23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Visual| Watoto wanavyokosa haki ya kunyonyeshwa

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Kama inavyofahamika kwamba Unyonyeshaji una faida kubwa kwa mama na mtoto ikiwemo uimarishaji wa afya ya akili katika maendeleo ya mtoto, kuwalinda watoto dhidi ya magonjwa, kupunguza hatari za utipwatipwa, kupunguza gharama za huduma kwa mtoto na pia kuwalinda kina mama wanaonyonyesha dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na ya matiti.

Kwani kwa maeneo ya mjini tunaelezwa kuwa wanawake wengi wamekuwa wakipata usaidi wa unyonyeshaji kwa kuwakupa maziwa ya kopo yanayouzwa kwenye maduka maalum.

Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la afya Ulimwenguni (WHO) na la kuhudumia watoto (UNICEF) na wadau wao, wametoa wito kwa serikali, wahudumu wa afya na tasnia nzima inayohusika na vyakula vya watoto kutekeleza kikamilifu na kutii mahitaji ya Kanuni za kiafya.

Wito huo unatokana na kwamba zaidi ya nusu ya wazazi na wanawake wajawazito yaani asilimia 51 waliohojiwa kwa ajili ya ripoti hiyo mpya ya WHO na UNICEF, wanasema wamekuwa wakilengwa na ushawishi wa biashara kutoka kwa makampuni ya maziwa ya viwandani, ambayo mengi yanakiuka viwango vya kimataifa vya ulishaji wa watoto wachanga.

UNICEF na WHO zinasema kuwa tasnia ya maziwa yenye thamani ya dola bilioni 55 inatumia mikakati ya kimasoko na isiyo ya kimaadili ili kushawishi maamuzi ya wazazi ya ulishaji wa watoto wachanga na mila za kinyonyaji zinazohatarisha lishe ya watoto na kukiuka ahadi za kimataifa.

Ripoti hii inaonesha kwa uwazi kwamba uuzaji wa maziwa ya kopo bado unaenea kwa njia isiyokubalika ya kupotosha na ya fujo.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Ghebreyesus, amebainisha kuwa kanuni za uuzaji wa unyonyaji zikubaliwe na kutekelezwa kwa haraka ili kulinda afya ya watoto.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa sio tu kwamba mbinu za uuzaji za tasnia hiyo ya maziwa ya watoto ni pamoja na ulengaji wa mtandaoni usiodhibitiwa na wavamizi, lakini pia mitandao ya ushauri iliyofadhiliwa; ilitoa matangazo na zawadi za bure kwa wafanyakazi wa afya na hivyo kuathiri mafunzo na mapendekezo ya wafanyakazi wa afya.

Vikwazo dhidi ya unyonyeshaji

Ripoti inasisitiza kwamba sekta hii mara nyingi hutoa taarifa za kupotosha na zisizothibitishwa kisayansi kwa wazazi na wafanyakazi wa afya na pia inakiuka kanuni ya kimataifa ya uuzaji wa bidhaa zinazotumika badala ya maziwa ya mama.

“Kanuni ambazo ni makubaliano ya kihistoria ya afya ya umma kulinda akina mama dhidi ya matangazo au uuzaji wa bidhaa kutoka kwa tasnia ya chakula cha watoto,” inabainisha ripoti hiyo na kuongeza kuwa:

“Baada ya kuwafanyia uchunguzi wazazi 8,500 na wanawake wajawazito na wahudumu wa afya 300 duniani kote, ripoti iligundua kuwa ushawishi wa uuzaji wa maziwa ya viwandani ulifikia asilimia 84 ya wanawake wote waliohojiwa nchini Uingereza; asilimia 92 nchini Vietnam na asilimia 97 nchini China na kuongeza uwezekano wao wa kuchagua ulishaji watoto wao kwa maziwa ya kopo au ya viwandani.

“Ujumbe wa uwongo na wa kupotosha kuhusu maziwa ya unga ni kikwazo kikubwa kwa unyonyeshaji. Unyonyeshaji ambao tunajua ni bora kwa watoto wachanga na akina mama,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell.

Hatua hizo zinakinzana na tathimini ya UNICEF ya mwaka Mwaka 2020 iliyobainisha kuwa maisha ya watoto 820,000 yanaweza kuokolewa kila mwaka kutokana na ongezeko la kiwango cha unyonyeshaji na hivyo kusaidia kuzalisha pato la zaidi ya dola bilioni 300.

Tathimihi hiyo iliweka wazi kuwa, mafanikio hayo yanaweza kupatikana iwapo tu aina mbalimbali za wataalam wa afya wataweza kutoa msaada wa kitaalam unaohitajika kama vile washauri wa unyonyeshaji katika mazingira ya kliniki au kwa kuwatembelea kina mama majumbani au kuwapo kwa program za jamii zitakazowasaidia watu moja kwa moja au kwa nia ya mtandao.

Pia licha ya mlipuko wa janga la Uviko-19 UNICEF imekuwa ikihimiza juu ya jamii kuwa na wataalmu mbalimbali wa unyonyeshaji kwa ajili ya kusaidia kutoa elimu kwa akina mama lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa janga hilo halikatizi haki ya mtoto ya kunyonyeshwa.

Kazini nako bado mwiba

Aidha, UNICEF katika ripoti yake ya mwaka 2019 ilibainisha kuwa asilimia 60 ya Watoto wachanga hawanyonyeshwi sababu ya sera za kazi.

Shirika hilo linabainisha kuwa sera zilizo rafiki kwa masuala ya familia ni muhimu katika kuhakikisha idadi ya watoto wachanga wanaonyonyeshwa katika miezi sita ya mwanzo ya maisha yao.

Maeneo mengi ya kazi yanaelezwa kutokuwa na sera za kuunga mkono unyonyeshaji kama vile likizo yenye malipo kwa wazazi na mapumziko ya kunyonyesha ambayo hayapo kwa kina mama wengi kote duniani.

“Sehemu nyingi za kazi duniani zinawanyima kina mama msaada wanaohitaji kuweza kunyonyesha, tunahitaji kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika likizo za malipo na msaada utakaowawezesha kina mama kunyonyesha katika maeneo yote ya kazi ili kuongeza kiwango cha unyonyeshaji wa maziwa ya mama kote duniani.

Mwaka 2018 watoto 4 tu kati ya 10 ndio walionyonyeshwa maziwa ya mama katika miezi sita ya mwanzo ya maisha yao sawa na asilimia 41 ya watoto wote.

Takwimu hizo za UNICEF zilitaja unafuu kwa nchi zinazoendelea kwani ndio zinaongoza kwa unyonyeshaji huo ikiwamo Rwanda iliyoshika nafasi ya kwanza kwa asilimia 86.9, ikifuatiwa na Burundi asilimia 82.3, Sri Lanka asilimia 82, Visiwa vya Solomon asilimia 76.2 na Vanuatu asilimia 72.6.

Utafiti pia ulionyesha kuwa watoto katika maeneo ya vijijini wana kiwango kikubwa cha kunyonyeshwa kuliko mijini.

Aidha nchi za kipato cha juu na cha kati viwango wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto ndio vya chini zaidi vikiwa ni asilimia 23.9 hivi sasa vikiwa vimepungua kutoka asilimia 28.7 mwaka 2012. Hivyo kina mama wanaofanya kazi hawapati msaada wa kutosha.

UNICEF inasema ni asilimia 40 tu ya wanawake wenye watoto wachanga kote duniani ndio wanaopata hata ile likizo ya msingi ya uzazi wakiwa kazini.

Na pengo ni kubwa zaidi miongoni mwa nchi za Afrika ambazo wanawake wanaopata likizo hiyo wakiwa kazini ili waendelee kunyonyesha watoto wao ni asilimia 15 tu, huku kukiwa na nchi chache tu zinazotoa likizo ya malipo kwa wazazi.

Sera ya shirika la kazi duniani ILO kuhusu likizo ya uzazi inasema angalau kuwe na likizo ya wiki 14 yenye malipo ya likizo ya uzazi huku nchi zikihimizwa kutoa wiki 18 pamoja na msaada kazini.

Lakini hadi sasa ni asilimia 12 tu ya nchi zote duniani ndizo zinazotoa likizo hiyo yenye malipo.
Sera mpya ya UNICEF iliyotangazwa mwaka huu kuhusu likizo ya uzazi inapendekeza miezi sita ya likizo yenye malipo kwa wazazi wote kwa jumla na kati ya miezi hiyo wiki 18 zitengwe kwa ajili ya kina mama.

Na inapendekeza kwa serikali na kampuni za biashara kutoa angalau miezi 9 ya jumla likizo kwa wazazi. Idadi ndogo ya watoto wananyonyeshwa pinditu wazaliwapo.

Katika hatua nyingine UNICEF kwa mwaka 2018 chini ya nusu ya watoto wote duniani au asilimia 43 ndio walioweza kunyonyeshwa katika saa ya kwanza ya uhai wao baada ya kuzaliwa hatua ambayo ni muhimu katika kumjengea mtoto kinga ya mwili na kumsaidia mama kujiweka tayari kuendelea kunyonyesha mwanaye kwa muda mrefu.

Maziwa ya mama kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO ni zaidi ya chakula kwa mtoto, pia ni dawa ya kumkinga na magonjwa mbalimbali na kifo.

Hali ilivyo nchini Tanzania

Mwongozo wa Kuadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji Tanzania kwa mwaka 2021 unaonyesha kuwapo kwa mafanikio makuba yaliyofikiwa nchini.

Kwani asilimia 98 ya wanawake wanachagua kuwanyonyesha watoto wao. Pia asilimia 53.5 ya watoto wanaanzishiwa kunyonya maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa.

Takwimu pia zinaonesha kuwa asilimia 58 ya watoto wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee ndani ya miezi sita ya Mwanzo.

Mwongozo huo unaendelea kubainisha kuwa watoto wanaoendelea kunyonyeshwa hadi kufikia umri wa mwaka mmoja ni asilimia 92.2 huku wale wanaoendelea kunyonyeshwa hadi kufikia miaka miwili ni asilimia 43.

Aidha, kiwango cha watoto wanaoanzishiwa vyakula vya nyongeza katika umri sahihi ni asilimia 87.
Pia asilimia 35 tu ya watoto ndio hupatiwa mlo kamili wenye mchanganyiko sahihi wa makundi ya vyakula, asilimia 58 ya watoto wenye umri wa miezi 6 – 23 wanapewa idadi sahihi ya milo kwa siku kulingana na umri wao.

Kwa ujumla, watoto wenye umri wa miezi 6 hadi 23 wanaopewa milo yenye ubora wa kukidhi mahitaji yao kilishe ni asilimia 30 tu, hii ni sawa na kusema kwamba asilimia 70 hawapati lishe kamili.
Wiki ya unyonyeshaji duniani kuadhimishwa kila mwaka kuanzia Agosti 1-7.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles