28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

VIWANDA 10 VYARUDISHWA SERIKALINI

Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA

SERIKALI imevichukua viwanda 10 na kurejesha umiliki wake serikalini katika awamu ya kwanza ya mpango huo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema viwanda hivyo vimechukuliwa baada ya mikataba ya mauzo kuchambuliwa na kubainika wamiliki wake wamevunja makubaliano.

Katika mkutano huo na waandishi, alikuwapo pia Naibu Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo, Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Antony Mavunde, na watendaji mbalimbali wa Serikali.

Katika maelezo yake, Mwijage alisema baadhi ya watu hawajui ni kwa nini Rais Dk. John Magufuli alisisitiza hivi karibuni umuhimu wa kufuta umiliki wa viwanda hivyo.

Mwijage alivitaja viwanda vilivyorudishwa serikalini kuwa ni Kiwanda cha Korosho Lindi, Mgodi wa Pugu Kaolin, Mkata Saw Mills Ltd, Manawa Ginnery Co. Ltd, Dabada Tea, Tembo Chipboard Ltd, Kilimanjaro Textile Mills, Mang’ula Mechanical and Machine Tools Co. Ltd, National Seal Coperation na Porikasadar.

“Pamoja na kwamba nimetaja orodha hiyo, ieleweke kwamba orodha hiyo siyo ya mwisho kwa sababu wataalamu bado wapo kazini.

“Tunataka zoezi hili tulimalize tarehe 22 mwezi huu na kama tarehe hiyo kuna mtu hajafika ofisini, basi itakuwa ni bahati mbaya kwake kwa sababu tunapenda viwanda vyote vifanye kazi.

“Wawekezaji wa viwanda hivi, tunawataka walinde viwanda vyao hadi makabidhiano rasmi na ofisi ya msajili wa hazina yatakapofanyika.

“Pamoja na kuvirudisha serikalini viwanda hivyo, kiwanda cha Mwanza Tanneries kimerudishwa na mmiliki kwa ridhaa yake mwenyewe,” alisema Mwijage.

Kuhusu viwanda ambavyo Serikali itavichukulia hatua, alivitaja kuwa ni Sabuni Industries Ltd, Tanzania Moshi Pesticides, Tanzania Bag Corporation, Ilemela Fish Processing Plant na Mzizima Maize Mill.

Wakati huo huo, Mwijage alisema viwanda vilivyobadilishwa matumizi bila idhini ya msajili wa hazina, wamiliki wake wanatakiwa kuwasiliana na msajili huyo kabla hawajachukuliwa hatua.

Pia, alisema tathmini iliyofanywa na ofisi ya msajili huyo mwaka 2015-2016 na kushirikisha wizara yake, inaonyesha viwanda 62 vinafanya kazi vizuri, viwanda vinavyofanya kazi kwa kusuasua ni 28, viwanda vilivyofungwa ni 56 na viwanda vilivyobinafsishwa kwa kuuza mali moja moja ni 10.

“Kwa hiyo, kati ya viwanda 156 vilivyofungwa, ufufuaji wa viwanda 11 umeanza,” alisema.

Akizungumzia viwanda ambavyo wamiliki wake wameonyesha utayari wa kuvifufua, alivitaja kuwa ni Bora Shoes, DOWICO, MOPROCO, Newala 1, TABOTEX, Kinu cha Manonga, Morogoro Canvas Mills (MCM) na Morogoro Shoes.

Alivitaja viwanda vingine kuwa ni Ubungo Garment Ltd, Kibaha Cashewnut Plant, Shinyanga Meat Factory, MWATEX, Urafiki na Mutex.

Alivitaja viwanda vilivyopata wawekezaji kuwa ni Morogoro Canvas Mills, Mwanza Textile, Kiwanda cha Nguo cha Urafiki, MUTEX ya Musoma na Mwanza Tanaries.

Hivi karibuni, Rais Magufuli alionyesha kutoridhishwa na utendaji kazi wa Waziri Mwijage kwa kuwa alikuwa haonyeshi nia ya kurudisha serikalini viwanda visivyofanya kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles