26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Virutubisho vitano muhimu kwa samaki

 Grace Shitundu 

UFUGAJI wa samaki ni biashara ambayo imeendelea kukua kwa kasi katika miaka ya karibuni. 

Wafugaji wengi wa samaki kwa sasa wanafuga kibiashara hivyo kuingiza kipato na kujiinua kiuchumi. 

Hata hivyo katika shughuli hiyo ya ufugaji wa samaki kuna changamoto ambazo huwarudisha nyuma wafugaji. 

Moja ya changamoto ambazo wafugaji wengi hukumbana nazo ni upatikanaji wa chakula cha samaki. 

Makala haya kwa msaada wa mitandao mbalimbali ya ufugaji inaangazia namna ambavyo mfugaji anaweza kutengeneza chakula cha samaki nyumbani ili kupunguza gharama katika ufugaji. 

Mfugaji anaweza kutengeneza chakula mwenyewe kwa kutumia malighafi zinazopatikana nyumbani. 

Anachotakiwa kufanya ni kuhakikisha anatengeneza chakula ambacho kina virutubisho vyote muhimu kwa uwiano unaotakiwa ambavyo vitasaidia samaki katika ukuaji wake. 

Mfugaji anashauriwa kuhakikisha chakula hicho kinakuwa na virutubisho kama protini (kiini lishe), wanga, mafuta (fat /lipid), vitamini na madini. 

Viritubisho hivyo vitano ni muhimu kwa samaki kwa sababu kila kimoja kina kazi yake ndani ya mwili wa samaki anayefugwa. 

Chakula cha samaki hutengenezwa kulingana na aina ya samaki husika, mfano kuna samaki aina mbalimbali kama Sato, Perege, Sehewa, Mwatiko, Kambale mchanganyiko wake huwa tofauti tofauti. 

Wafugaji wengi hufuga samaki aina ya Tilapia kama Sato na Perege hivyo katika makala haya chakula kinachoelekezwa kutengenezwa ni maalumu kwa samaki hao. 

Mahitaji ambayo mfugaji atahitaji kwa ajili ya kutengenezea chakula hicho ni pamoja na unga wa dagaa, soya lishe, pumba za mpunga au mahindi, unga wa mhogo, au unga wa ngano, machicha ya nazi au mashudu ya alizeti na Vitamin mineral mix, premix na D.I. Grow. 

Unga wa dagaa 

Dagaa wanatakiwa wawe wamesagwa na kuwa katika hali ya unga unga, unga wa dagaa ni protini ya mnyama na kazi kubwa ya protini hii ni kufanya mwili kukua vizuri. 

Protini hii huitajika kwa 

 wingi zaidi hasa kipindi ambacho samaki huwa mdogo na katika rika la samaki mzazi. 

Soya lishe 

Hii ni protini ya mmea ambayo hufanya kazi ya kuimarisha mwili na kukua kwa samaki vizuri. 

Protini hii hupatikana katika mimea jamii ya mikunde ambayo hutakiwa kuchemshwa kidogo kisha kuzianika mpaka zikauke halafu kuzisaga ili ziwe kwenye hali ya unga unga. 

Hutumika kwa wingi katika chakula cha samaki anapokuwa mdogo na kipindi anachofikia kuwa mzazi 

Pumba za mpunga, mahindi 

Hiki ni chakula jamii ya wanga ‘carbohydrate’ ambacho hufanya kazi ya kuongeza nguvu ndani ya mwili wa samaki. 

Pumba lazima ziwe zimesagwa vizuri na kuwa katika hali ya unga unga ili kumpa nafuu samaki katika ulaji wake. 

Huchanganywa na vyakula vingine zaidi katika kipindi ambacho samaki yupo katika rika la kati. 

Wataalam wanapendekeza kuanza kutumia pumba za mpunga kwani ni nzuri zaidi ila kama hazipatikani mfugaji anaweza pia kutumia pumba za mahindi. 

Unga wa mhogo, ngano 

Hii nayo ni aina mojawapo ya chakula aina ya wanga ambayo husaidia kumpa samaki nguvu ndani ya mwili wake. 

Kazi nyingine husaidia kuviunganisha virutubisho vyote kuwa kwenye sehemu moja hivyo humfanya samaki kula virutubisho vyote kwa wakati moja. 

Wataalamu wanapendekeza kuanza kutumia unga wa mhogo ila kama haupatikani basi unaweza kutumia unga wa ngano. 

Machicha ya nazi, mashudu ya alizeti 

Hii ni aina mojawapo ya virutubisho aina ya mafuta ambavyo hufanya kazi ya kunenepesha mwili wa samaki vizuri. 

Vitamin mineral mix, premix na D.I. Grow. 

Hizi ni aina za vitamini na madini ambayo hufanya kazi ya kuimarisha mifupa na kulinda mwili wa samaki dhidi ya magonjwa na mashambulio mengine. 

Endepo vitamin mineral haipatikani katika mazingira yako unaweza kutumia premix ya kuku wa kisasa ya kukuzia kwa ajili ya kukuzia samaki wako kwa sababu vitamini na madini yake yanafanana katika utengenezaji wa chakula. 

Ikiwa nayo pia haipatikani basi unaweza kutumia D.I Grow kwa ajili ya kutengenezea chakula chako. 

Kiwango na namna ya kuchanganya 

Unga wa dagaa ni asilimia 18.25, soya lishe asilimia 25, pumba za mpunga/mahindi asilimia 36.42, machicha ya nazi au mashudu ya alizeti asilimia 10, unga wa muhogo au ngano asilimia 6 na vitamin mineral mix, premix, D.I Grow asilimia 4.33. 

Mfano mfugaji anatengeneza chakula cha samaki cha kilo hamsini (50 kg) 

Unga wa dagaa 18.25%÷100.50,000 = 9.125 kilogram, soya lishe asilimia 25÷100.50,000 = 12.5 kilogramu, pumba za mpunga/mahindi 36.42 ÷100.50,000 = 18.21. 

Unga wa mhogo/ngano asilima 6 ÷100.50,000 = 3kilogramu na machicha ya nazi, mashudu ya alizeti asilimia10÷100.50,000 = 5kg. 

Vitamin mineral mix, premix, D.I Grow 4.33÷100.50,000=2.165kg. 

Mchanganyiko huo huchanganywa na maji nusu ya uzito wa chakula, mfano chakula unachotengeneza kilo 50 chang

 anya na maji lita 25. 

Endapo mchanganyiko bado ni mkavu sana unaweza kuongeza maji pia unaweza kuanza kuweka maji taratibu mpaka mchanganyiko utakaposhikana. 

Mchanganyiko usiwe na maji mengi sana na usiwe na maji kidogo sana yawe ya wastani. 

Chakula kisianikwe kwenye jua kwani linapoteza virutubisho vyake katika njia ya mvuke, anika kivulini ili kikaushwe na upepo. 

Baada ya kukamilisha chakula kihifadhiwe mahali salama ili kisiweze kuoza na kutoa fangasi au ukungu mweupe ambao hutokea kwenye chakula cha samaki. 

Endapo unahitaji kutengeneza chakula kidogo yaani kama unataka kutengeneza chakula cha kilo 25 basi unagawa kila chakula kwa mbili. 

Endapo unahitaji kutengeneza chakula kingi zaidi basi unazidisha mara mbili kwa kila chakula. 

Mfugaji anatakiwa kulisha samaki chakula hiki mara mbili kwa siku, asubuhi katika hali ambayo kiwango cha jua hakijawa kikubwa na jioni jua linapokuwa limepungua. 

Kiwango cha kulisha samaki wako njia rahisi ni siku mbili za mwanzo ndizo zitatoa majibu samaki wako wanahitaji kula kiasi gani. 

Kama siku ya kwanza mfugaji aliweka kiwango kadhaa wakabakisha basi kesho yake punguza kipimo mpaka uone sasa chakula unachowapa kinawatosha na hawabakishi. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles