23 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Viungo vya binadamu vyazua balaa

Mtanzania
Mtanzania

Aziza Masoud na Neema Bariki (TSJ), Dar es Salaam

SAKATA la kutupwa kwa viungo vya binadamu limezidi kuzua balaa, baada ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kusema Chuo Kikuu cha Kimataifa, Matibabu na Teknolojia (IMTU) kimepoteza sifa ya kufanya tafiti na kutoa mafunzo ya tiba kwa kutumia viungo au miili ya binadamu.

Kauli ya MAT imekuja siku moja baada ya Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, kuthibitisha kutupwa kwa masalia ya miili ya binadamu ambayo ilionekana katika bonde la mto Mpiji, Mbweni eneo la Bunju na kukiri kuwa wahusika wa tukio hilo ni watumishi wa Chuo cha IMTU.

Mpaka jana jeshi hilo linawashikilia watu wanane wakiwemo madaktari wa chuo hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Rais wa MAT, Dk. Primus Saidia, alisema kitendo cha kutupa masalia hayo kwa kiasi kikubwa kimekiuka sheria, taratibu, utu wa binadamu, maadili ya ufundishaji na taaluma ya udaktari.

“Watu na taasisi iliyohusika na kitendo hiki wote kwa pamoja wamepoteza sifa ya kufanya tafiti au kutoa mafunzo kwa kutumia viungo au miili ya binadamu.

“Hii ina maana kama ni taasisi ya utafiti imepoteza sifa ya kufanya tafiti na mafunzo…imepoteza sifa zote za kutoa tiba kwa binadamu,” alisema Dk. Saidia.

Alisema kitendo hicho katika nchi nyingine kinatosha kabisa kuifungia taasisi kuendelea na mafunzo, tafiti au huduma kwa binadamu.

Alisema katika tasnia ya tiba nchini na duniani kote, kuna utaratibu wa kutumia viungo vya binadamu kufundishia na kufanyia tafiti mbalimbali za afya ambao ni wa kawaida na unakubalika kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa.

Alisema miili na viungo hivyo hutumika kwa heshima kubwa kama walimu wa kwanza katika mafunzo na tafiti za tiba ya mwanadamu.

Alisema tafiti na mafunzo hayo, ndiyo nguzo kuu ya kukuza ufahamu wa mwili wa binadamu na kusaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya.

Alisisitiza taratibu za kuipata, kusafirisha, kuhifadhi, kutumia na kusitiri mabaki baada ya matumizi hufanyika kwa kufuata sheria, maadili, afya ya jamii, utamaduni, miiko na heshima kwa utu wa binadamu na jamii husika.

“Daktari yeyote mwenye ngazi ya kuanzia stashahada hawezi kufikia hatua ya udaktari kabla ya kupitia mwili wa binadamu aliyekufa,” alisema Dk. Saidia.

Alisema sheria ya mwili wa binadamu kutumika katika tafiti na mafunzo ipo tangu mwaka 1963, isipokuwa haijulikani kwa watu wa kawaida.

Kuhusu kubadilishana maiti ya nchi moja kwenda nyingine kwa mafunzo, Dk. Saidia alisema suala hilo linaruhusiwa endapo mhusika akiwa hai na kama atakubali kwa maandishi na kuwa anahitaji mwili wake kwenda nchi fulani kwa ajili ya mafunzo.

Alisema baada ya kutumika kwa miili hiyo, hutakiwa kuzikwa au kuchomwa moto hadi kuwa majivu kabisa na sio kuitupa kiholela kama walivyofanya.

Alisema MAT inatoa wito kwa vyombo husika kama Jeshi la Polisi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Baraza la Madaktari Tanzania, Tume ya Usimamizi wa Vyuo Vikuu (TCU), Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika wote.

“Mbali ya kutaka vyombo vya dola kuchukua hatua, tunachukua fursa hii kuwatoa hofu wananchi na kuwaomba wawe watulivu wakati vyombo husika vikichukua hatua stahiki,” alisema Dk. Saidia.

WIZARA YA AFYA

Naye Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja, alisema IMTU imefanya kitendo kipya katika tasnia ya kitabibu kwani kuna utaratibu wa kuhifadhi miili hiyo.

Alisema kiutaratibu kila hospitali na taasisi za tiba, zinatakiwa kuwa na vifaa vya kuteketeza miili iliyokwishatumika katika mafunzo.

“Ni tukio jipya katika jamii yetu, kwa maana hiyo hata sisi tumepatwa na mshtuko na tumetuma wataalamu wa kuchunguza kiini cha tatizo hili ambalo halijawahi kutokea nchini,” alisema Mwamwaja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles