30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Viongozi wa dini wampa neno JPM

Andrew Msechu na Aziza Masoud – DAR ES SALAAM

VIONGOZI wa dini wa madhehebu mbalimbali waliokutana wametoa rai na pongezi kwa Rais Dk. John Magufuli, wakimwomba atoe mwanya wa demokrasia na kusimamia sera za maendeleo alizoziasisi.

Akizungumza katika mkutano wa Rais Magufuli na viongozi wa dini Ikulu Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Wachungaji ya Umoja wa Makanisa, Mchungaji Amani Lyimo (KKKT), alisema Watanzania wengi wana hofu na hawawezi kuzungumza kwa sababu ya kuminywa kwa demokrasia.

Kutokana na hali hiyo, alimwomba Rais Magufuli kuwapa watu nafasi ya kuzungumza kwa sababu mwisho wa siku watu hawatachagua maneno bali watachagua kazi aliyofanya kiongozi huyo.

Alisema ni wazi kwamba kwa sasa japokuwa watendaji wake hawamwambii ukweli, Watanzania wengi wana hofu, hawathubutu kuzungumza licha ya kuwa anafanya mambo mengi mazuri.

“Kwa kazi unayoifanya hawatachagua maneno, watachagua kazi, kama kuna uwezekano waachie pumzi wazungumze, ninajua hawawezi kukushinda kwa maneno yao kwa kuwa utawashinda kwa kazi yako,” alisema.

Alitaka pia kuwe na kamati maalumu itakayoangalia usajili wa madhehebu kama ilivyokuwa kipindi cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere ambapo kabla dhehebu jipya kusajiliwa, kamati hiyo ilikuwa ikijadili kwanza na kutoa ushauri wake.

Kuhusu Wizara ya Elimu, aliipongeza akisema pamoja na kutoa elimu bure, ipo haja ya kuruhusu michango ya wazazi pale wanapokubaliana kupitia kamati zao za shule, lengo likiwa kuboresha maeneo yenye udhaifu.

Aliitaka wizara hiyo pia kuangalia suala la mikopo ya elimu ya juu kwa jicho la pili hasa kwa watoto wa masikini wasio na uwezo.

“Ninampongeza Joyce Ndalichako (Waziri wa Elimu) kwa kuimudu wizara yake, lakini kwa elimu ya juu kuna watoto wengi wa masikini wasio na uwezo wamekosa mikopo na kushindwa kuendelea na masomo.

“Hivyo ninaomba Bodi ya Mikopo iliangalie hili. Hata sisi viongozi wa dini mkishindwa tutawasaidia, pia kuweze kufanyika uchunguzi maalumu maana kuna wenye uwezo wa kulipa, lakini bado wanapata mikopo,” alisema.

PILI ABDALLAH

Mwenyekiti wa wanawake wa Kiislamu Mkoa wa Dar es Salaam, Pili Abdallah, aliwaomba mawaziri kuwa na mazoea ya kukutana na viongozi wa dini ili kuwa na uhuru wa kuwaeleza masuala mengi ya kitaifa.

Alisema kuna masuala ambayo hayafai kuzungumza moja kwa moja na Rais, hivyo itakuwa rahisi kuyazungumza wakikutana na mawaziri.

“Rais ninaomba mawaziri nao waonane na viongozi wa dini kwa wakati wao kama ulivyokutana hivi, mawaziri wakiita vikao kama hivi tutaweza kuzungumza nao mengi kwa sababu baba (Rais Magufuli) unatisha, siyo rahisi mtu kuropokaropoka, tunaweza tukawa na mengi lakini tukayafichaficha,” alisema.

MTUME JOSEPHAT MWINGIRA

Kiongozi wa Kanisa la Efatha, Mtume Josephat Mwingira alimtaka Rais kuangalia utaratibu wa kupunguza mamlaka ya wakuu wa wilaya, hasa katika suala la kutoa amri za kuweka watu ndani kwa saa 48, kwa kuwa wanatumia madaraka hayo vibaya na kuidhalilisha Serikali, hivyo kusababisha wananchi kuiona ni mbaya.

Mtume Mwingira alisema viongozi hao wa wilaya wamejipa mamlaka ya kupitiliza kwa kuwakamata watu na kuwaweka ndani, akitolea mfano wachungaji wa kanisa lake wawili aliosema kuwa wamewahi kukamatwa.

Alisema kuwa wakuu hao wa wilaya wanavuka mipaka na kwenda mbali mno.

“Unamuweka tu ndani halafu baadaye humfungulii mashtaka wala nini, unamwacha unaenda. Umemdhalilisha, mimi naona kama wanaidhalilisha Serikali.

 “Wakamkamata mchungaji wangu, wa kwanza wakamtia ndani, nikauliza mkuu wa mkoa inakuwaje (bila kumtaja mkuu wa mkoa aliyemuuliza), mkuu wa mkoa akampigia simu mkuu wa wilaya akamwachia, unamuweka mtumishi wa Mungu ndani!

“Haya, mwingine ni yule wa Sengerema akamuweka mchungaji wangu ndani, nikamuuliza ananiambia ndiyo nimemuweka. Akaenda mbali na kubomoa na kanisa, ukifuatilia tu kuna mtu ana pesa zake anataka hilo eneo, aah sasa hapa, nikamuuliza unataka tuione Serikali yetu ni mbaya au?” alisema.

Mtume Mwingira pia alimshauri Rais Magufuli kuwa ni vyema kujenga utaratibu wa kuwaita mapema viongozi wa kidini kabla hajazipeleka sera zake kwa wananchi ili wajadiliane kwa pamoja kwakuwa akifanya peke yake inakuwa vigumu kufanikiwa.

 “Utaratibu wa miundombinu ya taifa letu kidogo inaleta kizungumkuti, hatuna mipango endelevu, kila siku utasikia watu wanavunjiwa nyumba, vibanda vyao, ni vizuri watu wa barabara, umeme, maji, simu, wakae pamoja wajue namna ya kufanya kazi zao, tuwe na mikakati iliyo bora,” alisema.

ZAINUDIN ADAMJEE

Makamu Mwenyeketi Jumuiya ya Mabohora, Zainudin Adamjee ameonesha kukerwa na mchezo wa kamari ambao vijana wengi wamekuwa wakiucheza na kupoteza muda badala ya kujishughulisha na shughuli nyingine za kuwaingizia kipato.

Kikubwa ni kwamba kamari ni haramu, lakini hapa nchini vijana wanacheza kamari nje nje kupitia mitandao badala ya kufanya kazi, utaona hata kwenye Tv matangazo yanarushwa, kila ukiwasha mara utasikia tatu mzuka.

“Kila siku wanacheza kamari wakifikiria watatajirika halafu wanaposhinda wanapewa zawadi na mkuu wa mkoa au wa wilaya, hivyo tatizo kubwa sasa ni nguvu kazi kubwa inacheza kamari zaidi kuliko kufanya kazi,” alisema.

CHARLES KITIMA

Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Charles Kitima alipongeza jitihada za Serikali na kugusia suala la ajira akiwataka watendaji wa wizara mbalimbali kukaa na wazazi kujadiliana namna ya kuunda ajira kwa vijana.

Aidha alisema kuwa wao kama viongozi wa dini wanapinga ndoa za jinsi moja kwa sababu hakutakuwa na dunia maana wawili hao hawana uwezo wa kuzaa, hivyo maana yake dunia itakwisha.

HAIDAR KAMWILI 

Mkurugenzi wa Hija Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Haidar Kamwili, alisema kumekuwa na usumbufu kwa vijana wanaopata ufadhili wa masomo nje ya nchi, ambao huzuiwa bila sababu za msingi wanapofika uwanja wa ndege hata kama wana barua na vibali vinavyowaruhusu kusafiri.

“Vijana wetu wanapopata fursa ya masomo nje ya nchi wakifika katika uwanja wa ndege wanawekwa rumande kwa siku hata mbili, hata kama wana barua halali za kuwaonesha kuwa wana kibali.

“Wakati mwingine wanashindia mikate, hivyo ni bora kama kutakuwa na tatizo wakaambiwa maana wengine wanapelekwa hata sehemu wasizozijua,” alisema.

ASKOFU ALINIKISA CHEYO

Askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Kusini Magharibi, Alinikisa Cheyo, amemtaka Rais Magufuli kutoa nafasi za ajira kwa vijana kwani kutofanya hivyo kunaweza kuwasababisha kuingia katika mambo maovu.

Alisema wapo baadhi ya wahitimu ambao fani walizosomea zinawaruhusu kujiajiri bila matatizo yoyote, lakini wapo pia wahitimu ambao fani zao haziwaruhusu kufanya hivyo.

“Tayari umeshaondoa watumishi hewa, walio na vyeti feki, ni jambo ambalo linapaswa kusifiwa na kujivunia kama nchi, hivyo umefika wakati sasa wa wewe kuwaangalia vijana wetu waliohitimu.

 “Wapo vijana wengi ukienda vijijini utakuta wamemaliza vyuo lakini hawana kazi yoyote ya kufanya, angalau hata sisi tuliosoma wakati wa awamu ya kwanza tulifundishwa namna ya kujitegemea bila kuajiriwa,” alisema Askofu Cheo.

ASKOFU JOSEPHAT GWAJIMA

Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, amepinga kauli ya Mchungaji Lyimo kwa kusema kuwa si sahihi kusema kusiwe na madhehebu mengi kwani madhehebu yanayohubiri dini sawasawa ni baraka kwa nchi na kwamba ikiwezekana yaongezeke lakini wahubiri wahubiri kinachotakiwa.

Pia aliitaka Serikali kujenga maeneo maalumu ya kuabudia katika sehemu za kazi na maeneo mbalimbali ambayo watu watahitaji huduma hiyo ikiwemo viwanja vya ndege.

“Katika viwanja vya ndege wenzetu Waislamu wana maeneo ya kuabudu, lakini Wakristo hatuna maeneo hayo kwani hitaji hili ni kwa wote, sio kwamba sisi tunaabudu mara moja kwa wiki, bali tuna ibada za rohoni kila wakati,” alisema.

SHEIKH HASSAN CHIZENGA

Katibu wa Baraza la Ulamaa la Bakwata, Sheikh Hassan Chizenga, alisema hatua ya Rais Magufuli kuwajali watu wa hali ya chini inaonesha kuwa yeye ni madini bora yenye thamani kubwa.

Sheikh Chizenga alisema miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakiwatatiza ni mfumo wa vyeti vinavyotolewa na Wakala wa Usajili , Ufilisi na Udhamini (RITA) kutotosheleza haja zao.

Alisema kuwa dini yao inaruhusu kuoa mke zaidi ya mmoja, lakini mfumo wa RITA hautambui hilo, suala aliloomba liangaliwe upya.

 “Kutokana na mahitaji yetu ya kidini tumejikuta vyeti vya ndoa vinavyotolewa na RITA havitoshelezi haja zetu sawa sawa, hivyo tukaamua kutengeneza vyeti vyetu.

“Tunapata tabu sana kwa sababu watu tunaowafungisha ndoa kutokana na mahitaji yetu, kuna mahali wakienda hawatambuliwi na hawapati haki zinazowastahili watu wenye ndoa. Tunaomba mfumo huo uangaliwe upya,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,396FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles