29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi wa Serikali wazungumzia ziara za Rais Samia

Na Esther Mnyika,Mtanzania Digital

Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan katika nchi za Morocco na Saudia Arabia,imeleta manufaa makubwa nchini kwenye sekta mbalimbali ikiwemo mifugo, nishati , ajira na uwekezaji.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 15,2023, jijini Dar es Salaam katika mkutano wa wandishi habari uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali kwa lengo la kuzungumzia mafanikio Rais Dk. Samia aliyofanya katika nchi hizo.

Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano ya Rais Ikulu,Zuhura Yunus,akielezea ziara hiyo iliyoanza Novemba 8-11, 2023, amesema Rais Dk.Samia alishiriki kwenye Jukwaa la Wawekezaji barani Afrika uliofanyika Mracesh, Morocco ambalo lilianzishwa mwaka 2018.

Amesema lengo la kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni kutafuta fedha za ufadhili miradi ya
miundombinu yenye sifa za uwekezaji ili kuhamasisha sekta binafsi ziwe zinachangia na kuwakutanisha wadau mbalimbali.

Amesema mkutano wa Saudi Arabia na nchi za Afrika uliofanyika
Riyadh, taasisi ya kimaendeleo ya Saudi Arabia imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 533 kwenye mataifa ya Afrika ikiwemo Tanzania.

“Kampuni ya Almaray iko tayari kuja nchini kwa ajili ya kuanzisha uzalishaji wa majani kulisha mifugo. Kampuni hiyo imeanzisha mazungumzo na Wizara ya Mifugo.

“Kampuni nyingine ambayo imeonyesha nia ni Salic ambayo inaitwa Crown Agricultural ambayo nayo inalenga kuanzisha uzalishaji wa majani ya kulisha mifugo mradi wa kunenepesha ng’ombe na pia kuuzwa
katika soko la Mashariki ya Kati,” amesema Zuhura.

Amesema katika ziara hiyo, nchi hizo mbili zimetia saini hati za makubaliano kwenye eneo la wafanyakazi wa ndani vile vile kwenye eneo la nishati na Tanzania imefanikiwa kupata mkopo wa dola milioni 32 kwa umeme.

Naye Waziri wa Wizara ya Uvuvi na Mifugo,Abdallah Ulega, amesema ziara anazozifanya Rais zinaleta tija, dunia ya sasa haina haja mpango ya kujifungia inahitaji ushirikiano ili utangaze fursa zinazopatikana katika Taifa lake.

“Tanzania kuna vivutio vya utalii, madini na rasilimali nyinginezo lazima wavitangaze ili waweze kuja kununua na kutalii, hivyo wanatarajia Shirika la Ndege nchini (ATCL) na la Saud Arabia kujenga ushirikiano wa karibu,” amesema Ulega.

Akizungumzia kuhusu kuongeza uzalishaji wa nyama, Ulega amesema Tanzania imeongeza usafirishaji wa nyama kutoka tani 1700 hadi kufikia tani 14000 katika mauzo ya nje nchi ambapo Saudi Arabia kwa mwaka huu wamenunua tani 1400 kwa hivyo wapo tayari kushirikiana na Tanzania.

“Asilimia 80 ya nyama iliyouzwa nje ya nchi ni mbuzi na kondoo, kwa upande wa nyama ya ng’ombe bado haijakidhi ubora na kuna changamoto, tunahitaji mjadala kwa sababu mifugo ni utajiri lazima iende sokoni kwa sababu inachangia asilimia saba ya pato la Taifa,”amesema.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Fedha na Mipango Zanzibar, Dk. Saada Mkuya, amesema ziara zinatoa fursa ya kukutana na wawekezaji na mashirika mbalimbali ambayo wanashirikiana nayo katika kutekeleza miradi ya fedha nchini.

Akielezea mradi wa bandari ya Mwangapwani ambayo ni bandari jumuishi amesema itakuwa ya makontena, mafuta na gesi,sehemu ya abiria pia kutakuwa na eneo chelezo la watoa huduma za meli.

“Tunavyojua nchi kama Zanzibar uchumi wake unategemea mafanikio ya bandari kwa hiyo kwetu sisi katika miradi ambayo ni kipaombele ni bandari pamoja na miundombinu kwa hiyo tunaanza na bandari ya makontena na mizigo,” amesema.

Amesema kupitia mradi huo watatengeneza ajira 200 za moja kwa moja kwa sababu itakuwa inahusisha matumizi ya makubwa ya mashine lakini pia inatarajia kutoa ajira zipatazo 1000.

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshawekeza karibu Dola milion 35 kwa ajili ya kuweka miundombinu ya msingi, serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ambazo zitakuwa zinaingia ndani ya bandari yetu, ” Amesema Waziri Mkuya.

Amesema tayari wameanza upembuzi yakinifu kwaajili ya ujenzi wa ungwe ya kwanza ya bandari na tayari ambayo tayari Dola mlion 450 zimetolewa.

Akizungumzia suala la wafanyakazi za ndani nchini Saudi Arabia kutoka Tanzania,Balozi wa Tanzania nchini humo,John Kilima, amesema habari za watanzania wanaofanya kazi katika nchi hizo kuwa wanateseka sio kweli.

Amesema mashariki ya kati kwa kiasi kikubwa ni tegemezi ya nguvu kazi kutoka nje takwimu za idadi ya watu wa nchi hizo.

“Ukienda UAE inakwenda mpaka kufikia asilimia 50 ya idadi ya watu ni wageni sasa hili linaonyesha kabisa kuwa wenzetu ni wategemezi wa nguvu kazi kutoka nje ya eneo lao, nguvu kazi za aina zote.

“Kumekuwa na swala ambalo limejengeka kupitia mitandao ya kijamii lakini pia ikiwemo vyombo vya habari kwamba watu wengi wanateseka wakiwa uarabuni, naweza kusema ni asilimi 92 habari hizi si za kweli, ni kwamba wapo watu wanafanya kazi katika mazingira mzuri na kipato wanachopata ni kikubwa,” ameeleza.

Balozi Kilima amesema Oman ina watanzania 25000 ambapo kati yao zaidi ya 17000 wanafanya kazi za ndani,hivyo uwepo wao kwa wingi ni ushahidi tosha kwamba wanafanya kazi katika mazingira mazuri.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC),Masanja Kadogosa amesema ujenzi wa reli kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro umekamilika kwa kiasi kikubwa ukiacha na sehemu chache ambazo bado hazijakamilika kwa mfano katika eneo la Vingunguti na Banana.

“Kitu ambacho kilikuwa kimetusimamisha kwa muda ni vichwa, tulikuwa hatujapata vichwa sasa hilo linaweza likawa na maelezo mengi sana kwa nini vichwa vimechelewa, lakini tumekuwa na changamoto hiyo ya kutokupata vichwa vya treni ,“ amesema Kadogosa.

Amesema kwa sasa TRC wako katika hatua ya kuvifanyia majaribia vichwa hivyo katika hatua mbili ili kupima ufanisi na mwendo wa kusafiri kwa mwendo wa kilomita moja kwa saa.

Akizungumzia sula la uwekezaji Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) , John Mnali, amesema suala la uwekezaji kila nchi ina taratibu za uwekezaji.

“Suala la kutafuta uwekezaji ni suala la ushindani, TIC tunapata njia rahisi kuleta wawekezaji ambapo Januari hadi Septemba miradi 137 ilisajiriwa ukilinganisha na miradi 89 iliyokuwepo mwaka jana takribani ajira 12000 ziliongezeka,” amesema Mnali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles