24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

VIONGOZI NA WANAHABARI HUTEGEMEANA

Wanahabari wakiwa kazini

 

 

Na Balinagwe Mwambungu,

NIMETAFUTA kwenye Kamusi ya TUKI iliyochapishwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, maana ya ‘Black Out’ sikuiona. Tafsiri yangu ya karibu ni uwepo wa giza au kukosekana kwa mwanga. Lakini katika fani ya uandishi wa habari ni kutotangazwa (news black out) au kutoandikwa popote (magazetini) au kwenye machapisho au kususiwa na vyombo vya habari.

Kwa tasnia ya habari, black out ni kitendo cha kuzuia habari inayomhusu mtu au taasisi zisiandikwe au kutotangaza mambo anayoyafanya mtu fulani (maarufu) au yanayofanywa na taasisi fulani.

Aidha, black out inaweza kufanywa na mtu maarufu kukataa kutoa habari kwa kwa vyombo fulani au vyote kutokana na sababu mbalimbali. Wakati wa vita kwa mfano, Serikali huzuia kutangaza habari zozote zinazotoka uwanja wa vita, mpaka ziidhinishwe na wenye mamlaka. Au Serikali inakataza habari zake (hasa) mbaya zisitangazwe kwa sababu ni zenye madhara kwa jamii au nchi.

Kwa hiyo, black out ni kama shilingi; ina sura mbili. Upande mmoja ni Serikali na taasisi, kampuni, vyama na mashirika. Upande wa pili ni vyombo vya habari kwa ujumla. Kwa upande wa kwanza ni rahisi kuamua au kukataza taarifa zake, nzuri au mbaya zisitangazwe au kuandikwa kwa sababu hautaki zijulikane.

Aina moja ambayo Serikali (dunia nzima) huzihifadhi kama habari za siri (classified information), zinajulikana kwa watu wachache. Ndani ya Serikali wanazijua watu wachache wenye ngazi fulani. Hawa huwa wanakula kiapo cha kutunza siri za Serikali.

Kama mawasiliano ni kwa njia ya barua, basi neno ‘siri’ hugongwa juu ya bahasha na kwenye barua yenyewe juu na chini.

Katika nchi za Kiafrika, neno siri hutumiwa vibaya kuficha vitendo vibaya au mipango mibovu, hujuma na maamuzi yasiyo na tija kwa nchi na wananchi wake. Ni usiri huo ndio unaowafanya wanahabari wazitafute siri hizo kwa siri na kuzianika hadharani.

Chombo cha habari kama hicho, kwa kawaida huwa si rafiki kwa waficha siri na huwa kinasuswa (black listed) na wenye madaraka.

Lakini Serikali inaweza pia kuzuia vyombo vya habari kutangaza jambo ambalo dunia nzima inalijua kwamba litatendeka. Kwa mfano, Serikali ya China ilizuia kutangaza habari za kumbukumbu ya miaka 20 ya maandamano yajulikanayo kama Tiananmen Square ya mwaka 1989, ambapo watu takribani milioni moja; wengi wakiwa ni wanafunzi waliuliwa na jeshi la nchi hiyo. Wanafunzi hao walikuwa wameiteka Barabara ya Tiananmen wakidai mabadiliko ya kidemokrasia.

Serikali nyingi za Kiafrika pia huzuia vyombo vya habari kutoa taarifa za moja kwa moja wakati wa uchaguzi mkuu. Hapa Tanzania, ni msimamizi wa uchaguzi tu anayeruhusiwa kutoa matokeo ya kura, isipokuwa kura za rais.

Vyombo vya habari duniani vikiwa kwa makundi au kwa mtu mmoja mmoja au kwa umoja wao, vinaweza kuamua kumsusia mtu au taasisi kutangaza habari zake. Hii ndio silaha pekee ya wandishi wa habari waliyo nayo. Mara nyingi hapa Tanzania waandishi wamekuwa wakinyanyaswa na viongozi na kuonewa au kupigwa na kujeruhiwa na polisi.

Waandishi walipigwa na Askari Magereza na kujeruhiwa mwaka 2008. Omar Ramadhan Mapuli (marehemu), alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa mwaka 2014, aliwasapoti askari wake, vyombo vya habari vikamsusia. George Mkuchika, akiwa Waziri wa Habari, alisusiwa kwa kipindi cha miezi mitatu, baada ya kulifungia gazeti la MwanaHalisi bila kuwapa wahusika nafasi ya kujitetea.

Aliyekuwa Waziri wa Habari, Fenella Mukangara naye alisusiwa kwa kufungia Radio tano na gazeti la Mawio.

Mwaka huu vyombo vya habari vimemsusia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kufuatia sakata la Clouds Meadia Group.

Kuwafungia viongozi ni njia pekee ya kufikisha ujumbe kwamba wanatuhitaji wao zaidi kuliko sisi. Umaarufu wao katika jamii wanaupata kwa kutangazwa na vyombo vya habari. Wanahabari wanawahitaji viongozi kwa nia ya kuupasha umma habari, lakini nchi inaweza kusimama kama vyombo vya habari vitaamua kutotangaza matukio na hotuba za viongozi.

Lakini kubwa zaidi ni kwamba wakubwa wanatakiwa kubadilika, vyombo vya habari vina uwezo wa kwenda moja kwa moja na kuwapa sauti wananchi ili watoe dukuduku zao. Hawahitaji uwepo wa msemaji au mwanasiasa au mtu maarufu ndipo waandike habari.

Black out si lazima vyombo vyote vitelekeze maagano kwa sababu mbalimbali. Waandishi wa habari wengi hawana vyombo vya kutangazia, ni wajiriwa na hawana nguvu ya kumlazimisha mwenye chombo kususa kutangaza habari za mtu au taasisi.

Ikumbukwe kuwa wenye vyombo vya habari ni wafanyabiashara, kwa hiyo inabidi apime mwenyewe kunyoa au kusuka.

Pili vyombo vingine vina mkono wa Serikali. Viongozi wakuu ni wateule wa Rais. Na vingine ni wateule wa chama tawala. Kiongozi aliyeguswa ni mteule wa Rais kutoka chama tawala. Hayo ndio mazingira ya vyombo vya habari Tanzania.

Katika nchi ambayo Serikali haina vyombo vya habari, vinaweza kususa kuandika habari za mkuu wa nchi hata kama anafanya shughuli za umma, ila utekelezwaji wake ni mgumu kwa sababu ya nipe nikupe.

Umekuwapo ubishi kwamba uamuzi wa vyombo vya habari kususa kutangaza shughuli za Mkuu wa Mkoa zinahujumu haki ya wananchi kupata habari. Ni kweli, lakini wahenga walisema: “Mwenzio akinyolewa, wewe tia maji.” Kwa kuwa leo liko kwa mwenzako, kesho linaweza kuwa kwako. Kulinyamazia sakata la Clouds Media Group ingekuwa sawa na kuisaliti tasnia ya habari na kusema kila mmoja kivyake.

Watu ambao si wanataaluma ya habari wanawazodoa viongozi wa tasnia ya habari, kwa kuwa hawajui ni mambo mangapi ambayo wakuu wa vyombo hivyo wanayavumilia. Kusema wanarukia mambo yasiyowahusu, ni kwa sababu hawajui yaliyoko nyuma ya pazia. Ya Ngoswe mwachie Ngoswe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles