Na Brighiter Masaki, Mtanzania Digital
Naibu Waziri wa Afya Dk. Godwin Mollel, amewataka viongozi wa dini kutumia nafasi yao katika jamii juu ya utekelezaji wa dawa kinga ya virusi vya Ukimwi.
Akizungumza leo Agosti 17, Dar es Salaam wakati aliposhiriki kikao cha Uraghibishaji (Advocacy) juu ya utekelezaji wa dawa kinga ya virusi vya Ukimwi kilichojumuisha viongozi wa dini nchini Tanzania.
Dk. Mollel amesema kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuwa mfano katika jamii kwa jambo lolote na si kupotosha watu juu ya ukweli unaosemwa na wataalaam wa afya.
“Viongozi wa dini mnatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuendelea kuelimisha jamii dhidi ya kujikinga na virusi vya Ukimwi.
“Kati ya watu ambao wanaweza kuongea kitu na kufika kwa haraka ni viongozi wa dini, hao wanamchango mkubwa sana katika jamii ni wadau wa karibu zaidi na serikali katika utekelezaji na ufuatiliaji wa udhibiti wa maambukizi mapya,”amesema.
Ameongeza endapo viongozi wataonyesha utofauti na wataalam wa afya watamfinya kidogo ili heshima iwepo haiwezekani madaktari waache kufanya tafiti za dawa na kuangalia aina ya virusi waanze kujibu tuhuma za kwenye mitandao.