja huo.

Ni jambo la kushangaza kwani licha ya ukongwe wao wamepitwa hata na Azam FC ambayo imeanzishwa miaka ya 2000, lakini wanamiliki uwanja pamoja na hosteli kwa ajili ya wachezaji wake.

Lakini gharama wanazozitumia Simba na Yanga kukodisha viwanja vya mazoezi si chini ya Sh 300,000 kwa siku, laiti wangekuwa na eneo lao gharama hizi zisingewakuta.

Kwa sasa wamekuwa wakihaha kutafuta uwanja wa mazoezi na mara kwa mara wamekuwa wakipokezana Uwanja wa Polisi Kurasini.

Ni aibu kubwa, hili linapaswa kuwa somo kwa klabu hizi, tena ipo haja ifahamike kuwa Uwanja wa Taifa una hadhi yake na unapaswa kutumika kwa matukio makubwa hasa yanayohusu taifa, labda tu inapotokea wanacheza michuano mikubwa, hapo ndipo hupata heshima ya kuutumia na si vinginevyo.

Klabu ya Shrewsbury Town inayoshiriki Ligi Daraja la Pili (Legue One) nchini England ina uwanja mdogo uitwao Greenhous Meadow, lakini licha ya udogo wake unaochukua watazamaji 9,875, lakini imewahi kucheza na Chelsea katika uwanja huo katika mechi ya raundi ya nne ya michuano ya kuwania taji la Capital One Oktoba 28 mwaka juzi.

Tukirejea hapa Tanzania, hali ni tofauti na hili sasa la kuufungia Uwanja wa Taifa, linaweza kuzisaidia klabu hizi kujenga viwanja vyao, kwani licha ya kuharibu miundombinu ya uwanja huo, lakini limekuwa likiminya uhuru wa klabu nyingine katika ligi kuu.

Simba na Yanga haziendi kucheza mechi zake za ligi na zile za Kombe la FA ugenini katika Uwanja wa Azam Complex unaomilikiwa na  Azam FC, Uwanja wa Mabatini (Ruvu Shooting, JKT Ruvu), Karume (African Lyon) wala ule wa Manungu unaomilikiwa na Mtibwa Sugar.

Msimu huu kwenye Ligi Kuu England (EPL) iliyoanza Agosti 13, 2016, Uwanja wa Vitality unaomilikiwa na Bournemouth, ndio uwanja mdogo kuliko wote kwa timu zote za ligi hiyo ukiwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 11,464, lakini timu zote zitalazimika kwenda kucheza hapo zitakapocheza ugenini dhidi ya wenyeji hao.

Lakini hapa nchini Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), linavitambua viwanja vinne vyenye uwezo wa kuchezewa mechi za kimataifa zinazoandaliwa na mashirikisho hayo, ambavyo ni Taifa, Uhuru na Azam Complex vya Dar es Salaam pamoja na ule wa CCM Kirumba, Mwanza.

Na ili viwanja vipewe hadhi hiyo lazima viwe na baadhi ya vitu kama sehemu nzuri ya kuchezea (pitch), uzio wa kutenganisha sehemu ya kuchezea na majukwaa ya mashabiki, vyumba vinavyokidhi vya kubadilishia nguo (dressing room), ubao wa matokeo (scoring board), chumba cha kupima wachezaji (doping room), chumba cha kukaa wasimamizi wa mchezo (official room).

Sasa Simba na Yanga, ni lazima wajifunze kuwa wanapswa kuwa na viwanja vyao, wanajishusha hadhi kufanya mazoezi katika viwanja visivyo na sifa kama Kinesi, TCC Chang’ombe, Bora na kwingineko.

Laiti wangekuwa na viwanja vyao ingekuwa jambo bora na heshima sana kwao, hata mechi zao wenyewe zingekuwa zikichezwa katika viwanja vyao.

Sasa klabu hizi zinabidi zikubali kuwa ‘watumwa’ wa kutafuta viwanja nje ya Dar es Salaam jambo ambalo litawasababishia wanachama na mashabiki wao kuzifuata huko kwa gharama kubwa.

Sasa Simba na Yanga baada ya Uwanja wa Taifa, wanaweza kufuata viwanja kama CCM Kirumba wa Mwanza ambao ni uwanja wa pili kwa ukubwa ukichukua watazamaji 45,000 na ulijengwa mwaka 1980 na ni mali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Huu kwa sasa unatumiwa na Toto Africans na Mbao hivyo ni ngumu kwa Simba na Yanga kwenda huko.

Kutokana na jiografia ilivyo, Simba na Yanga itabidi wakune vichwa kwa kuangalia viwanja vilivyopo kwenye mikoa ya jirani kama Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, ambao unamilikiwa na CCM na unachukua watazamaji 20,000.

 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ambao unachukua watazamaji 20,000, huu hauna timu ya ligi kuu kwa sasa.

 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha ambao hauna timu ya Ligi Kuu, unamilikiwa na CCM na unachukua watazamaji 25,000.

Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, unamilikiwa na Serikali pia, unachukua watazamaji 15,000, ni ngumu kwa Simba na Yanga kuutumia katika mechi zake kubwa kutokana na idadi ya watazamaji.

Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kwa sasa hauna timu ya Ligi Kuu kutokana na timu zake tatu za Coastal Union, Mgambo na African Sports kushuka daraja msimu uliopita.  

Uwanja huu unamilikiwa na CCM na unachukua watazamaji 15,000, hivyo Simba na Yanga wanaweza kuomba kuutumia pia kama uwanja wao wa nyumbani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,528FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles