LEONARD MANG’OHA – DAR ES SALAAM
SHIRIKISHO la viongozi wa dini nchini, limehoji kukosekana viongozi wanawake mashuhuri nchini tofauti na ilivyokuwa kwa Bibi Titi Mohamed, Getrude Mongella na Asha Rose Migiro waliofahamika kitaifa na kimataifa.
Pia shirikisho hilo linaloundwa na Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Baraza la Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) limehoji ushiriki mdogo wa wanawake katika nafasi za kuchaguliwa kuongoza nchi ngazi ya kitongoji, kijiji, kata na taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu TEC, Padre Charles Kitima, alisema wakiwa kama viongozi wa dini, hawajui ni nani ambaye kwa sasa anaonekama ni kielelezo na kinara wa kitaifa na kimataifa kwa kina mama.
Alisema kutokana na hali hiyo wanaona umuhimu wa kuwaleta kina mama pamoja wajitambue na kuchukua nafasi yao na kujipanga vizuri ili washiriki kwa haki na kwa uwezo wao katika fursa za kuongoza nchi yao.
“Ifike mahali Watanzania wote tuseme huyu mama anaweza, na inaonekana wana moyo fulani wa kupenda maendeleo yanayomvuta kila mtu, labda kwa sababu ya majukumu yao ya kifamilia wanaona umuhimu wanaposhika nafasi wanaangalia nchi na jamii yote.
“Hata ukiangalia katika tafiti zilizofanywa, kina mama ambao labda wako kwenye ufisadi ni wachache, ni ule moyo wao wa kupenda maendeleo shirikishi, maendeleo ya wote.
“Kwa hiyo tumeona huu ni mtaji kwetu kwa sababu sasa hivi taifa letu linahitaji viongozi makini, wanaojali vijana, wanaojali watoto. Kina mama kwenye nchi yetu ndio wanaobeba mzigo mkubwa wa kulea familia kiuchumi,” alisema Padre Kitima.
Alisema utafiti walioufanya wamebaini kuwa wanawake wengi bado wanahitaji kujengewa uwezo wa kujiamini kwamba wanao uwezo wa kugombea nafasi mbalimbali na kuchaguliwa na kutoa mchango wao katika kuendeleza nchi.
Kutokana na hali hiyo, alisema wameamua kuratibu mafunzo ya siku mbili kwa wanawake wapatao 100 kutoka madhehebu mbalimbali ili kuwajengea uwezo na kuwaonyesha fursa ya kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za kuchaguliwa.
Padre Kitima alisema mafunzo hayo yanayoanza leo, pia yatashirikisha wadau mbalimbali ikiwamo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), taasisi na mashirika mbalimbali.
Alisema ni lazima kuwa na jamii inayompa kila raia fursa ya kushiriki kuongoza kwa sababu Watanzania zaidi ya milioni 55 lazima wapate wachache wawaongoze ili wafikie hatima ya mafanikio ya nchi yao.