28.6 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

VITA DAWA ZA KULEVYA: KAMISHNA SIANGA ABADILISHA GIA YA MAKONDA

Na Elizabeth Hombo – Dar es Salaam

WAKATI baadhi ya Watanzania wakitarajia kuwekwa hadharani kwa majina 97 yaliyokabidhiwa juzi kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga, kiongozi huyo amesema jambo hilo halitafanyika.

Kamishna Sianga amesema badala yake, watayafanyia uchunguzi majina hayo na watakaobainika kuhusika watakamatwa huku watakaogundulika kutoa taarifa za kusingizia wengine nao pia watachukuliwa hatua.

Mfumo huo wa Kamishna Sianga, ni tofauti na ule uliokuwa ukitumiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alyekuwa akitaja hadharani majina ya watu wanaotuhumiwa kufanya biashara ya dawa za kulevya ama kuzitumia.

Akihojiwa na redio ya Idhaa ya Sauti ya Ujerumani (DW), Kamishana Sianga alisema: “Baada ya kupata orodha hii ya majina (97 aliyokabidhiwa na Makonda), sisi tunayo majina mengine ambayo tutaichanganya pamoja na hiyo.

“Tutaipitia orodha hiyo na kuthibitisha ushiriki wa kila mtuhumiwa na pale tutakapokuwa tumejiridhisha kwamba anashughulika na biashara hiyo, tutamkamata na kumpeleka mahakamani.

“Hatutaichukua hatua ya kumkamata moja kwa moja kwa sababu kuna watu ambao wanatoa majina kwa nia ya kuwakomoa watu, unaweza ukachukua na kurukia jina kumbe huyo mtu ni ‘innocent’ (hana hatia) ukamwadhibu, ukamweka katika hatari ya kupata adhabu wakati huyu mtu hana hatia amekomolewa na rafiki yake kwa kisasi au madeni waliyonayo anamtoa kwenye orodha, hivyo lazima tuthibitishe kama kweli mtu anahusika au hahusiki na baada ya kuthibitisha tutachukua hatua,” alisema Kamishna Sianga.

Alipoulizwa sababu ya kutoendelea na utaratibu wa kutaja majina hadharani kabla ya kuchunguza watuhumiwa, Kamishna Sianga alisema: “Unajua hiki chombo kilikuwa hakipo, mamlaka hii ilikuwa bado kwa ajili kushughulikia mambo haya, hivyo lazima sasa tuende kwa kufuata sheria.” 

Kuhusu wale wanaotaja watu kwa kuwasingizia, Kamishna Sianga alisema: “Kama mtu ametajwa na hahusiki yule aliyemtaja kama amembambikia huyo tutakwenda naye kwa sababu hatuonei mtu.”

Akieleza mikakati yake kwenye vita hiyo, alisema mikakati yao ni pamoja na kuhakikisha wasafirishaji na wafanyabiashara wa dawa za kulevya wanakamatwa na kuadhibiwa na wale ambao wameathirika na dawa za hizo wanapatiwa matibabu.

Alisema watumiaji hao watakuwa pia ni sehemu ya kueleza watu wanaowauzia dawa hizo.

Akizungumzia sababu inayowafanya sasa waamini kuwa wataishinda vita hiyo, alisema: “Kitu kipya ni ufuatiliaji na ‘political will’ (utayari wa kisiasa), kwanza kuwepo kwa ‘political will’ kunasaidia katika mapambano haya ya dawa za kulevya, kuundwa kwa hii mamlaka ambayo sasa ina ‘power’ (nguvu) za ku-investigate to arrest (kuchunguza, kukamata) chombo kilichokuwepo kilikuwa hakina mamlaka, lakini sasa kuna mamlaka ya kufanya vyote vitatu, jambo hili pekee ni hatua kubwa.”

Juma lililopita, baada ya kuibuka hoja ya dawa za kulevya na jinsi Makonda anavyolishughulikia jambo hilo, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema), akizungumza bungeni alikumbusha umuhimu wa kuunda mamlaka hiyo kama sheria mpya ya kupambana na dawa za kulevya inavyoagiza.

Bulaya ni sehemu ya chimbuko la kuundwa kwa mamlaka hiyo kutokana na hoja binafsi aliyoiwasilisha bungeni mwaka 2013.

Katika hoja yake aliyoitoa mapema wiki hii, alisema kimsingi hapingani na vita dhidi ya dawa za kulevya, lakini akashauri wale wote wanaotaka kupambana wasimwogope rais, bali ashauriwe amteue kamishna wa chombo hicho kama sheria inavyoagiza.

Bulaya ambaye pia ni Waziri Kivuli katika Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia dawa za kulevya, alisema yeye, Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenister Muhagama, ndio waliokuwa mstari wa mbele kushinikiza kutungwa kwa sheria hiyo.

 “Sisi ndio tulianza huu mchezo, tutakapohakikisha hiki chombo kinapata kamishna wa kumsaidia rais tutakamata wale wanaoingiza dawa za kulevya, wale mapapa, hawa wanaokamatwa sasa hivi ni waathirika, wanatakiwa kupelekwa Muhimbili, Mwananyamala wakapate tiba,” alisema.

Kabla ya kutungwa kwa sheria hiyo, mapambano hayo yalikuwa yakiongozwa na chombo maalumu kilichokuwa chini ya Jeshi la Polisi kikiongozwa na Kamishna Godfrey Nzowa, ambaye kwa sasa amestaafu.

Juni 2015, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya na Usafirishaji Haramu, alisema ametia saini sheria mpya ya dawa za kulevya ya mwaka 2015, ambayo ilitarajiwa kwenda sambamba na kuundwa kwa mamlaka itakayoongoza vita hiyo.

“Sheria hii mpya nina hakika kabisa itasaidia kutokomeza mianya ya uingizwaji, utumiaji na usafirishaji wa dawa za kulevya nchini,” alisema Kikwete.

Alisema sheria hiyo itazaa taasisi hiyo itakayokuwa na uwezo wa kuwakamata na kuwashtaki wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo, huku ikishirikiana na DPP na mhusika akikamatwa atafungwa kifungo cha maisha jela.

Kikwete alisema anaondoka madarakani huku sheria hiyo ikiwa tayari imeanza kufanya kazi na atahakikisha inapitishwa mapema ili rais ajaye akute taasisi hiyo imeanza kazi.

“Sheria hii ambayo tayari nimeshaweka saini ina majibu yote ya Watanzania waliokuwa wakijiuliza kwa miaka yote kuhusu mianya inayotumika kuingiza dawa hizi haramu nchini. Pia, ni sheria itakayotupatia ufumbuzi wa matatizo ya sasa na miaka ijayo itazaa taasisi itakayoratibu, kupambana, kukamata, kupeleleza na hata kupekua ikibidi ili kutokomoza janga hili,” alisema Kikwete.

Alisema ili kupambana na hali hiyo, Serikali imeimarisha vyombo vya dola katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya sambamba na tume ya kudhibiti na kupambana na dawa hizo, polisi ambao wamepewa mamlaka ya kukamata wafanyabiashara na watumiaji wa dawa hizo.

Hata hivyo, azma yake hiyo haikuzaa matunda kwani sheria hiyo sasa ndiyo itaanza kufanya kazi baada ya kuteuliwa kwa viongozi wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles