24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi Morogoro wakerwa kasi ujenzi barabara

Ashura Kazinja -Morogoro

KASI ndogo ya ujenzi wa barabara ya Kidatu hadi Ifakara wilayani Kilombero, imewakera viongozi wa Mkoa wa Morogoro na kusema hawaridhishwi na kazi hiyo ambayo kwa sasa imefika asilimia 10 badala ya 90 iliyotarajiwa.

Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Emmanuel Kalobelo, alipotembelea ujenzi wa mradi huo unaojengwa na Kampuni ya ujenzi ya Reynold Construction (RCC) ya kutoka nchini Nigeria, mwishoni mwa wiki, alisikitishwa na ujenzi huo kufanywa kwa kusuasua.

Alisema barabara hiyo ni ya pekee kutoka Ifakara hadi Mikumi inayotegemewa na wananchi wa maeneo hayo, uchelewaji wake unawaathiri kwa mambo mengi wakazi wa maeneo hayo.

“Mradi uko asilimia kumi ya utekelezaji wakati muda umekwisha kwa asilimia 90, hii haisuburi mtu aambiwe kuwa kazi hairidhishi, kazi hii hairidhishi. Na hairidhishi kwa sababu kutoka Mikumi mpaka Ifakara ni barabara hii moja tu, hakuna barabara nyingine inayotegemewa,” alisema Kalobelo.

Alisema matumaini ya Rais Dk. John Magufuli aliyezindua ujenzi wa barabara hiyo, ni mradi huo kukamilika kwa wakati ambao ni ndani ya miezi 36 ili kuwaondolea wananchi kero ya usafiri.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata ole Sanare ambaye amekuwa haridhishwi na ujenzi wa mradi huo, Kalobelo amewaagiza mkandarasi mshauri na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Morogoro, kumsimamia kwa karibu mkandarasi huyo na pale ambapo atakwenda ndivyo sivyo wachukue hatua mara moja.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, James Ihunyo, alisema barabara hiyo imekuwa kero kwa wasafiri na wenyeji wa wilaya hiyo, hususan katika kipindi hiki cha mvua.

“Usiku wa kuamkia Januari 25, mwaka huu karavati moja eneo la Kanolo, Kata ya Kisawasawa lilichukuliwa na maji na kusababisha mawasiliano kukatika kwa zaidi ya saa saba,” alisema Ihunyo.

Naye mhandisi wa miradi wa Tanroads Mkoa wa Morogoro, Salehe Juma, alikiri kuwa hakuna kiongozi yeyote katika ofisi yao anayeridhika na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo na kwamba hadi sasa mkandarasi yuko nyuma ya muda kwa wiki 79, huku akifafanua kuwa taarifa zote na ushauri mbalimbali ulishafikishwa ngazi za juu.

Akizungumza kwa niaba ya mhandisi mshauri wa ujenzi huo, Maburuge Mapambano alikiri mradi huo kuwa nyuma ya wakati, ambapo hata hivyo alijitetea kuhusu ucheleweshwaji wa kazi hiyo kuwa unatokana na ushuru bandarini ambako vifaa vyake vilikwama kwa kipindi kirefu.

Nao Shaban Likulike na Ally Miginga ambao ni wakazi wa Kijiji cha Kanolo wilayani Kilombero, ambacho ni miongoni mwa vijiji vinavyotakiwa kunufaika na barabara hiyo, wameiomba Serikali kumbadilisha mkandarasi huyo kwa kuwa ameonyesha hana uwezo wa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.

Ujenzi wa barabara hiyo inayojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 101, ulizinduliwa na Rais Magufuli Mei, 2018 na umebakiza takribani miezi mitatu kati ya 36 kukamilika, lakini bado ujenzi wake ni asilimia 10 tu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles