29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

Vita ya Yanga, Azam, Simba

simba,azam,yangaNA ZAINAB IDDY, DAR ES SALAAM

TIMU za Yanga, Azam na Simba, leo zinaingia kibaruani kwa mara nyingine katika viwanja tofauti katika raundi ya 12 ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga, wao watakuwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuwakabili Stand United ya Shinyanga.

Yanga, wanaoongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 27 baada ya kucheza mechi 11, wanashuka dimbani wakitokea mkoani Tanga, ambako wamecheza mechi mbili baina ya Mgambo Shooting na Africans Sports, ambao wameambulia pointi nne pekee kati ya sita.

Kikosi hicho kinachonolewa na kocha Hans Pluijm, kinaingia kikiwa na matumaini makubwa ya kupata ushindi katika mchezo huo mbele ya Stand, wanaoonekana kuwa na kiu ya pointi tatu baada ya kupoteza mechi iliyopita mbele ya Mwadui FC walipofungwa mabao 2-0.

Simba, wenye pointi 22, wakiwa nafasi ya nne, watakuwa ugenini katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, kuwakabili Toto Africans, iliyopo chini ya kocha msaidizi, John Tegete.

Katika mchezo uliopita, Simba walilazimishwa sare ya mabao 2-2 na Azam FC katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, hali inakayowalazimu kupigana kufa na kupona ili kupata pointi tatu mbele ya Toto, waliotoka kuwanyuka Majimaji kwa mabao 4-1.

Azam FC, waliopo nafasi ya pili wakiwa na pointi 26, watakuwa ugenini mjini Songea mkoani Ruvuma katika Uwanja wa Majimaji kuwakabili wenyeji wao, Majimaji, huku Kagera Sugar wakiwakaribisha Africans Sports, wakati Tanzania Prisons watakuwa nyumbani katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, kumenyana na Mtibwa Sugar ya Morogoro na Mwadui FC kuwakaribisha Ndanda FC.

Mechi nyingine zitapigwa kesho baina ya JKT Ruvu dhidi ya Coastal Union katika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, huku Mbeya City wakicheza nyumbani katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya kuivaa Mgambo Shooting kutoka mkoani Tanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles