23.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 3, 2023

Contact us: [email protected]

Viongozi wa dini wanena mazito kwenye mazishi ya JPM

Na Allan Vicent, Chato

Maaskofu wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo na Shekhe Mkuu wa Tanzania (Mufti) Abubakar Bin Zuberi wamemwelezea hayati Rais Dk. John Magufuli kuwa kiongozi aliyekuwa na uthubutu mkubwa, mcha Mungu na mwenye maono makubwa ya maendeleo.

Wakizungumza katika ibada ya mazishi yake iliyofanyika jana katika uwanja wa Magufuli ulioko wilayani Chato mkoani Geita walisema kuwa Rais Magufuli alikuwa kiongozi aliyejitoa kuwatumikia wananchi, hakuwa na tamaa na hakutanguliza maslahi binafsi katika utendaji wake.

Askofu Renatus Nkwande wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza alisema kuwa hayati Magufuli mara zote alisimama na kutetea wanyonge, hakupenda kuona wananchi wake wakinyanyasika au kutendewa yasiyofaa.

Alisisitiza kuwa Kiongozi huyo alimtanguliza Mungu katika kila jambo, hakuangalia elimu yake, hili lilimpa ujasiri mkubwa wa kuwatumikia Watanzania pasipo ubaguzi, hivyo akawataka viongozi waliopewa dhamana kuiga mfano huo.  

‘Viongozi mliopo madarakani mtangulizeni Mungu katika utendaji wenu, msiruhusu mambo yasiyofaa katika nchi yetu, ushoga, ndoa za jinsia moja, utoaji mimba na kubadili jinsia, haya hayafai ni chukizo mbele za Mungu’, alisema.  

Askofu Nkwande alilitaka bunge kutoruhusu mijadala ya namna hiyo kwa kuwa Bunge ni mahali patakatifu, alisisitiza kulinda heshima ya nchi na kutoiga mambo yanayofanywa na mataifa ya Magharibi bali wamtangulize Mungu mbele kwa kuwa hakuna maendeleo pasipo mkono wa Mungu.

Aidha alimwomba Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kusimama imara na kutoruhusu mambo yasiyofaa katika nchi yetu ikiwemo ushoga, ndoa za jinsia moja au kubadili jinsia.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Askofu Flavian Kassala alibainisha kuwa hayati Magufuli alitumia dhamana yake ya uongozi kwa manufaa ya wananchi, hivyo akawataka viongozi waliobaki kuiga mfano huo.

Aliahidi kuwa TEC itaendelea kumpa ushirikiano unaostahili Rais Samia Suluhu ili aweze kutekeleza wajibu wake wa kuwaletea maendeleo Watanzania ipasavyo.

Mwakilishi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Askofu Alenikisa Cheyo alisema maendeleo makubwa tunayoyaona leo yametokana na ubunifu, bidii ya kazi na kumtanguliza Mungu, hivyo akataka viongozi wote kufuata nyanyo hizo.

Naye Mufti wa Tanzania Shekhe Abubakar Bin Zuberi alisema kuwa hayati Rais Magufuli aliwaunganisha watanzania wote na alikuwa mstari wa mbele kusimamia maendeleo ya wananchi na kuhamasisha ujenzi wa misikiti na makanisa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles