JOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM
KWA mara nyingine wanasiasa wa Afrika wameonesha rangi yao halisi kuashiria Bara hili lina safari ndefu ya kukomaa kisiasa na kidemokrasia kuanzia serikalini hadi ngazi ya vyama vya siasa.
Mbali ya wajibu wao unaofahamika kwa Taifa, wanasiasa hutakiwa kuwa mfano kwa wapiga kura wao hususani vijana na watoto ili kuchochea Taifa imara na komavu kisiasa la kesho.
Hilo huwezekana vijana wanapoishi katika utamaduni, ambao baba au baba zao wanasiasa wanavumiliana ili kuweka mbele maslahi ya Taifa, wanaheshimu, kuitii na kuogopa kuikiuka Katiba na sheria nyinginezo.
Bila kizazi cha wanasiasa kilichopo kuheshimu na kutii misingi ya Katiba na Sheria walizoshiriki kuzitengeneza na kuzipitisha, kizazi cha wanasiasa wanaofuata hakitakuwa tofauti na wao kwa vile kinaishi kikijifunza utamaduni ule ule wenye mmomonyoko wa maadili, ukiukaji wa Katiba, haki za binadamu, kukosa kuvumiliana kisiasa.
Mwenendo huo mbaya ulioanza tangu Mataifa ya Afrika yajipatie uhuru wao kabla na baada ya mwaka 1960, ikichagizwa na kutoachiwa misingi mizuri na wakoloni mbali ya changamoto nyingine imeendelea hadi leo.
Vizazi vinavyopishana katika majukwaa ya siasa Afrika vimeshindwa kubadilika kutokana na kukosekana kwa ‘kiongozi wa mabadiliko’ au kuzidiwa na uwekaji mbele maslahi binafsi kabla ya Taifa.
Matokeo ya hali hii ni kuendelea kwa tawala kandamizi, za kiimla, kijeshi, kidikteta na hivyo kuchelewesha maendeleo na ustawi wa Taifa.
Lakini kuna mataifa machache, ambayo yamepiga hatua katika ukomavu wa kidemokrasia na kuashiria kumbe Afrika ikiamua inaweza kupiga maendeleo katika eneo hilo sawa na mataifa mengine yaliyoendelea.
Hata hivyo, licha ya mafanikio yaliyofikiwa kisiasa na kidemokrasia katika miongo ya karibuni miongoni mwa mataifa haya machache ya Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika, baadhi yamekuwa yakipiga hatua moja, mbili, tatu mbele na baadaye kurudi hatua hizo au zaidi nyuma.
Kenya ni mfano. Kwa mara ya pili imeonesha mfano mbaya, baada ya awali kumwagiwa sifa kuwa miongoni mwa demokrasia komavu barani Afrika na pengine kiongozi kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
Sifa hiyo ilianzia pale kilichokuwa Chama tawala cha tangu Uhuru, KANU kilipokubali kushindwa katika Uchaguzi Mkuu na kukabidhi madaraka kwa amani kwa uliokuwa Muungano wa upinzani wa NARC mwaka 2002.
Hata hivyo, sifa hiyo ya muda mfupi ikaharibika mwaka 2007 wakati matokeo ya kupikwa yaliyolenga kumuepusha Rais Mwai Kibaki na aibu ya kuwa Rais wa muhula mmoja yaliposababisha machafuko yaliyoua watu 1,300.
Uchaguzi uliofuata mwaka 2013, pengine kutokana na funzo lililotokana na 2007, ulifanyika kwa amani safari hii Raila Odinga akikubali matokeo japo kwa shingo upande baada ya Mahakama ya Juu kuthibitisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta.
Huo ni mwaka ambao, kile kinachoelezwa kuwa moja ya Katiba bora barani Afrika ilitumika mara ya kwanza katika uchaguzi huo.
Hata hivyo, Katiba hii, ambayo ilitegemewa ingeiumba upya Kenya kisiasa, kijamii, kiuchumi imekuwa kama pambo kutokana na wanasiasa wa upinzani na Serikali kwa jeuri na viburi vyao kukataa kuiheshimu.
Kilichojiri kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8, ambao matokeo ya urais yalifutwa na ule wa marudio wa Oktoba 26 uliosusiwa na NASA na yanayotokea sasa, kunadhihirisha safari ndefu Afrika inapitia kuelekea ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia.
Tabia ya kudharau Katiba kunakosababishwa na jeuri fulani ya madaraka au ngome kubwa za kisiasa kunatengeneza utamaduni mbaya katika jamii na vizazi vijavyo, vinavyoona kuwa ukiukaji huo ni kitu kinachokubalika na hivyo migogoro nayo inakuwa sehemu ya utamaduni.
Muungano wa NASA ukifahamu Katiba hairuhusu vitendo kama hivyo na vinavyofanana navyo, katika mwendelezo wake wa kutoutambua urais wa Uhuru Kenyatta waliamua ‘kumuapisha’ kuwa Rais wa watu kiongozi wake Raila Odinga kwenye bustani ya Uhuru mjini Nairobi Jumanne wiki iliyopita.
Licha ya kuwa upinzani unalitazama tukio kuwa halali na hivyo hakuna kesi ya Uhaini dhidi ya Odinga wala wale walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha hafla hiyo, kwa kile ilichodai aliapishwa kuwa Rais wa wananchi si wa Jamhuri, kitendo hicho kwa vyovyote hakikubaliki wala hakiakisi ukomavu wa kisiasa.
Mapema kabisa Odinga alifahamu kitendo hicho si kizuri kwa Taifa, ambalo ametumia sehemu kubwa ya uhai wake kulipigania kidemokrasia, ndiyo maana mara mbili alikwepa kuapishwa.
Mara ya mwisho Desemba mwaka jana, alisema kwa kuangalia heshima na hadhi aliyonayo katika Jumuiya ya Kimataifa, haitapendeza akijiapisha.
Lakini msimamo wake huo mzuri uliyeyuka baada ya kunywea kwa shinikizo la wafuasi wake wasioambilika ama kusikia la mwanzini wala la mnadi swala na ambao wamejiapiza kufa kwa ajili yake.
Kwa kuapishwa Jumanne wiki iliyopita, Raila aliweza kukonga nyoyo za wafuasi wake huku vinara wenzake akina Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula wakishambuliwa mitandaoni kwa usaliti katika ngome zao wenyewe kutokana na kukwepa hafla hiyo.
Hata hivyo, Odinga kama mwanasiasa mbobezi na msomi alitakiwa kuweka mbele maslahi ya Taifa na kuonesha msimamo na ukomavu wa kiuongozi na kisiasa kutokuwa tayari kufuata matakwa ya watu wanaoongozwa zaidi na hisia, ghadhabu na chuki za kikabila.
Wafuasi hawa wengi wao hawana muda wa kuitafakari kesho, hawajui lolote, au kwa wale wanaojua hawajali juu ya ubaya na gharama za kuinajisi Katiba au vitendo vyovyote vinavyobomoa misingi ya utaifa.
Sasa wakati Serikali ya Jubilee ikiishutumu NASA kwa kuvunja Katiba na kwamba ijiandae kulipia kosa hilo, ambalo ilishaonya kuwa adhabu yake ya juu ni kifo, nayo imeingia katika mtego huo huo wa upinzani wa kutoheshimu Katiba na Sheria kwa namna nyingine.
Kuelekea hafla ya kumuapisha Odinga, Serikali ya Jubilee iligawanyika baina ya wahafidhina wenye msimamo mkali na wanasiasa wa msimamo wa wastani.
Wahafidhina walikuwa wakisisitiza ikibidi nguvu itumike ili kuzuia kufanyika kwa hafla ya kumuapisha Odinga Uhuru Park, kitu ambacho hata hivyo ni wazi kingesababisha umwagaji mkubwa wa damu.
Tangu Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8 mwaka jana, wahafidhina wakiongozwa na Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’I na Makamu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe walionesha misimamo mikali.
Matokeo yake, kati ya hiyo Agosti na Novemba mwaka jana kamata kamata na makabiliano yanayohusiana na chaguzi ikiwamo maandamano ilisababisha vifo vya watu zaidi ya 50 wakiwamo watoto huku wengine wakibakwa.
Serikali ilishutumiwa na Jumuiya ya Kimataifa na makundi ya haki za binadamu kwa matumizi makubwa mno ya nguvu ya polisi katika kushughulikia wafuasi wa upinzani.
Safari hii busara ilitumika, baada ya askari polisi kuamriwa kuondoka Uhuru Park katika dakika za mwisho na hivyo kunusuru umwagaji mkubwa zaidi wa damu kwa kuzingatia majibizano yaliyoambatana kuapizana kutoka pande hizo mbili kulionesha dalili hizo.
Pongezi kwa Serikali kwa kutumia busara hiyo, zikakosa maana baada ya kuhamisha hasira zake kwa vidagaa; si tu wanasiasa na wanaharakati wadogo wadogo bali pia vyombo vya habari, ambavyo havihusiki na tukio hilo zaidi ya jukumu lake la kuihabarisha jamii kinachojiri ndani na nje ya mipaka yao.
Hatua ya kwanza ya Serikali ilikuwa kuvifungia vituo vitatu vikubwa vya televisheni mapema asubuhi ya Jumanne ya tukio hata kabla ya Odinga hajala kiapo, kuwasaka wapinzani huku ikimgwaya Odinga pamoja na kujaribu kuwakamata waandishi kadhaa.
Hata hivyo, waandishi hao walikingiwa kifua na Mahakama iliyotoa amri kwa polisi iache kuwakamata.
Jaji Luka Kimaru alitoa agizo hilo hadi pale kesi dhidi ya Waandishi Linus Kaikai, Ken Mijungu na Larry Madowo wote wa Kampuni ya Nation Media itakaposikilizwa.
Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano ilivifungia vituo hivyo vya televisheni vya NTV, KTN News na Citizen kwa madai ya kukiuka onyo la Rais la kutorusha moja kwa moja hafla hiyo ya kumuapisha Odinga.
Wakati ikifungia vituo hivyo binafsi vinavyotazamwa zaidi nchini Kenya, imeviacha vile vilivyoegemea mrengo wa Serikali KBC na K24 inayosemekana kuwa na uhusiano na familia ya Rais Kenyatta.
Mbaya zaidi katika tukio lingine wiki iliyopita, Rais Kenyatta ingawa wasaidizi na wapambe wake wanadai ukimya wake kuhusu kuapishwa kwa Odinga unaashiria hababaishwi na tukio hilo, alionesha chuki za wazi kwa wanahabari katika tukio moja la kitaifa.
Mara baada ya kutoa hotuba, akionesha kujawa dhahabu, alisema kwa Kiswahili: Sasa si mzime hivyo vitu vyenu (Kamera za TV) na muondoke? Kazi yenu imeisha.
Kitendo hicho kimelaaniwa si tu nchini humo bali pia na Jumuiya ya Kimataifa, ambazo si tu zimekosoa hatua ya NASA kumuapisha Odinga, bali pia Serikali kwa kuwaandama wanahabari na kuzima matangazo ya vituo vya televisheni.
Umoja wa Ulaya umesisitiza umuhimu wa viongozi wote kuheshimu Katiba ya Kenya na sheria zake kwa jumla huku Marekani ikikosoa vitendo vyovyote vinavyokiuka sheria za nchi.
Kwa kuheshimu sheria ni sawa na kuheshimu Uhuru wa kutangamana, vyombo vya habari na kujieleza.
Kwa mantiki hii hatua ya Serikali ya kuvibana vituo vya televisheni kurusha matangazo, ambapo iwapo leo vitaendelea kuwa gizani itakuwa siku ya tisa ni kinyume na maadili.
Ifahamike kuwa Mahakama Kuu tayari ilishaamuru tangu Jumatano iliyopita Serikali ivifungulie vituo hivyo ili viweze kurusha matangazo bila mafanikio.
Mbali ya kugoma kuidharau mahakama katika suala la vyombo vya habari kwa kutoheshimu maagizo yake kama inavyotakiwa kikatiba, Serikali pia imegomea uamuzi wa chombo hicho kilichotaka kuachiwa kwa dhamana kwa mwanaharakati wa upinzani aliyejitangaza kuwa jenerali wa Vuguvugu la upinzani la NASA, NRM, Miguna Miguna.
Tayari NASA imeonya kuwa itahamasisha wafuasi wake kwa namna ile ile kama ilivyotokea Uhuru Park, kujazana katika kituo kikuu cha polisi kushinikiza Miguna aachiwe ama polisi iwakamate wote kwa wingi wao kwa vile nao walishiriki tukio la kiapo.
Dharau hizo kwa mahakama na Katiba zitakuja kuwaandama wanasiasa mara watakapoondoka madarakani na hawatakumbukwa kwa mazuri kama wajenzi wa demokrasia.
Serikali inayotishia, kandamiza na kufungia vyombo vya habari achilia mbali upinzani ambao imewanyan’ganya viongozi wake walinzi ina na upungufu mkubwa katika demokrasia.
Wanasiasa hawa hawana cha kulifunza Taifa la kesho zaidi ya kuliambukiza utamaduni mbovu kisa tu ‘mbona Raila alifanya hivi na vile’ bila mtu wa kumnyooshea kidole na kadhalika Serikali.