26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Virusi vya Corona sasa vyasambaa kote China, waliofariki wafika 170

Beijing, China

Vifo vinavyosababishwa na mlipuko wa virusi vya corona vimepanda hadi kufikia 170  ikiwa ni ongezeko la vifo 38 ndani ya siku moja.

Kuthibitika kwa kesi ya ugonjwa huo katika eneo la Tibet maana yake ni kwamba sasa virusi hivyo vimeenea kila mahala nchini China.

Mamlaka za afya za China zilisema kuwa kulikuwa na kesi 7,711 zilizothibitishwa hadi kufikia jana.

Maambukizi ya virusi hivyo tayari yamesambaa katika nchi nyingine 16 duniani.

Jana Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikuwa linakutana kujadili kama wanaweza kutangaza hali ya dharura duniani.

“Katika siku chache maendeleo ya virusi, hususani katika baadhi ya nchi na vinavyoenea kutoka kwa binadamu kwenda kwa binadamu, yametutisha,”  Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus alikaririwa akisema Jumatano wiki hii.

Alizitaja Ujerumani, Vietnam na Japan, ambako kulikuwa na kesi za watu kupata virusi hivyo kutoka kwa wale ambao walikuwa nchini China.

“Ingawa idadi ya watu nje ya China bado ni ndogo mno, lakini wamebeba uwezo wa kutokea mlipuko mkubwa,” alisema Mkuu huyo wa WHO.

Watu wengi sasa wameathirika na virusi hivyo nchini China kuliko ilivyokuwa wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Sars mwanzoni mwa miaka ya  2000, ingawa idadi ya vifo imebaki ndogo  ukilinganisha na ugonjwa huo.

Sars, kama ilivyo kwa virusi vya corona nayo ilikuwa inasababisha matatizo ya kushindwa kupumua.

Watafiti wanapambana kuhakikisha wanagundua tiba ya kuondoa virusi hivyo vya corona.

Maabara moja ya California ina mipango ya kutoa chanjo ambayo wanaweza kuiingiza kwenye majaribio mwezi Juni au Julai mwaka huu.

Kuhama kwa hiyari kwa mamia ya raia wa kigeni kunaendelea nchini China hususani  kutoka katika eneo la Wuhan.

Uingereza, Australia, Korea Kusini, Singapore na New Zealand  zimetengaza kuwatenga katika eneo maalumu raia wake  kutoka China  na kuwaangalia kwa wiki mbili kuona kama wana dalili za ugonjwa huo.

MELI YAZUIWA

Wakati huo  huo meli iliyobeba abiria 6,000 imezuiwa karibu na Roma baada ya wapenzi wawili kutoka Hong Kong kupata homa kali iliyosababisha washindwe kupumua.

Wapenzi hao wamechukuliwa na kutengwa ndani ya meli hiyo wakati wakichukuliwa vipimo .

Urusi imeufunga mpaka wake wa kilomita 4,300 upande wa mbali mashariki katika mpaka wake na China.

Aidha safari za ndege kwa ajili ya kuwachukua raia wa Uingereza na Korea Kusini kutoka Wuhan zilicheleweshwa na mamlaka za China zinazotoa vibali.

Ndege mbili za Japan  tayari zimekwishatua Tokyo.

Vyombo vya habari vya Japan vimeeleza kuwa abiria watatu wamejulikana kuwa na virusi hivyo.

Aidha raia karibu 200 wa Marekani nao wameondolewa kutoka Wuhan  na watatengwa katika kituo cha jeshi cha California kwa saa 72.

Ndege mbili  nazo zinatarajiwa kubeba raia wa Ulaya wakiwamo 250 wa Ufaransa ambao watawasili katika ndege ya kwanza.

VIRUSI VYAFIKA INDIA

Virusi  vya corona vimeripotiwa kufika nchini India baada ya nchi hiyo kuripoti kesi ya kwanza ya mwanafunzi wa jimbo la Kerala lililoko kusini ambaye alikuwa akisoma Wuhan

Rais wa China, Xi Jinping ameapa kupambana na virusi hivyo alivyoviita ‘shetani’.

Jimbo la Hubei, ambako vifo karibu vyote vimetokea huko shughuli zote zimesimama.

Jimbo hilo lina watu takribani milioni 60 na Wuhan ambako ugonjwa huo ulianzia ni sehemu yake.

Wafanyakazi wa Hubei wameambiwa na waajiri wao kufanya kazi zao kutokea majumbani mwao hadi pale watakapowaarifu kuwa hali ni shwari.

UCHUMI

Virusi hivyo tayari vimetajwa kuathiri uchumi wa China, ambao ni wa pili kwa ukubwa duniani, huku idadi ya nchi ambazo zinazuia raia wake kwenda nchini humo kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi zikizidi kuongezeka.

SAFARI ZA NDEGE

Mashirika kadhaa ya kimataifa ya ndege yametangaza kusitisha safari zake  nchini China na kampuni kama Google, Ikea, Starbucks na Tesla zimefunga maduka yao au zimesitisha shughuli zake.

Kumekuwa na ripoti ya kuwako kwa upungufu wa chakula katika baadhi ya maeneo.

Chombo cha habari cha serikali kimeeleza kuwa serikali inafanya juhudi kuhakikisha bei za bidhaa hazipandi.

WANAOATHIRIKA NI KINA NANI?
 Ingawa kuna maambukizi karibu 8,000, kuna taarifa chache zinazotolewa za wagonjwa walioathirika.

Kesi nyingi zilizothitibishwa zinahusisha watu ama kutoka Wuhan na ambao wamekuwa karibu na walioathirika.

Ugonjwa huo unahusishwa na vyakula vya baharini au wanyama na unadaiwa kuripuka kutoka katika soko linalouza vyakula hivyo Wuhan.

Homa na kifua ndivyo vinavyotajwa kuwa ni dalili kubwa ya kuugua virusi hivyo.

Wagongwa 17 wametajwa kukumbwa na matatizo ya kushindwa kupumua na  11  wamekufa baada ya moyo au figo kushindwa kufanya kazi huku 31 kati  99  wameruhusiwa kutoka hospitalini hadi kufikia Januari  25 mwaka huu.

Watafiti wanasema maambukizi yanaonekana zaidi kwa wanaume wenye umri mkubwa na ambao wanapatiwa matibabu ya magonjwa mengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles