24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

VIVIAN: BINTI ALIYEPATA ULEMAVU GHAFLA AKIWA MATEMBEZINI

Vivian akisaidiwa kunyanyuka na ndugu zake

 

 

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

HUJAFA hujaumbika, ndivyo unavyoweza kusema iwapo utakutana na Vivian Filbert (21), Mkazi wa Chasimba, jijini hapa.

Vivian alizaliwa mwaka 1996 akiwa hana ulemavu wa aina yoyote lakini sasa ni mlemavu wa miguu na mikono.

Hivi majuzi, MTANZANIA lilimtembelea Vivian nyumbani kwao na kufanya naye mahojiano.

Akisimulia kisa kilichomsababishia kupata ulemavu, Mama mzazi wa binti huyo, Mariam Hamis anasema hali hiyo ilianza kujitokeza alipokuwa na miaka 13.

“Vivian ni mwanangu wa pili, hakuwa na tatizo lolote, alipofikisha miezi minne baba yake naye alifariki dunia, tangu wakati huo maisha yetu yalibadilika, yakawa magumu,” anasema.

Anadai baada ya kifo cha mumewe, ndugu waliteka mali, kuziuza na kugawana wenyewe bila kujali kwamba aliacha familia.

“Ikabidi wanangu wachukuliwe na babu yao (upande wa baba) wakalelewa huko, mimi nikarudi kwetu hadi nilipobahatika kuolewa tena na mwanamume ambaye naishi naye hadi leo,” anasema.

Jinsi alivyopata ulemavu

Anasema Vivian akiwa na umri wa miaka 13 alikuwa darasa la tatu, alianza kuishiwa nguvu miguuni na kushindwa kutembea.

“Kumbuka alikuwa anaishi na babu yake, kila walipofunga shule alikuwa anakuja kukaa na mimi nyumbani kwangu hasa wakati wa sikukuu.

“Siku moja nilishangaa kuona akitembea katika hali isiyokuwa ya kawaida, alikuwa kama mtu anayejitahidi kunyanyua miguu atembee lakini hakuweza, ulianza mguu wa kushoto kupata tatizo,” anasimulia Mariam.

Anasema alimuuliza mwanawe kwanini hali hiyo ilimtokea hata hivyo hakuweza kueleza.

Vivian anasema; “binafsi sikuelewa nimepatwa na nini, nilishangaa mno, siku moja tulikwenda kutembea na marafiki zangu (ilikuwa sikukuu) ghafla nikashindwa kabisa kutembea, nikadondoka chini, sikuweza tena kutembea,” anasema.

Anasema marafiki zake hao walimnyanyua na kumshikilia ili aweze kutembea wakamrudisha nyumbani kwao.

“Tangu siku hiyo sikuweza tena kunyanyuka kadri muda unavyosonga mbele ndivyo hali yangu inavyozidi kuwa mbaya,” anasema kwa huzuni.

Safari ya kusaka tiba

Ni miaka saba sasa tangu Vivian apatwe na hali hiyo, Mariam anasema jambo hilo linampa huzuni na simanzi kubwa ndani ya moyo wake.

“Awali majirani walinishauri nimpeleke kwa waganga wakidai huenda amerogwa, nikampeleka huko lakini hakupona wala kupata nafuu, ndiyo kwanza hali ilizidi kuwa mbaya,” anasimulia.

Anasema hali hiyo ilimlazimu kumpeleka Hospitali ya CCBRT iliyopo Msasani.

“Daktari aliyemfanyia uchunguzi alitueleza kwamba alikuwa na tatizo la upungufu wa vitamin mwilini na kwamba anatakiwa apewe dawa maalumu ambazo zingemsaidia,” anasema.

Anasema dawa hizo zilikuwa zinauzwa Sh 100,000 fedha ambazo hakuwa nazo ikawalazimu kurudi nyumbani.

“Maisha yetu ni duni, sikuwa na fedha hizo, ili nipate fedha ya kujikimu nilikuwa naenda kuponda kokoto mimi na mume wangu, kule tunalipwa kwa wiki Sh 20,000 hadi 25,000 fedha ambazo ni kidogo mno kuendesha maisha,” anasema.

Anasema wapo ambao walimshauri ampeleke kwenye maombezi, alifanya hivyo lakini bado hali ya Vivian iliendelea kuwa mbaya.

“Nilikuwa nampeleka katika kanisa moja (analitaja) huko Mwenge, ili tufike huko nalazimika kumbeba mwanangu mgongoni. Niliwahi kwenda hadi Kibaha kufuata maombezi, lakini yeye ni mzito kuliko mimi ikafika kipindi nikachoka, sikumpeleka tena hadi leo,” anasema.

Hawezi tena kuponda kokoto

Mariam anasema analazimika kukaa nyumbani kumlea mtoto wake huyo maana hawezi kufanya chochote bila msaada.

“Dada (mwandishi), nimelazimika kuacha kwenda kuponda kokoto ili nimsaidie mwanangu, mume wangu analazimika kwenda huko mwenyewe ili tupate fedha za kujikimu.

“Hawezi kabisa kutembea, hapo alipokaa ndivyo hivyo hivyo, akihitaji kwenda hata msalani inabidi nimbebe nimpeleke, kujisafisha inabidi nimsaidie.

“Naumia mno kumuona mwanangu katika hali hiyo, nikimuacha hapa nani atamsaidia? Bora ikiwa wakati wa kiangazi angalau anakuwa anasota chini kutoka sehemu moja hadi nyingine ikiwa anahitaji kitu fulani, sasa hivi ni kipindi cha mvua, nje kumelowana inabidi nimbebe mwenyewe,” anasema Mariam kwa masikitiko.

Ndugu wamemtenga

Mariam anasema hakuna ndugu hata mmoja aliyefika japo kumjulia hali Vivian.

“Wametutenga tangu baba yao alipofariki, msaada mkubwa naupata kwa huyu mume wangu, kama hivi sasa yupo huko kibaruani akitafuta fedha, ili tuishi,” anasema kwa masikitiko.

Ombi lake kwa Watanzania

Mama huyo anasema anahitaji kumpeleka mwanawe huyo Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako ameambiwa ndiko kwenye matibabu mazuri ya kibingwa.

“Kuna daktari mmoja aliwahi kuniambia kwa hali aliyonayo mwanangu anahitajika kufanyiwa vipimo vya uchunguzi mwili mzima, kuanzia ubongo wake na uti wa mgongo,” anasema.

Anasema hata hivyo alimjulisha kuwa ili kufanikisha matibabu hayo anahitaji kuwa na kiasi cha kutosha cha fedha kulipia huduma.

“Suala hilo ndilo linaloniumiza kichwa hadi nikaomba uje, kama nilivyoeleza awali, shughuli niliyokuwa nafanya na mume wangu ni kuponda kokoto, sasa hata kwenda kuponda kokoto siendi, anaenda mume wangu peke yake.

“Nimelazimika kufanya hivyo ili nimsaidie mwanangu, fedha tunayopata ni ndogo, siwezi kufanikisha matibabu ya mwanangu,” anasema.

Anasema jambo jingine analohitaji watanzania wamsaidie ni angalau kupata baiskeli ambayo itamuwezesha Vivian kutembea.

“Naamini itamsaidia mno hasa kama nitakuwa sipo nyumbani kwa dharura, japo mikono yake nayo imeanza kulemaa lakini bado ina nguvu si kama miguu ambayo yenyewe haina nguvu kabisa na ana ulemavu wa kusikia, naamini itamsaidia kutoka eneo moja hadi jingine akibaki mwenyewe nyumbani,” anaongeza.

Daktari anena

Mtaalamu wa Fisiolojia ya Mazoezi na Homon, Dk. Fredirick Mashili anasema kitaalamu upo uwezekano wa mtu kukakamaa viungo vya mwili kutokana na ukosefu wa vitamin mwilini.

“Uwezekano huo upo, ingawa si ‘common’sana, kwa sababu vitamin huwa zinahusika kwenye matatizo ya mfumo wa fahamu, lakini mara nyingi huwa hayafikii katika ‘level’ ya mtu kukakamaa,” anasema.

Dk. Mashili ambaye pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) anasema kwa kuwa amekakamaa ni wazi tatizo lipo kwenye uti wa mgongo au ubongo wenyewe.

“Tatizo halipo kwenye mishipa ya pembeni, ikiwa shida ipo kwenye mishipa ya pembeni, mwili wa mtu huwa legelege, lakini likiwa kwenye ubongo na uti wa ubongo huwa mwili unakakamaa,” anasema.

Anasema mtu huweza kupata tatizo hilo iwapo mwili wake utshambuliwa na virusi, ugonjwa wa uti wa mgongo, bakteria, fangasi na vimelea vyote vinavyosababisha magonjwa mbalimbali.

“Ugonjwa wa uti wa mgongo husababisha shingo kukakamaa, lakini pia mtu akikosa virutubisho vya chakula ikiwamo vitamin, madini na vinginevyo huweza kusababisha mwili kuathirika,” anasema.

Anasema sumu za aina zote nazo huweza kusababisha mtu kupata tatizo na kuumia mwili kutokana na ajali.

“Matibabu yake huwa ya muda mrefu atapewa dawa mbalimbali lakini pia sehemu kubwa ya matibabu huhusisha mazoezi ya viungo,” anasema.

Ikiwa umeguswa na kisa hiki cha Vivian na unataka kumsaidia wasiliana na namba hizi 0652 170 521 au 0713 658 523.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles