FLORENCE SANAWA, MTWARA
VIWANDA vinne vya kubangua korosho vimeingia mkataba na Serikali kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kwa ajili ya kubangua korosho zaidi ya tani 7,500 mkoani Mtwara.
Mkataba huo umefikiwa jana baada ya Serikali kufanya mazungumzo na viwanda hivyo ambapo hadi sasa imekusanya zaidi ya tani 200,000.
Akizungumza katika kikao na wamiliki wa viwanda hivyo, Waziri wa Kilimo, Japhet
Hasunga, alisema Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kuwa korosho
zinabanguliwa hapa hapa nchini.
Aliongeza kuwa ubanguaji wa korosho
hapa nchini mbali na kuongeza ajira nchini bado Serikali itaingiza mapato
kupitia korosho zilizobanguliwa kuliko kuuza korosho ghafi nje ya nchi.
“Unajua zoezi la ubanguaji lilishaanza katika Shirika letu la Viwanda vidogo
vidogo (Sido) ambapo wameajiri wafanyakazi 155 mara baada ya kuingia mkataba na
bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko ambapo tunaamini watazingatia ubora wa
kubangua korosho.
“Tunatamani kuona korosho zetu zikiuzwa duniani kwa jina la nchi yetu kwa kuwa
sisi ndio wazalishaji wa korosho bora duniani, tuna kila namna ya kuboresha na
kuongeza thamani zao hili kutokana na uwezo mkubwa wa kuchangia pato la taifa.”
“Awali Serikali ilichukua Kiwanda cha Buko kilichopo mkoani Lindi lakini
sasa kitaitwa Kiwanda cha Ubanguaji Lindi baada ya ukarabati, kinatarajiwa
kuanza kazi hivi karibuni lakini pia Serikali inachukua kiwanda cha Agrofocus
cha Newala, lakini bado tuko kwenye mazungumzo na kampuni nyingine ambazo
zitaongezeka hivi karibuni,” alisema Hasunga.
Kwa upande wake Ofisa Mawasiliano na Mahusiano wa Kiwanda cha Export Trading
Group, Frank Mtui, alisema wamepokea korosho kwenye viwanda vyao vitatu ambapo
katika kiwanda cha Micronix Newala watabangua tani 2,400, Micronix Mtwara tani 1,200
na Korosho Afrika tani 2,400.
“Viwanda vyetu vyote vitatu vina uwezo wa kubangua tani 12,500 kwa sababu tumeshachelewa tutaweza kubangua
tani 10,000 tu, hivi sasa tumechukua chache kwa kuwa mikataba iko wazi tunatarajia
tukimaliza tutachukua nyingine.
“Unajua ukisimama bila kubangua korosho kwa muda mredu ni madhara zaidi,
lakini kitendo cha Serikali kutuletea korosho kwetu imesaidia hata wafanyakazi
wa kiwanda chetu kupata ajira,” alisema Mtui.
Naye Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha Hawte Investment Limited, Saadat Abdul, alisema
kiwanda hicho kinatarajia kuanza ubanguaji mwezi huu ambapo wafanyakazi wote
watarejea kazini.
“Sisi tuna wafanyakazi 700 ambao ndio walikuwa wakifanya ubanguaji wa
korosho, lakini walienda likizo kwa muda sasa upatikanaji wa korosho hizi
utarejesha wafanyakazi wote kazini ambapo tunatarajia kufungua kiwanda Januari 17
na uwezo wetu kwa mwaka ni tani 1,500 ingawa tunatarajia kuongeza uzalishaji
hivi karibuni,” alisema Abdul.