27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Vita mpya umeya Dar

kubenea-620x307Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

VITA ya uchaguzi wa mameya wa Manispaa za Kinondoni na Ubungo  Dar es Salaam, imeanza kupamba moto huku vyama vya CCM na Chadema vikishutumiana kwa hofu ya kuhujumiana.

Hatua ya kufanyika uchaguzi huo, imekuja baada ya kuvunjwa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Kinondoni Septemba 16, mwaka huu.

Baraza hilo lilivunjwa kutokana na Wilaya ya Kinondoni kugawanywa na kuwa wilaya mbili za Kinondoni na Ubungo.

Kuvunjwa kwa baraza hilo kumezifanya manispaa hizo kuanzia jana kuanza mchakato wa uchaguzi wa meya.

Inaelezwa  mchakato  utachukua wiki mbili hadi kukamilika na kupatikana  mameya wapya wa manispaa za Kinondoni na Ubungo.

Akizungumza na MTANZANIA, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba alisema chama hicho kimejipanga kuhakikisha kinashinda nafasi hiyo hasa kwa Manispaa ya Kinondoni.

Alisema kwa sasa kipo kwenye maandalizi ya kuhakikisha kinapata mgombea mzuri na mwenye kukubalika ndani ya jamii na hata mbele ya madiwani wa vyama vyote.

“Uchaguzi ni hesabu na si lelemama, nasi kama CCM ni lazima kwanza tuishukuru Serikali ya awamu ya nne na tano kwa kukubali ombi letu la kuwa na manispaa tano katika Jiji la Dar es Salaam.

“Kwa muda mrefu tangu walipochaguliwa Chadema kuongoza wameharibu na kila unapofika uchaguzi ni lazima waanze kuweweseka.

“Tumejipanga na kwa hesabu zetu tutashinda tu, unajua hapa hakuna Ukawa maana mwanzo Chadema waliitumia CUF kufanikisha mambo yao lakini baada ya muda mambo yameonekana,” alisema Simba.

Alidai  CCM inajua hila zinazofanywa na Chadema ikiwamo kuwalazimisha baadhi ya madiwani wao wa viti maalumu warudi manispaa ya Kinondoni ingawa uteuzi wao ni wa majimbo ya Ubungo na Kibamba.

Alipoulizwa idadi ya madiwani wao ambayo itaifanya CCM   kuibuka kidedea katika kinyang’anyiro hicho, hakuwa tayari kusema chochote ingawa alisisitiza  kuwa uchaguzi ni hesabu.

Kauli ya Chadema

MTANZANIA ilimtafuta Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema)  ambaye alisema hakuna hesabu zozote zinazoipa CCM ushindi kwa manispaa zote.

Kubenea ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Madiwani, alisema   katika baraza la Kinondoni lililovunjwa, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vilikua na viti vya udiwani 38.

Alisema Chadema kilikuwa na madiwani 29, wakati CUF (9), huku CCM ikiwa na viti 15.

“Jambo la msingi hapa ni kwamba halmashauri mpya ya Ubungo nayo itaongozwa na Ukawa, ndiyo wenye viti vingi vya udiwani.

“Ingawa katika mgawanyo uliotokea inasadikiwa takriban madiwani 18 wa Ukawa watakuwa kwenye halmashauri mpya ya Ubungo, huku CCM ikihama na madiwani saba tu.

“Wanaodhaniwa kubakia Kinondoni Ukawa ni 20 na CCM wanane, haihitaji muujiza kujua Ukawa inaenda kuongoza halmashauri zote hizi mbili,”alisema Kubenea.

Hata hivyo, alituhumu kile alichodai mpango wa CCM kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutaka kufanya mgawanyo upya wa madiwani wa viti maalumu jambo ambalo si sahihi kwa mujibu wa sheria.

“Ninashangaa CCM wanapodai watashinda uchaguzi sijui ni kwa hesabu zipi?  Iwe mchana au usiku hawawezi ingawa zipo taarifa za ndani kwamba wanataka kufanya mgawanyo wa madiwani wa viti maalumu kama njia ya kuongeza namba ya madiwani wa kuwapigia kura  waweze kushinda.

“Tena si hilo tu upo mpango wa ndani eti wanataka hata Mbunge wa Viti  Maalumu (CUF), Salma Mwassa wamtoe Kinondoni kama njia ya kuongeza kura CCM.

“Nasema hilo halitawasaidia hata kidogo. Ukawa tupo imara na tumejipanga kuwatumikia wananchi kwa kuwaletea maendeleo ya kweli kwa vitendo,”alisema Kubenea.

Katibu wa  Chadema  Kanda ya Pwani, Kasmir Mabina alisema wamejiandaa kushinda nafasi za umeya wa Halmashauri ya Kinondoni na Ubungo.

Alisema uchaguzi ni namba na namba hizo zinaonyesha idadi ya madiwani wa Chadema nawa Chama cha Wananchi (CUF) kupitia Ukawa ni wengi kuliko wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa uchaguzi huo wa mameya kukumbwa na mvutano kati ya Ukawa na CCM kama ilivyotokea katika uchaguzi wa awali, Katibu huyo alisema:

“Tumejiandaa kushinda, siku zote uchaguzi ni namba, naamini safari hii wenzetu CCM watakuwa waungwana  kuruhusu namba zitoe majibu sahihi”.

Wilaya ya Kinondoni itakuwa   halmashauri moja na majimbo mawili ya uchaguzi  ya  Kinondoni na Kawe.

Wilaya ya Ubungo nayo itakuwa na halmashauri moja yenye majimbo mawili ya uchaguzi ambayo ni Ubungo na Kibamba.

Ikiwa uchaguzi huo utafanyika na Ukawa  kushinda watakuwa wanaongoza wilaya za Ilala, Kinondoni, Ubungo   na Jiji la Dar es Salaam, huku CCM ikibaki kuongoza wilaya za Temeke na Kigamboni ambako chama hicho tawala kinapewa nafasi kubwa ya kushinda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles