26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi, wanasiasa wamlilia Filikunjombe

IMG_9980Na Agatha Charles

VIONGOZI, wanasiasa na watu wa kada mbalimbali wameeleza kushtushwa na kifo cha aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Ludewa mkoani Njombe kupitia  Chama Cha Mapinduzi (CCM), Deo Filikunjombe.

Mgombea urais anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alisema pamoja na taarifa hizo kumshtua sana, lakini Taifa limepata pigo kubwa ndani ya kipindi kifupi baada ya kuondokewa na wanasiasa wengine mahiri.

“Ni taarifa ya kushtusha sana ya msiba wa mwanasiasa chipukizi na jasiri.. ni pigo lingine kubwa ambalo katika kipindi kifupi taifa limepata, huku bado likiwa na kidonda cha kuondokewa na wanasiasa wengine mahiri, marehemu Celina Kombani, Dk. Abdallah Kigoda na Dk. Emmanuel Makaidi aliyefariki juzi,” alisema Lowassa.

Alisema Filikunjombe alikuwa mbunge mahiri aliyesimama imara kutetea masilahi ya wananchi wa jimbo lake la Ludewa na Watanzania kwa ujumla.

Lowassa alisema mbunge huyo alikuwa mwiba kwa Serikali ya CCM katika kutetea masilahi ya nchi.

“Mfano ni katika kashfa ya Escrow (uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow) ambapo Filikunjombe alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyochunguza kashfa hiyo,” alisema Lowassa.

Lowassa alisema anamwomba Mungu awape moyo wa subira familia, jamaa, marafiki na wananchi wa Ludewa, katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao.

Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, ametoa salamu zake za rambirambi kwa msiba huo akisema ameshtushwa na habari hizo.

“Kama unavyojua namfahamu sana Filikunjombe, alikuwa mbunge mwenzangu katika Bunge lililomaliza muda wake mwaka huu… alikuwa mtumishi hodari, mwaminifu, mwadilifu kwa Watanzania na hasa wananchi wa Jimbo la Ludewa… Hata nilipofanya ziara ya kampeni katika jimbo lake mwezi uliopita nililala nyumbani kwake, hiyo inaonyesha nilikuwa karibu naye…,” alisema Dk. Magufuli.

Dk. Magufuli pia alituma salamu hizo kwa Meya wa Ilala, Jerry Silaa ambaye katika ajali hiyo amempoteza baba yake ambaye alikuwa rubani wa helikopta hiyo, William Silaa.

Naye Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo Filikunjombe alikuwa Mbunge wake, Dk. Thomas Kashillilah, alielezea namna alivyomfahamu Filikunjombe.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Dk. Kashillilah alisema alikuwa na uwezo mkubwa katika kusimamia jambo.

Alisema alimfahamu vizuri Filikunjombe kutokana na kuwa mchapakazi na mtu mwenye kujiamini.

MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta kwa njia ya simu Spika wa Bunge, Anne Makinda, lakini simu zake hazikuwa hewani.

Alipotafutwa msaidizi wa Spika, Herman Berege, alisema haikuwa rahisi kuzungumza na Makinda kwa wakati huo kutokana na kutokuwa katika hali nzuri kufuatia msiba huo.

“Naomba mmwache kwanza Spika, unajua Deo alikuwa ni kama mtoto wake, yaani haamini kilichotokea, hapa alipo analia tu,” alisema Berege.

Mmoja wa wabunge marafiki wakubwa wa Filikunjombe, Zitto Kabwe, alipotafutwa na gazeti hili kwa njia ya simu alishindwa kupokea na badala yake alijibu kwa ujumbe mfupi.

Ujumbe huo ulisomeka; “Nimepoteza rafiki, nimepoteza ndugu, nimepoteza mtu mtiifu kabisa niliyewahi kuwa naye, sina cha kueleza zaidi, Mungu ana mipango yake,” alisema Zitto.

Itakumbukwa kuwa Zitto na Filikunjombe walikuwa marafiki wakubwa na walifanya kazi pamoja kwa ushirikiano ndani na nje ya Bunge.

Wote wawili waliongoza Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), moja kati ya kamati zilizokuwa na nguvu, Zitto akiwa Mwenyekiti na Filikunjombe Makamu wake.

PAC pamoja na mambo mengine mwaka jana iliwasilisha bungeni maoni yake kuhusu ripoti ya uchotwaji wa zaidi ya shilingi bilioni 300 katika Akaunti ya Tegeta Escrow na kutaja majina ya wahusika.

Kabla ya zoezi hilo, Filikunjombe akiwa na Zitto pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, walikesha nje ya Ofisi za Bunge mjini Dodoma ili kuhakikisha ripoti hiyo haiibwi na vigogo waliokuwa wakiinyemelea.

Itakumbukwa kuwa sakata la Escrow liliwaondoa madarakani aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Anna Tibaijuka, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kipindi hicho, Andrew Chenge, aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Naye mbunge mwingine ambaye pia alikuwa rafiki wa karibu na marehemu Filikunjombe kiasi cha kumsimamia katika harusi yake, David Kafulila, alisema atamkumbuka kutokana na namna alivyokuwa akijiamini.

“Binafsi ninaweza kusema kwamba Deo alikuwa rafiki mwenye kujiamini, asiyependa ubabaishaji kwani alikuwa mkali hata kama ukiwa rafiki yake,” alisema Kafulila.

Kafulila alisema marehemu hakupenda mambo yapindishwe na hakujali kuwa alikuwa chama tawala bali alishirikiana na wenzake bila kujali kuwa ni wa upinzani.

“Alikuwa Best man katika harusi yangu, akiwa rafiki yako hakupenda mambo yapindishwe popote, alikubali kunisimamia pamoja na kuwa CCM. Kipindi hicho nilikuwa niko kwenye wakati mgumu, nilikuwa nasimamia suala la Tegeta Escrow lakini alijitoa hakuhofia kuwa nilikuwa upinzani,” alisema Kafulila.

Kafulila alisema pia atamkumbuka marehemu Filikunjombe kutokana na kutetea jambo aliloliona kuwa liko sahihi bila kuhofia upande alioko.

“Nakumbuka siku moja bungeni nilisema: ‘Nchi imebakwa na mafisadi ndiyo maana haiendelei’. Mwenyekiti siku hiyo alikuwa Zungu (Mussa Zungu) hivyo alinitaka nifute kauli. Kesho yake Filikunjombe alifika na kuomba mwongozo wa Spika na kufafanua kauli hiyo namna ‘Nchi ilivyobakwa’ alikuwa anajitegemea na si kufuata mkumbo,” alisema Kafulila.

Mwingine ambaye pia ni mmoja wa makada wenzake ndani ya CCM, January Makamba alipozungumza na gazeti hili aliomba yachukuliwe maoni ambayo tayari alikwishayaandika kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Katika ukurasa huo January alisema: “Siku mbili kabla ya jana, (juzi) Filikunjombe alinipigia simu akitaka tuzungumze kuhusu mikakati ya ushindi wa CCM. Tukaongea kwa saa nzima. Akawa anawahi kwenye shughuli nyingine. Leo naambiwa hatunaye. Siamini. Siamini kwasababu bado nasikia sauti yake kichwani mwangu,” alisema January.

Alisema alimfahamu Filikunjombe tangu mwaka 2010, wakati anaanza kugombea ubunge na ingawa alikuwa hajawahi kukutana naye kabla, lakini alimtafuta na kuomba washauriane kwasababu baadhi ya makada walikuwa wanataka kumwekea mizengwe ili asipitishwe (hata baada ya kushinda kura ya maoni) kwa madai kuwa ni “mhuni”.

“Tukashauriana. Mizengwe ikashindwa. Tukawa marafiki. Kuna siku mapema mwaka huu, alinipigia bila kutegemea akisema kwamba anataka kunipa ‘a portable PA system’ ili niwe naitumia jimboni. Sikuwa nimemuomba wala sikuitegemea. Alifanya kwa mapenzi,” alisema January.

January alisema juzi usiku wakati akitoka Handeni kumzika Dk. Kigoda, habari za ajali ya helikopta ya kampeni ya CCM zilienea kwa kasi, huku wengine wakisema kwamba ndani ya helikopta hiyo yumo Kinana (Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM), Mwigulu, (Mwigulu Nchemba ambaye ni mjumbe wa kamati ya kampeni ya CCM) na hata mwenyewe (January).

Alisema hilo lilimlazimu kufuatilia habari hizo kwa viongozi waliokuwa katika helikopta zote zilizokodishwa na CCM ili kupata uhakika.

“Nikafuatilia viongozi wote waliokuwemo kwenye helikopta zote tulizokodisha rasmi kama chama. Kila mmoja akasema yuko salama. Tukaripoti kuwatuliza wanachama. Tukaomba Mungu tetesi za ajali ya helikopta yoyote ile zisiwe za kweli. Hatukukubaliwa. Tetesi zikathibitishwa kwamba Deo alikuwa na helikopta aliyokodi binafsi tofauti na zilizokodishwa na chama na kwamba ni kweli ilipata ajali na wote waliokuwemo walifariki,” alisema January.

Kwa upande wake mgombea ubunge wa Ukonga (CCM), Jerry Silaa ambaye katika ajali hiyo alimpoteza baba yake aliyekuwa rubani wa helikopta hiyo alielezea masikitiko yake.

“Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa rasmi kutoka kwa timu ya uokoaji imefanikiwa kufika eneo la ajali na kukuta abiria wote na rubani wamepoteza maisha. Nimepoteza Baba na rubani mzuri wa nchi yetu Kapt. William Silaa, nimepoteza rafiki na kiongozi wangu Filikunjombe. Nawapa pole wote waliopoteza ndugu zao. Nawaombea marehemu mapumziko ya amani,” aliandika Slaa.

Silaa aliwashukuru pia walioshirikiana na familia hiyo kusaidia uokozi.

“Namshukuru Rais Jakaya Kikwete, Dk. John Magufuli, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Ernest Mangu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Adelhelm Meru, Kampuni ya Everest Aviation, wabunge, wakuu wa wilaya, Maofisa wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na wote walioshiriki kuwatafuta wahanga wa tukio hili. Tutajuzana taarifa na mipango mingine,” alisema Silaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles