Viongozi wa dunia wamcheka Rais Trump akihutubia UNGA

0
931

NEW YORK, MAREKANI


RAIS wa Marekani, Donald Trump alilazimika kukabiliana na pengine moja ya nyakati dhalilishi zaidi kwa Rais wa Marekani mbele ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) baada ya viongozi wa dunia kumcheka wazi kwa kejeli.

Akizungumza katika hotuba yake ya mara moja kwa mwaka katika UNGA, Trump alijigamba kwamba utawala wake umepata mafanikio makubwa kwa kipindi kifupi kuliko utawala wowote ule katika historia ya taifa hilo.

Kauli hiyo ikaitikiwa kwa kicheko cha pamoja karibu ukumbi mzima na Rais Trump kulazimika kuangaza kabla ya kutabasamu kana kwamba kauli yake hiyo ililenga kuzua kicheko.

“Sikutegemea mwitikio huu, lakini hakuna shida,” Rais Trump alisema.

Kwa muda mrefu, Trump amekuwa akidai watangulizi wake walikuwa dhaifu kiuongozi hali iliyosababisha mataifa mengine kuicheka Marekani.

Baadhi ya viongozi pia waliguna wakati Trump alipotoa kauli; “tunakataa itikadi ya utandawazi na alipokosoa mataifa kama Ujerumani kwa kukubali kuingia makubaliano ya bomba la mafuta na Urusi.

Wakati Trump alipoukosoa usoshalisti, ujumbe kutoka Sweden ulikunja uso na kutoa mfyonzo mkali kuonesha kutokubaliana naye.

Trump pia alitambia uchumi wa Marekani na ukuu wake wa kijeshi, ambao unaonwa kutokuwa na nafasi katika dunia ya sasa ya maridhiano.

Trump alisema amemwagiza Waziri wa Mambo ya Nje, Mike Pompeo kufuatilia kwa karibu misaada ya kigeni, akisema Marekani ni mfadhili mkubwa zaidi duniani lakini inachopokea hakiendani na inachotoa.”

Alisema upitiaji huo utaangalia nini kinasaidia na nini hakisaidii na iwapo nchi zinazopokea misaada zina maslahi kamilifu kwa Marekani au unafiki.’

Trump alisisitiza taifa lake litatoa misaada ya kigeni kwa mataifa yanayoiunga mkono na kuiheshimu wazi wazi na ambayo ni rafiki wa kweli.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here