Ramadhan Hassan- Dodoma
VIONGOZI wa dini wameishauri Serikali kugharamia gharama za bima ya afya kwa kila Mtanzania ili apate matibabu ya uhakika pindi anapoumwa.
Hayo yalielezwa jijini hapa jana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Canon Matonya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ripoti iliyotolewa na Kamati ya Viongozi wa Dini kuhusu bima ya afya iliyoboreshwa (CHF).
Matonya ambaye ni Katibu Mwenza wa Kamati hiyo, alisema suala la bima la afya bado ni changamoto kubwa kutokana na watu wengi kutokuwa na bima.
Alisema kutokana na hali hiyo, ni vyema Serikali ikajitahidi kila Mtanzania awe na bima hiyo ili anapoumwa aweze kwenda hospitali haraka,ugonjwa haupigi hodi.
Alisema kutokana na utafiti walioufanya kwa muda wa mmoja, wamebaini mambo mbalimbali, ikiwamo wastani wa uchangiaji sekta ya afya umeonyesha Serikali inachangia asilimia 35,wadau wa maendeleo asilimia 37 na watoa huduma binafsi asilimia 28, jambo linaloonyesha utegemezi mkubwa katika vyanzo vya nje vya bajeti
Naye Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Sheikh Kasusu Mvumbo alisema afya ni suala muhimu kwa mwanadamu yoyote, wao viongozi wa dini wana jukumu kubwa kuhamasisha waumini kujiunga na bima ya afya iliyoboreshwa
Mratibu wa CHF kutoka Ofisi Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk.Boniface Richard alisema Serikali imejitahidi kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya kwa wananchi na bima ya CHF, iliyoboreshwa imeboreshwa zaidi kwa kupanua wigo wa matibabu kwa mchangiaji.