Sharifa Mmasi, Mtanzania Digital
BAADA ya waliokuwa viongozi wa Chama cha Mpira wa Kikapu Zanzibar (BAZA), kujitokeza hadharani jana Jumanne Septemba 7, kumpinga Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita, aliyetangaza kuvunja uongozi huo na wahusika kudai kuwa wataendelea na majukumu yao kama kawaida, sasa uzalendo umewashinda hivyo wameamua rasmi kuachia ngazi.
Akizungumza na Mtanzania Digital aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa BAZA, Rashid Hamza amesema, wamekubaliana kuachia madaraka hayo baada ya malengo yao kutimia.
Rashid aliendelea kusema kuwa, jana Jumanne waliamua kutangaza hayo (Hawataachia madaraka) kwakuwa, walitaka familia ya kikapu ijue kinacho endelea na kwamba, alichokifanya Waziri huyo hakikuwa sahihi hivyo tayari ukweli umejulikana hawana tena sababu ya kuongoza.
Ikumbukwe kuwa, Waziri Tabia alitoa sababu ya kuvunja uongozi huo kwa mujibu wa katiba 47 (2) inayoeleza kwamba, BAZA itafanya uchaguzi mkuu kila baada ya miaka minne na ulipaswa kufanyika mwaka jana lakini haikuwa hivyo na kwamba hawana uhalali wakuendelea kukaa madarakani.